HABIBU MCHANGE AWAVUA NGUO CHADEMA SUALA LA MAWASILIANO YA LEMA KUPITIA VODACOM
Nimeona mitandaoni kampeni inaendelea kutuhamasisha watu tusitumie mtandao wa Vodacom. 
Kampeni inasimamiwa na kusambazwa na viongozi na wananchama wa Chama kimoja cha siasa.
Wengine ni wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wanajenga hoja, na kwa kweli hoja wanayo.

Wanasema mtandao huo umeamua kutoa siri za wateja wao ili kusaidia upande wa washitaki wanaomshtaki mbunge na mwanachama wao.
Wanaendelea kusisitiza kwamba tuukatae mtandao huo kwa kuwa Leo wao kesho mimi na wewe.

WANASAHAU HARAKA SANA.
Mwaka 2011 mwezi Mei wakati nashiriki siasa na nikiwa Mwanachama wa Chadema.
Tukiwa katika uchaguzi wa nafasi za uongozi ndani ya Chama kupitia Vijana (Bavicha). Mimi nilikuwa miongoni mwa wagombea wa uenyekiti wa Taifa wa Vijana.
Pamoja na kwamba nilikuwa na nguvu za ushawishi kiasi cha kushinda.  Niliitwa kujieleza katika kikao cha uchujaji wagombea saa saba kasoro dakika 5 usiku.
Nikaenda katika kikao hicho Mbezi Garden Hotel Iliyoko Mbezi.
Pamoja na mambo mengine nilikuta nimetuhumiwa kwa makosa zaidi ya saba kwamba siwezi na sistahili kugombea nafasi Ile ya uenyekiti wa Vijana.
Shitaka langu namba Sita lilikuwa ni kutoa rushwa kwa njia ya simu kupitia M-Pesa.
Godbless Lema alikwenda Vodacom, akaprint muamala wangu wa Vodacom wakachukua mawasiliano yangu yote ya kifedha mpaka niliyowarushia ndugu zangu, rafiki zangu na wazee wangu wakasema niliwatumia pesa wajumbe wa Bavicha.
Wakamuandaa na kijana mmoja aliyeniomba nimkopeshe nauli ili ashiriki mkutano na kwamba akirudishiwa na Chama angenilipa kumbe ulikuwa mtego wakanituhumu nimetoa rushwa.
Wakati John Mrema akisoma miamala yangu katika kikao cha Kamati Kuu,  Mbunge Peter Msigwa alikuwa anarekodi kwa kutumia IPad yake. (Siwezi kulisahau hili tukio maisha yangu yote).
God bless Lema akawa shujaa kwenye hili. Kwamba aliweza kuingilia mawasiliano yangu.
Vodacom hawakuwa wabaya hapa.  Walisifiwa eti wamefichua njama za rushwa.
Hapa hawakujali kwamba mimi naye ni Binaadam na Nina privacy zangu.
Siku mbili baadaye 30.05.2011 Mwandishi Alfred Lucas wa  Gazeti pendwa la MWANAHALISI likaandika MASALIA YA ZITTO YAPUKUTISHWA CHADEMA.
 Gazeti la Mwanahalisi likachapisha miamala yangu yote waliyoiibua kwa rafiki yao aliyekuwa kigogo wa Vodacom.
Mtandao wa Jamiiforums nako wiki nzima habari ikawa miamala yangu ya Vodacom.
Bahati mbaya Sana Siku zinakimbia mno.
Leo LEMA aliyeprint Mawasiliano yangu kunikomesha naye wameprint yake na yuko matatani.
Msigwa aliyekuwa anashangilia na kurekodi kwenye IPad yake naye analalamika mawasiliano ya Lema  kuingiliwa. 
Pamoja na kwamba siungi mkono manyanyaso ya kisheria anayokutana nayo Lema, lakini ni vyema vijana kujifunza kuacha kukurupuka na kulalama hovyo bila kujua msingi wa jambo.
Leo tunajifunza kuwa kuna vitu vinaumiza vikitokea hasa vikitokea kwa upande wetu.
Maumivu niliyoyapata mimi Mwaka 2011 wanaoweza kusema japo kwa uchache ni Godwin Makomba na Emanuel Kidenya.
Rafiki na kaka yangu Zitto Kabwe alitumia nguvu kubwa kunitia moyo na  kunishawishi nisikishtaki Chama changu na Vodacom. Alinitia moyo kuwa "there is always next battle".
Wakili Peter Kibatala nilimshirikisha sana tuwashtaki Vodacom lakini alikuwa ananipiga chenga, kumbe alikuwa anajiandaa kuwa mwanachama hai.
Leo miaka 6 baadaye nikiwa si mwanachama wa chama chochote cha siasa yamewatokea yaliyonitokea.
Nawakumbusha Lema na Msigwa kuwa USILOPENDA KUFANYIWA KAMWE USIMFANYIE MWENZAKO.

Ndimi
Habib Mchange
Mwananchi