Featured Post

DENMARK KUHAMASISHA WAWEKEZAJI KUJA KUWEKEZA TANZANIA

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa kwanza kulia), akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na ujumbe kutoka nchini Denmark, ukiongozwa na Waziri wa nchi anayeshughulikia Sera, Bw. Martin Hermann, walipokutana Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam.
 
 Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.  Dkt. Philip Mpango na Ujumbe kutoka Serikali ya Denmark ukiongozwa na Waziri wa Nchi-Sera, Bw. Martin Hermann, walipokutana kwa mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, Mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Nchi anayehusika na masuala ya Sera, Bw. Martin Hermann (kulia) akiwa na ujumbe wake wakati wa mazungumzo kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (hayupo pichani), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam, ambapo nchi hizo zimekubaliana kuendeleza ushirikiano utakaojikita katika masuala ya uwekezaji na biashara kwa faida ya pande zote mbili. Kushoto ni Balozi wa Denmark hapa nchini Bw. Einar Jansen.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto), akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na ujumbe kutoka nchini Denmark, ukiongozwa na Waziri wa nchi anayeshughulikia Sera, Bw. Martin Hermann, (hayupo Pichani) walipokutana Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James, wakifuatilia kwa umakini mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Waziri wa Nchi anayeshughulika na masuala ya Sera wa Denmark, Bw. Martin Hermann (hawapo pichani), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nchi anayehusika na masuala ya Sera kutoka Denmark, Bw. Martin Hermann (kushoto) akimkabidhi Dkt. Mpango, nyaraka za kampuni zinazoonesha nia ya kuwekeza Tanzania katika Sekta ya Gesi na Mafuta wakati akiongoza ujumbe wa nchi hiyo katika mazungumzo kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kulia), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (katikati) akiangalia nyaraka alizokabidhiwa na Waziri wa Nchi wa Serikali ya Denmark anayehusika na Sera, Bw. Martin Hermann, wakati wa mazungumzo kati yao yaliyojikita katika masuala ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James na kulia kwa Waziri Dkt. Mpango, ni Naibu Katibu Mkuu Dkt. Khatib Kazungu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa pili kushoto) akiwa na wageni wake kutoka Serikali ya Denmark wakiongozwa na Waziri wa Nchi anayehusika na Sera, Bw. Martin Hermann (kushoto), baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati yao ambapo masuala kadhaa yamejadiliwa ikiwemo kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kijamii hususan katika uwekezaji na biashara, mazungungo yaliyofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto) akipeana mkono wa shukurani na mgeni wake kutoka Serikali ya Denmark, Waziri wa Nchi anayehusika na Sera, Bw. Martin Hermann (kushoto), baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati yao yaliyogusa Nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii hususan katika uwekezaji na biashara, mazungunzo yaliyofanyika makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
 
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto) akiwasindikiza wageni wake kutoka nje ya jengo la Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya ujumbe wa Serikali ya Denmark na Tanzania uliolenga kuimarisha uhusiano katika masuala ya uwekezaji na biashara.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM)

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
SERIKALI ya Denmark imeahidi kuwashawishi wawekezaji wakubwa kutoka nchini humo kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Viwanda, Bandari, Gesi na Mafuta.
Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam na Waziri wa Nchi wa Serikali ya Denmark anayeshughulikia Sera, Bw. Martin Hermann, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Makao Makuu ya Wizara hiyo.
Bw. Hermann alielezea kufurahishwa kwake na namna Serikali ya Awamu ya Tano ilivyojipanga kuwatumikia wananchi wake kwa kuwaletea maendeleo ya haraka ya kiuchumi pamoja na kuimarisha uwajibikaji, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, na kusema kuwa nchi yake inaunga mkono juhudi hizo.
Alisema kuwa nchi yake itasaidia juhudi hizo kwa kuzishawishi kampuni kubwa zenye mitaji na uwezo wa kiteknolojia kutoka sekta binafsi ili zije ziwekeze hapa nchini na hivyo kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi.
Amesisitiza pia umuhimu wa serikali kuwekeza juhudi kubwa katika kuendeleza kilimo kwa kuwa sekta hiyo inaweza kuchochea na kutoa mchango mkubwa na wa haraka wa ustawi na maendeleo ya wananchi.
Aidha, Bw. Hermann, ambaye aliambatana na Balozi wa Denmark hapa nchini, Bw. Einar Jensen, amesifu utendaji mzuri wa Rais Mhe. Dkt. John Magufuli katika mapambano dhidi ya vitendo vya ufisadi ikiwemo rushwa na kuishauri Serikali kuweka mfumo wa vita hiyo utakaokuwa endelevu.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alisema Serikali inathamini mchango mkubwa wa Denmark katika kukuza uchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla kwa kusaidia miradi ya maendeleo na ushauri wa kisera.
“Katika kipindi cha zaidi ya miaka 50 ya uhusiano kati ya nchi hizi mbili tumeshuhudia Serikali ya Denmark ikichangia maendeleo yetu katika nyanja zinazokwenda sambamba na vipaumbele vya maono ya mipango yetu ya maendeleo katika sekta za fedha, miundombinu, kilimo, afya na elimu”alisisitiza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango aliishauri nchi hiyo kwamba mwelekeo wa uhusiano huo sasa uwe katika kushirikiana kiuchumi kwa kuhamasisha uwekezaji na biashara kati ya pande hizo mbili.
Alifafanua kuwa amejaribu kutafuta takwimu za kiwango cha uagizaji na uingizaji wa bidhaa kati ya Tanzania na Denmark lakini cha kusikitisha hakuna biashara hiyo jambo ambalo amesema inabidi lilisisitizwe katika mfumo mpya wa ushirikiano kwa kuwa kuna fursa nyingi zinazoweza kusaidia pande zote mbili kiuchumi.
Alisisitiza kuwa mwelekeo huo ni muhimu utiliwe mkazo sambamba na jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini huku akitoa wito kwa kampuni za Denmark zilizopo hapa nchini pia kuvuta kampuni nyingine kutoka nchini mwao kuja kuwekeza Tanzania.
Dkt. Mpango, amewakaribisha wawekezaji hao kuwekeza katika katika sekta za ufugaji wa samaki, ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki, ufugaji wa ng’ombe wa kisasa na viwanda vya kusindika nyama na maziwa, hatua itakayo saidia kukuza mitaji, kuongeza tija katika sekta hizo na  ajira  kwa kundi kubwa la vijana.
Kuhusu ushauri uliotolewa na Waziri wa nchi wa Denmark anaye shughulikia Sera, Bw. Martin Hermann wa kujenga mfumo endelevu wa kupambana na rushwa na ufisadi, Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali imeanzisha mahakama maalumu ya mafisadi ambayo anaamini ni moja ya ujenzi wa mifumo hiyo endelevu ya kupambana na vitendo hivyo.

Comments