DAKTARI MMOJA KUHUDUMIA WAGONJWA 30,000 NI MAJANGA KWA TANZANIA
Na Daniel Mbega, FikraPevu
MWAKA 2016 wakati wa mojawapo ya vikao vya Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Rukwa, wajumbe walizizima kwa muda baada ya kupokea taarifa kuwa daktari mmoja mkoani humo alikuwa akihudumia wagonjwa 200,000.
Uwiano huo ni mara nane ya uwiano unaotakiwa kitaifa wa daktari mmoja kwa wagonjwa 25,000. 
Aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Gasper Nduasinde, aliambia kamati hiyo kwamba, upungufu wa madaktari uliokuwepo ni sawa na asilimia 60 ya mahitaji.

Mkoa huo wenye jumla ya wakazi 1,048,892, kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, una madaktari 10 sawa na asilimia 32 ya mahitaji, madaktari wasaidizi 59 sawa na asilimia 70 ya mahitaji na wauguzi 142 sawa na asilimia 25 ya mahitaji.
Aidha, mkoa huo unaelezwa kwamba una madaktari bingwa wawili, upungufu ambao umekuwa na athari kubwa kwa akina mama wajawazito na watoto waishio kwenye dimbwi la umaskini.
Katika kada ya wauguzi, uwiano wa kitaifa ni muuguzi mmoja kwa wagonjwa 5,000 lakini katika mkoa huo, muuguzi mmoja anahudumia wagonjwa 30,000. 
Na Mkoa wa Rukwa usitegemee kama changamoto hiyo ya uhaba wa madktari itapatiwa ufumbuzi kesho ama keshokutwa hasa kutokana na uamuzi wa serikali wa kutoajiri watumishi wapya.
Licha ya kuwepo kwa upungufu mkubwa wa watendaji katika sekta ya afya, lakini mikoa ya pembezoni, ukiwemo Rukwa, imeleemewa zaidi na uhaba huo kiasi cha uwiano wa watumishi kwa wagonjwa kuwa changamoto kubwa kiasi cha kuwalazimu baadhi ya wananchi wa mikoa hiyo kwenda kutibiwa nchi za jirani kama Malawi na Zambia ambako wanasema huduma zinapatika kwa uhakika.
Uwiano kati ya daktari na wagonjwa nchini Tanzania ni daktari mmoja kwa wagonjwa 30,000, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko uwiano wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa daktari mmoja kwa wagonjwa 1,000.
Aidha, takwimu za WHO zinaonyesha kwamba Tanzania bado ina uwiano mbovu wa madaktari kwa wagonjwa, ambapo kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita ilikuwa inashika mkia kwa kuwa na uwiano wa daktari mmoja kwa wagonjwa 50,000.
Takwimu hizo zilionyesha kwamba, Tanzania ambayo kwa sasa ina idadi ya watu 49.25 milioni, ilikuwa na uwiano sawa na Malawi (yenye watu 16.36 milioni) na ndizo zilikuwa zinaburuza mkia kwa Afrika.
Afrika Kusini, Misri, Congo DRC na Nigeria zina idadi kubwa ya watu, lakini uwiano wa madaktari kwa wagonjwa unaridhisha kama siyo kukidhi kwa kiasi chake.
CHANZO: FIKRAPEVU