Featured Post

WAAJIRI WAAGIZWA KUWASILISHA MAKATO YA FIDIA KWA WAKATI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu          Mh. Jenista Mhagama akiongea na wadau mbalimbali (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi uliofanyika  jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Benjamin Sawe-Maelezo).
Waziri wa  Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mh. Jenista Mhagama akizindua Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Kushoto ni Naibu Waziri Mh. uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Benjamin Sawe-Maelezo).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mh. Jenista Mhagama akisoma ujumbe mara baada ya kuzindua Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Benjamin Sawe-Maelezo).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mh. Jenista Mhagama akikabidhi Tuzo ya Ushiriki kwa mmoja wa wadau waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi uliofanyika jijin Dar es Salaam leo. (Picha na Benjamin Sawe-Maelezo).
Mkurugenzi Mtendaji Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Masha Mshomba akiongea na wadau mbalimbali kabla ya uzinduzi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi uliofanyika jijini Dar es Salaam leo (jana). (Picha na Benjamin Sawe-Maelezo).
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Emanuel Humba akiongea na wadau mbalimbali kabla ya uzinduzi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi uliofanyika jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Benjamin Sawe-Maelezo).
Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi wakimsikiliza Waziri wa Kazi, Mh. Jenista Mhagama wakati wa Mfuko huo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Benjamin Sawe-Maelezo).
Waziri wa  Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mh. Jenista Mhagama  (wanne kutoka kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali baada ya uzinduzi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi uliofanyika  jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Benjamin Sawe-Maelezo).
Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi wakimsikiliza Waziri wa Kazi, Mh. Jenista Mhagama wakati wa Mfuko huo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Benjamin Sawe-Maelezo).
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mh.  Antony Mavunde akiongea na wadau mbalimbali (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi uliofanyika  jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Benjamin Sawe-Maelezo).


Na Ismail Ngayonga
MAELEZO - Dar es Salaam
SERIKALI imewaagiza Waajiri wote nchini kuwasilisha kwa wakati michango ya mafao ya fidia kwa wafanyakazi ili kuwawezesha watumishi wao kupata huduma za matibabu pindi watakapoumia au kuugua wakiwa katika maeneo yao ya kazi.
Agizo hilo limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,  Ajira, Kazi na Ulemavu) Jenister Mhagama wakati alipokuwa akizindua huduma za utoaji wa mafao ya fidia na ubia baina ya mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) na watoa huduma za afya nchini.
Mhagama alisema suala la uchangiaji wa mafao hayo sio la hiari ila lipo kisheria na hivyo ni wajibu wa waajiri wote nchini kuhakikisha kuwa wafanyakazi wao wanaingizwa katika mfumo huo ili kuwawezesha wafanyakazi kuwa na uhakika wa kulipwa fidia pindi wanapokuwa kazini.
“Katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali imelipa michango yote ya wafanyakazi wake, na huu ni mfano unaopaswa kuigwa na waajiri wengine nchini, na natoa rai kwa Chama cha Waajiri Nchini (ATE) na Shirikisho la Wafanyakazi nchini (TUCTA) linasimamia suala hili” alisema Mhagama.
Aidha Mhagama alisema lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo wa wafanyakazi nchini ni kusaidia kutatua kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi wa sekta za umma na binafsi, ambao wamekuwa wakilalamikia huduma hafifu zinazotolewa pindi wapatapo majanga mbalimbali wakiwa kazini ikiwemo ajali na vifo.
Waziri Mhagama alitaka Bodi ya mfuko huo kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria zilizopo ili kuhakikisha kuwa waajiri wote hususani wa sekta binafsi wanawasilisha michango kwa wakati.
Akifafanua zaidi Waziri Mhagama aliuataka mfuko huo kujitangaza zaidi kwa sekta zisizo rasmi ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi hususani wa kipato cha chini kujiunga na mfuko huo na kuwasaidia kufaidi huduma zinazotolewa.
“Natoa rai kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii nchini ikiwemo wa WCF mjitangaze katika sekta zisizo rasmi ikiwemo waendesha bodaboda, akina mama lishe, kwa kuwa idadi yao ni kubwa  na hiyo itawezesha kupata wanachama wengi zaidi” alisema Mhagama.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Masha Musomba alisema hadi kufikia sasa mfuko huo umeweza kutoa usajili  wa waajiri 5945 pamoja na kuendesha mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo watumishi wa mfuko huo ikiwemo madaktari.
Aidha Musomba anasema pia mfuko huo umeingia ubia na taasisi 7 za utoaji huduma za afya nchini, ambazo ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), na Taasisi ya Kansa ya Ocean Road.
Musomba anazitaja taasisi nyingine kuwa ni Strategis, AAR, mfuko wa Jubilee, na Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo taasisi hizo zinazoendelea kushughulikia kesi 189 zilizolipotiwa katika mfuko huo.
Naye Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Nchini (ATE), Aggrey Mwinuka alisema mfumo huo wa fidia umekuja katika wakati muafaka kwa kuwa sheria zilikuwepo katika vitabu na hazikuwa na utekelezaji uliokusudiwa.
Mwinuka alisema ili kuhakikisha kuwa malengo ya mfuko huo yanatekezeka ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kuwa inafanya majadiliano ya mara kwa mara na waajiri ili kuangalia viwango vya makato ya michango ya wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi.
Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo, Emmanuel Homba alisema uwekaji wa mfumo wa mafao ya fidia utawezesha wafanyakazi katika sekta  za umma na binafsi kuchangia kikamilifu katika Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini.

Comments