Featured Post

LOWASSA ANAWEWESEKA, ALISHINDWAJE KUTATUA KERO YA MAJI KWA MIAKA 5?





Na Daniel Mbega
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, sasa ‘anaweweseka’ kwa kukosa hoja zenye mashiko za kuikosoa Serikali ya Awamu ya Tano.
Katika kipindi ambacho Serikali inafanya kila jitihada za kulifufua na kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege, yeye anabeza na kuona kwamba hicho siyo kipaumbele, bali fedha hizo zingetumika kupeleka maji safi na salama vijijini.
Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na vijana wa Chadema ambao ni wanafunzi wa vyuo vikuu (Chadema Students Organisation – Chaso) mjini Tabora na kuhoji kwa nini serikali imeshindwa kupeleka huduma muhimu vijijini.

"Tumesikia nia njema yao ya kuagiza ndege nyingine zaidi miaka miwili ijayo, lakini tunajiuliza, je isingekuwa busara kutumia fedha hizo kupeleka maji safi na salama mijini na vijijini?" alikaririwa akihoji.
Binafsi nimeshtushwa na kauli hiyo ya  Lowassa kupinga ununuzi wa ndege katika shirika ambalo kwa miaka mingi limegubikwa na kashfa mbalimbali za matumizi mabaya ya fedha huku likiwa halina ndege hata moja.
Mzalendo yeyote angepaswa kupongeza jitihada hizi za serikali, kwani hivi sasa siyo kwamba tutaachana na tabia ya kukodi ndege, lakini pia kwa kumiliki ndege zetu wenyewe tuna uhakika wa kufungua safari za nje kama ilivyokuwa zamani kabla ya ‘wapiga dili’ ndani ya serikali hawajalihujumu shirika na kuingiza ndege zao wenyewe.
Lakini nikashangazwa zaidi na kauli kwamba ni vyema serikali ipeleke maji vijijini, ambayo inatolewa na Lowassa mwenyewe kwa namna ambayo inaonyesha wazi ni kutafuta ‘kick’ ya kisiasa.
Nimeshangaa, na ninaamini Watanzania wengine wamemshangaa, kwa sababu jukumu la kupeleka huduma ya maji vijijini Lowassa mwenyewe alishindwa kulitekeleza kwa miaka mitano mfululizo, kuanzia mwaka 2000 hadi 2005, wakati Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, alipompa dhamana ya kuongoza Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo.
Kama waziri mwenye dhamana ya maji, alipaswa kuhakikisha wananchi, hasa wa vijijini, wanapata maji safi na salama, lakini hilo halikufanyika na ni wakati yeye akiwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo ndipo tulishuhudia wimbi la wafugaji, wengi wa jamii wa Wamasai na Wasukuma, wakihama kutoka kwenye makazi yao na kuvamia maeneo ya Mashariki, Kusini na Kusini-Magharibi mwa Tanzania, hasa mikoa ya Morogoro, Mbeya, Rukwa, Lindi, Pwani na Mtwara ambako hata ng’ombe wenyewe walikuwa hawawajui zaidi ya wengi wao kuwaona kwenye picha!
Matokeo ya kuhama huko kwa wafugaji tangu kipindi hicho ndiyo mapigano ya wakulima na wafugaji ambayo tunayashuhudia sasa na yamepoteza maisha ya Watanzania wengi kama kule Kiteto na Kilosa.
Lowassa anafahamu fika kwamba bajeti zetu ni ndogo, hazitoshi, na hata mradi ambao leo anaweza kujivunia kuufanikisha wa Maji ya Ziwa Victoria, zilikuwa fedha kutoka Benki ya Dunia kupitia shirika lake la WaterAid.
Anafahamu kwamba, mradi ule tusingeweza kuugharamia kwa bajeti yetu, ndiyo maana ulichelewa kutanuliwa kutoka Shinyanga kwenda mikoa mingine.
Vinginevyo aseme leo hii ni kwa nini kwa mamlaka yake alishindwa kuyafikisha maji hata Tabora, ambako siyo mbali na Shinyanga.
Leo hii serikali inayo mipango mizuri ya kuhakikisha maji hayo yanafika mpaka Singida, lakini anabeza.
Niliwahi kusema wakati fulani kwamba, ‘Ukweli wa mwanasiasa ni jina lake tu’, na sasa wengi wanaamini, kwa sababu mambo mengi wanayoyasema wanasiasa, hasa walio nje ya madaraka, yanalenga kukosoa serikali iliyoko madarakani na siyo kujenga, hata kama mambo hayo hayana ukweli wowote.
Ni Lowassa huyu ambaye aliwahi kusema kwamba ndiye aliyejenga Shule za Kata, lakini nakumbuka kauli hiyo ilipingwa hadharani na Joseph Mungai, ambaye alisema: “Lowassa ana mawazo mgando na akili ya kusahau, shule za Kata zilijengwa na wananchi chini ya Mkapa.”
Pengine kwa kuwa alisomea sanaa ndiyo maana sasa ameamua kuishambulia serikali kwa suala la maji, lakini naamini kwa kauli yake hiyo hata wananchi wa Monduli, wakiwemo wa kijijini Ngarash alikozaliwa siku ile ya Jumatano, Agosti 26, 1953 akiwa ni mtoto wa 4 kati ya watoto 23 wa mzee Ngoyai Lowassa, wanaweza kumsuta.
Lowassa amekuwepo Bungeni kwa miaka 30 – kwanza akiwa Mbunge kupitia Jumuiya ya Vijana kuanzia 1985 – 1990, na kisha Mbunge wa Monduli kwa miaka 25 kuanzia mwaka 1990 – 2015.
Lakini leo hii, siyo Monduli tu, lakini hata kijijini Ngarash kuna shida kubwa ya maji, na aeleze leo ni kwa nini kwa miaka yote aliyokaa Bungeni, akishika nyadhifa mbalimbali za uwaziri, hakuweza kusaidia walau kupatikana maji ya uhakika.
Lowassa amekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (anayeshughulikia Sera, Uratibu wa Bunge na Maafa) kati ya 1990-1993 chini ya Mzee John Malecela aliyekuwa Waziri Mkuu; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini kati ya 1993 – 1995; Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano) kati ya 1995 – 2000); na Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo kati ya 2000 – 2005.
Lowassa amekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka miwili, mwezi mmoja na siku 17 kati ya Desemba 20, 2005 hadi Februari 8, 2008 alipolazimishwa kujiuzulu kwa kashfa ya kampuni ya ufuaji umeme wa dharura ya Richmond Development LLC.
Hivi katika kipindi chote hicho alishindwa hata kuleta maendeleo ya jamii ikiwemo huduma ya maji huko Monduli, achilia mbali Tanzania kwa ujumla.
Hizi ni propaganda za kisiasa ambazo zinapaswa kupuuzwa kwa sababu zinalenga kukwamisha mipango madhubuti ya maendeleo ya serikali.
Pengine kwa faida ya walio wengi, tafsiri ya haraka ya neno ‘Propaganda’ ni taarifa, mawazo au uvumi unaosambazwa kwa makusudi kumsaidia au kumharibia mtu, kundi la watu, harakati, taasisi, taifa na kadhalika.
Propaganda pia inatafsiriwa kama namna ya mawasiliano yanayolenga kuwashawishi baadhi ya watu waunge mkono jambo fulani.
Lakini tafsiri nyingine ya Propaganda ni taarifa ambazo siyo sahihi zinazotumika kwa msingi wa kushawishi hadhira na kuchochea agenda, mara nyingi kwa kuwasilisha taarifa zilizopangwa ama kutengenezwa (pengine kudanganya hapa na pale) ili kuhamasisha kundi linalolengwa liamini kinachoelezwa na liunge mkono.
Neno hili kwa sasa limebebeshwa mtazamo hasi kwa kulihusisha na harakati za kurubuni kwa maslahi ya kundi linaloendesha harakati hizo na kwamba wanaofanya propaganda wanaweza kuwaaminisha watu kwamba ile rangi ‘nyeusi’ ni ‘nyeupe’ na kinyume chake.
Pengine hakuna mtu katika historia aliyetumia nguvu ya propaganda kwa mafanikio ya kutisha kama alivyofanya Paul Joseph Goebbels, ambaye alikuwa Waziri wa Propaganda wa chama cha Nazi cha Ujerumani kati ya mwaka 1933 hadi 1945 wakati wa Hitler.
Wakati wote wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, yeye ndiye aliyedhibiti mawasiliano yote nchini Ujerumani na kufanikiwa kulibadilisha taifa lote kuwa kakamavu na la kijeshi.
Inaelezwa kwamba, isingekuwa mbinu za Goebbels, chama cha Nazi kisingeweza kutawala Ujerumani kwani licha ya kuhamasisha magwaride ya kijeshi, ndiye aliyewafanya Wajerumani wawe makatili hata wakati wa vita kiasi cha kufanya mauaji ya kutisha, ikiwa ni pamoja na kuwateketeza Wayahudi.
Goebbels ndiye aliyehamasisha hadi kuanzishwa kwa somo la propaganda shuleni, ambapo watoto walianza kuaminishwa mambo mbalimbali tangu wakiwa wadogo, hata kama yalikuwa ya uongo.
Kiongozi wa chama cha National Socialism (au kwa Kijerumani: Nationalsozialismus), ambacho ni maarufu zaidi kama Nazi, Adolf Hitler, anasema katika kitabu cha Mein Kampf Sura ya VI (nanukuu kwa tafsiri ya Kiswahili): "Daima propaganda lazima ijidhihirishe kwa watu wengi. (...) Propaganda zote lazima ziwasilishwe katika mfumo maalumu na lazima zijikite kwanza kwa wasomi ili zisiwe juu ya vichwa vya watu wenye uelewa mdogo ambao ndio walengwa. (...) Sanaa ya propaganda hasa inahusisha uwezo wa kuamsha matamanio ya watu kwa ushawishi wa kutumia hisia zao, ili kutafuta mfumo mzuri wa kisaikolojia ambao unaweza kuteka umakini na kuchochea msukumo mioyoni mwa wananchi wengi. Makundi makubwa ya wananchi hayaundwi na wanadiplomasia au maprofesa wala hayahusishi watu wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi baada ya tafakuri katika kadhia husika, bali ni makundi ya vijana ambao wanayumbishwa na wazo moja baada ya jingine. (...) Kundi kubwa la wananchi katika taifa lina tabia za kike na mtazamo ambao mawazo na mwitikio wao unatawaliwa na huruma badala ya tafakuri makini. Halitofautiani sana, lakini lina mtazamo hasi na chanya wa kupenda na kuchukia, sahihi na isiyo sahihi, ukweli na uongo.
"Propaganda haihitaji kufanya uchunguzi wa ukweli wa jambo (objectively) na, kwa namna inavyotamaniwa na upande mwingine, inatakiwa kuwasilishwa kwa mujibu wa nadharia ya utawala wa haki; lakini lazima iwasilishwe kwa misingi ya ukweli ambao upande husika unataka. (...) Uwezo wa wananchi wengi umedumaa, na uelewa wao ni mdogo. Kwa upande mwingine, ni wepesi sana wa kusahau. Kwa msingi huo, propaganda zote zinatakiwa kujikita katika mambo machache muhimu na hayo yanapaswa kuhubiriwa katika fomula nyepesi inayofanana. Kauli mbiu hizo zinatakiwa kurudiwa kila wakati ili kumfanya mpaka mtu wa mwisho aweze kuelewa na kushawishika na yanayosemwa. (...) Kila badiliko linalofanywa kuhusu hoja fulani ya propaganda lazima kila wakati iwe na suluhisho moja. Kauli mbiu kubwa lazima iwekwe katika njia tofauti na kwa namna mbalimbali, lakini mwisho wa siku lazima kurejea kwenye fomula ile ile."
Mbinu hii ya propaganda ndiyo iliyotumiwa na Lowassa kwa wanavyuo wale Tabora, ambapo hakuna aliyekumbuka kwamba kiongozi huyo huyo ndiye aliyekuwa na wajibu wa kuwaletea maji miaka 15 iliyopita wakati akiwa waziri wa maji lakini akashindwa.
Watanzania wanapaswa kuwa makini na propaganda hizi, kwa sababu ndizo kwa miaka mingi zimekwamisha maendeleo.
Lowassa ana haki ya kujinadi na kugombea kwa sababu ni haki yake ya Kikatiba, lakini hana budi kuunga mkono juhudi njema za serikali zenye kuleta maendeleo.

+255 656 331974


Comments