Featured Post

KUWAIT YAIPATIA TANZANIA MKOPO NAFUU WA UJENZI WA BARABARA MKOANI TABORA

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (kushoto) akizungumza na ujumbe kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait, kuhusu miradi ya miundombinu itakayofadhiliwa na Mfuko huo, ukiwemo mradi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Chaya kwenda Nyahua mkoani Tabora. Kulia ni mwakilishi wa Balozi wa Kuwait hapa nchini Bw. Mohammad Rashid Alamiri, Makao Makuu ya Wizara, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (kushoto) akipeana mkono na Mwakilishi wa Balozi wa Kuwait Bw. Mohammad Rashid Alamiri huku wakifurahia jambo baada ya kumalizika kwa mkunano kati yao uliojikita katika mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo barabara na sekta ya afya, Mkutano huo umefanyikaatika Makao makuu ya Wizara, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe toka Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (Kuwait Fund) baada ya kumalizika kwa kikao kati yake na wajumbe hao ambapo mbali na kutoa mkopo wa ujenzi wa barabara kutoka Chaya kwenda Nyahua mkoani Tabora, walionesha nia ya kutoa mikopo mingine yenye masharti nafuu katika miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania. Kikao hicho kimefanyika Makao Makuu ya Wizara hiyo, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (kulia), akisalimiana na Mshauri wa masuala ya ufundi kutoka Kuwait Bw. Mohammad Alhadidi, baada ya kumalizika kwa kikao kati ya Waziri huyo na Wajumbe kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait, katika ukumbi wa Wizara hiyo Jijini Dar es salaam.
Wataalamu toka Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (kushoto) na wataalamu kutoka Tanzania (kulia) wakijadili kuhusu mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Kuwait, utakao saidia kujenga barabara Mkoani Tabora, Mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo, Jijini Dar es salaam.
Maafisa waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakimsikiliza Mwakilishi wa Balozi wa Kuwait Nchini Tanzania Bw. Mohammad Rashid Alamiri (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza katika Kikao kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), katika Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
Serikali ya Kuwait imeahidi kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Kimarekani milioni 34 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 74.8 kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilometa 85 kwa kiwango cha lami kutoka eneo la Chaya hadi Nyahua mkoani Tabora.
Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam na mwakilishi wa Balozi wa Kuwait hapa nchini, Bw. Mohammad Rashid Alamiri, aliyeongoza ujumbe kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait, ulipomtembelea na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ambapo wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania na Kuwait.
Dkt. Mpango ameushukuru Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (Kuwait Fund) kwa kuipatia Tanzania mkopo  huo wenye masharti nafuu utakaochochea maendeleo kwa Watanzania hususani wanaoishi katika maeneo ambayo barabara itajengwa kwa kuwa watarahisishiwa usafiri na usafirishaji wa bidhaa zao hivyo kukuza uchumi wao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Amesema kuwa kipande hicho cha barabara kutoka Chaya hadi Nyahua, ambacho kiko Barabara Kuu itokayo Dar es salaam kwenda katika mikoa ya Tabora na Kigoma, licha ya umuhimu wake katika kukuza biashara na usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo ikiwemo inayokwenda nchi jirani, ilikuwa haijapata fedha kwa ajili ya ujenzi wake.
“Riba waliyoiweka mezani kwa mazungumzo ni asilimia 2 lakini nimewaomba waangalie uwezekano wa kuiteremsha walau ifike asilimia 1.5 na wamependekeza kipindi cha kuanza kulipa mkopo kiwe miaka ishirini ijayo lakini nimewaomba wasogeze hadi kufikia miaka 25 kama ilivyo kwa mradi wa Hospitali ya Mnazimmoja” aliongeza Dkt. Mpango
Dkt. Mpango amesema Serikali ya Kuwait kupitia Mfuko wake huo wa Maendeleo wameonesha nia ya kutoa mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyoko Visiwani Zanzibar.
“Nawahakikishia kuwa baada ya muda si mrefu wananchi wa mikoa ya Tabora na Kigoma watarajie kuona mkandarasi akiingia kazini ili kujenga barabara hii muhimu sana kwao na kwa uchumi wa Taifa kwa ujumla” Alisisitiza Dkt. Mpango.
Ameeleza kuwa ujenzi wa kipande cha barabara hiyo kutoka Chaya hadi Nyahua  unatarajia kugharimu shilingi Bilioni 61 lakini Kuwait haitatoa fedha zote hivyo ameuomba Mfuko huo uangalie uwezekano wa kutoa kiasi hicho chote cha fedha  ili uweze kukamilika mapema.

Comments