Featured Post

KESI ZA MAXENCE MELO ZAPIGWA KALENDA HADI JANUARI 26, 2017!



Na Daniel Mbega
KESI mbili kati ya tatu zinazohusiana na Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cyber Crimes Act, 2015) zinazomkabili Maxence Melo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jamii Media inayomiliki mtandao wa JamiiForums, zimeahirishwa tena jana hadi Januari 26, 2017.

Katika kesi namba 456 ambayo iko mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba, upande wa mashtaka ukiongozwa na Mohammed Salum umeiomba mahakama iahirishe kesi hiyo kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Vile vile katika kesi namba 457 iliyoko mbele ya Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa katika Mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, upande wa mashtaka ukiongozwa na Mohammed Salum umeiomba mahakama iahirishe kwa kuwa hawajakamilisha upelelezi.
Katika kesi hizo, Maxence anatetewa na mawakili Peter Kibatala, Jeremiah Mtobesya, Benedict Ishabakaki, Jebra Kambole, Hassan Kyangiro na James Malenga.
Kwa mara ya kwanza, Melo alifikishwa mahakamani Ijumaa, Desemba 16, 2016 akikabiliwa na mashtaka manne katika kesi tatu tofauti, huku kesi mbili mashtaka yake yakifanana isipokuwa matukio ya tarehe ni tofauti.
Kesi namba 456, iliyoko mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Thomas Simba, ambapo upande wa Jamhuri ulieleza kwamba, katika siku na tarehe tofauti kati ya Aprili 1, 2016 na Desemba 13, 2016 katika eneo la Mikocheni ndani ya Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Melo akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd ambayo inaendesha mtandao wa JamiiForums, wakati akijua kwamba Jeshi la Polisi Tanzania linafanya upelelezi wa jinai kuhusiana na mawasiliano ya kimtandao yaliyochapishwa kwenye mtandao wake, kwa nia ya kuvuruga uchunguzi, alikaidi kwa makusudi amri ya kutoa taarifa ambazo alikuwa nazo, kinyume na kifungu cha 22(2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cyber Crimes Law) namba 14 ya mwaka 2015.
Katika namba 457,  ilielezwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwambapa kwamba, katika siku na tarehe tofauti kati ya Mei 10, 2016 na Desemba 13, 2016 katika eneo la Mikocheni ndani ya Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Melo akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd ambayo inaendesha mtandao wa JamiiForums, wakati akijua kwamba Jeshi la Polisi Tanzania linafanya upelelezi wa jinai kuhusiana na mawasiliano ya kimtandao yaliyochapishwa kwenye mtandao wake, kwa nia ya kuvuruga uchunguzi, alikaidi kwa makusudi amri ya kutoa taarifa ambazo alikuwa nazo, kinyume na kifungu cha 22(2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cyber Crimes Law) namba 14 ya mwaka 2015.
Aidha, katika kesi namba 458, ambayo iko mbele ya Hakimu Nongwa, Melo anakabiliwa na shtaka la kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa nchini Tanzania (domain) kinyume na kifungu cha 79(c) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Namba 3 ya mwaka 2010 ikisomwa pamoja na Kanuni ya 10 na 17 (4) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Namba 428 za mwaka 2011.
Upande wa Jamhuri ulieleza katika kesi hiyo kwamba, katika siku na tarehe tofauti kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13, 2016 katika eneo la Mikocheni ndani ya Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Melo akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd iliyosajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Kampuni (Sura ya 212 kama ilivyorejewa mwaka 2002) yenye hati ya usajili Namba 66333 amekuwa akiendesha na kutumia tovuti inayojulikana kama jamiiforums.com ambayo haijasajiliwa kwenye code za Tanzania (country code Top Level Domain - ccTLD), inayofahamika kama do-tz.
Maxence yuko nje kwa dhamana.

Comments