Featured Post

KAFULILA ANATANGATANGA, ATAKUWA KAMBI YA NANI CHADEMA?


Na Daniel Mbega
DESEMBA 15, 2016, Katibu Mwenezi wa NCCR-Mageuzi, David Kafulila alitangaza rasmi kurejea katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kuwa katika chama hicho kwa takriban miaka 7 na siku kadhaa tangu alipojiunga nacho mwaka 2009.

Wakati ule aliitwa ‘mkorofi’ kwa kitendo chake cha kuwasema hadharani na kuwakosoa viongozi wa Chadema, ambacho kilimgharimu uongozi.
Wengi wanamkumbuka Kafulila kwa jinsi alivyolivalia njuga sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu (BoT) lililohusu kampuni ya kufua umeme ya IPTL ambapo mabilioni ya fedha yalichotwa na watu binafsi wakagawana.
Inakumbukwa jinsi sakata hilo lilivyoiyumbisha serikali kiasi cha kulifumua Baraza la Mawaziri na kumjengea umaarufu.
Hata hivyo, wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Kafulila alishindwa kurejea Bungeni na akashindwa pia kwenye kesi yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi.
Kafulila alikuwa Mbunge wa Kigoma Kusini kupitia NCCR-Mageuzi kati ya mwaka 2010-2015, alijiunga baada ya kutangaza kuachana rasmi na Chadema Novemba 18, 2009, zikiwa ni siku saba tu tangu yeye na Danda Junju walipovuliwa nyadhifa zao na Sekretarieti ya chama hicho.
Katika waraka wake wa wazi kuhusu uamuzi wake wa kujitoa NCCR-Mageuzi, Kafulila alieleza kwamba ameamua kujivua uanachama na nafasi ya uongozi aliyokuwa nayo na kuelekea Chadema.
Pamoja na mambo mengine, katika waraka huo Kafulila aliushukuru uongozi wa NCCR-Mageuzi kwa muda wote aliokuwa nao na akaeleza uamuzi wake wa kujivua nafasi yake ya uongozi na nia yake ya ‘kufuata mabadiliko’ licha ya ukandamizwaji unaofanywa na vyombo vya kusimamia haki.
Akasema kwamba, anaamini hakuna chama ambacho kinaweza kuunganisha nguvu na kuwa na chama kimoja cha upinzani chenye mikakati thabiti ya kuleta mabadiliko zaidi ya Chadema.
Mara kadhaa nimekuwa nikisema; ‘Ukweli wa mwanasiasa ni jina lake tu’, lakini mengine yote ni mbwembwe za kutafuta maslahi na kuungwa mkono.
Nakumbuka vizuri kwamba Novemba 10, 2009 Kafulila na Danda teuzi zao zilitenguliwa ndani ya Chadema – Kafulila ndiye aliyekuwa Msemaji wa Chadema (nafasi ambayo sasa inashikiliwa na Tumaini Makene) na Danda alikuwa anahusika na masuala ya Bunge.
Kilichowaponza wakati ule ni uswahiba wao na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa Chadema, Zitto Zuberi Kabwe, ambaye wakati huo alikuwa na mvutano na uongozi wa juu wa Chadema, ikiwemo kutaka kugombea uenyekiti.
Kafulila alishtukia mapema kwamba anatimuliwa kwenye nafasi yake, na hiyo ilifuatia kikao cha viongozi (Sekretarieti) wa Chadema kilichofanyika Dodoma, ambapo aliwahi mapema kwenye vyombo vvya habari na kusema kwamba kuna mpango wa viongozi wa Chadema kutaka kumtimua.
Alipozungumza na wanahabari Novemba 10, 2009, Kafulila alisema aliambiwa kwa mdomo na Katibu Mkuu Dk. Wilbrod Slaa, na kwamba aliitwa kwenye kikao cha sekretariati siku hiyo kuhojiwa kuhusu matamshi yake kwenye vyombo vya habari yaliyomtuhumu Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kufanya kikao kisicho rasmi Dodoma kwa ajili ya kumwengua uanachama yeye na wenzake.
Dk. Slaa mwenyewe alisema: "Tena andika wala usiogope ni kwamba, leo kulikuwa na kikao, nimekiongoza mwenyewe na maamuzi nimeyatoa mwenyewe..., tumetengua uteuzi wao. Sasa ni wanachama wa kawaida… Tunataka kusafisha chama..., maana tukiacha hali hii tunaweza kuingia Ikulu na mambo ya ajabu."
Ndicho kipindi ambacho zengwe la kutaka kumng’oa Zitto lilikuwa limeshika kasi huku wakimtuhumu mwanasiasa huyo kutaka kukigawa chama hicho ambacho wakati huo kilikuwa ‘kinapambana na ufisadi’ wa majukwaani.
Na hata Kafulila alipoondoka Chadema na kujiunga na NCCR-Mageuzi, bado aliendelea na uswahiba wake na Zitto kiasi kwamba iliripotiwa kuwa hata magari aliyotumia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010 yalikuwa ya Zitto.
Kuenguliwa kwa Kafulila na Danda katika nafasi zao kuliwafurahisha wanachama wengi ambao waliowaona wanasiasa hao ni wakorofi na wenye kutaka kuleta migogoro isiyokuwa na sababu.
Nakumbuka Zitto alimtetea kwa nguvu zote Kafulila kupitia kwenye mitandao na akawakosoa wale wote waliokuwa wakichangia mijadala kwamba ndio wanaotaka kusababisha migogoro kwenye chama.
Katika majibizano hayo, Zitto aliwahi kusema: “Can you back up your allegations? Don’t spin! Mambo ya Chadema tuachie Chadema sawa? Why are you defensive? Justice will prevail.”
Hata hivyo, baada ya kupata taarifa rasmi, Zitto, ambaye alikuwa nje ya nchi, alionekana kutofurahishwa na uamuzi huo na katika ujumbe wake kwa gazeti moja la kila siku, alisema: "Ninasikitika kuwa tunachukua maamuzi kama haya kipindi hiki ambacho nchi inahitaji chama imara cha upinzani. Kafulila ni mgombea mtarajiwa wa ubunge katika Jimbo la Kigoma Kusini ambalo CCM wamefanya vibaya katika uchaguzi wa serikali za mitaa kuliko majimbo yote nchini. Uamuzi huu unaweza kuwashtua sana wanachama wetu Kigoma Kusini na mkoa wa Kigoma kwa ujumla."
Zitto alikumbusha kuwa Kafulila aligombea uenyekiti wa jumuiya ya vijana ya Chadema na akashinda, lakini uchaguzi ulivurugwa na kufutwa na hivyo utarudiwa na hivyo uamuzi wa kumfukuza Kafulila ni dalili za wazi za watu waliofuta uchaguzi huo kuleta vurugu kwenye chama kwani wanachama hawatakubali uonevu.
"Kwangu mimi Kafulila ni kijana mahiri mwenye kukipenda chama chetu na ndio maana niliamua kumgroom (kumkuza) ili aje kuwa mgombea ubunge na baadaye mbunge katika Jimbo la Kigoma Kusini. Anakipenda chama chake, ana akili nyingi na mjuzi wa kujenga hoja katika kutetea chama bila woga," alisema Zitto.
Kama katika kipindi kile walau alikuwa na mtetezi ndani ya Chadema (Zitto Kabwe), je, safari hii nani atamtetea ikitokea kwamba misimamo yake itaendelea kubaki ile ile? Au kwa vile Dk. Slaa sasa hayupo?
Je, amerejea Chadema kwa nia ya dhati au kwa sababu amekosa ubunge kupitia NCCR-Mageuzi na hakusaidiwa wakati wa kesi yake? Au amemfuata mkewe, Jesca Kishoa, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum?
Kama wakati ule aliamua kuondoka Chadema baada ya kuvuliwa uongozi kwa sababu ya kuusema uongozi, je, wana-Chadema leo waamini kwamba amebadilika na hataweza kuwakosoa viongozi wake kama ilivyokuwa mwanzo?
Kuna mashaka na kurejea kwake na haifahamiki ni kutangatanga kusaka madaraka ama kweli amesukumwa na msimamo wa Chadema, kama anavyodai mwenyewe kwamba ndicho chama kitakacholeta mabadiliko.
NCCR-Mageuzi ni miongoni mwa vyama vilivyokuwa vikiunda umoja mfu wa Ukawa, na Kafulila anatambua kwamba yeye pia alikuwa mmoja aliyeunga mkono umoja huo. Sasa ana uhakika gani kama Chadema itakuwa na nguvu kama ilivyokuwa mwaka 2015 chini ya Ukawa?
Tusubiri tuone itakavyokuwa, vinginevyo ni staili zile zile za wanasiasa za kutangatanga kusaka tonge na kusahau walichokisema jana.

0656331974

Comments