- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
BERNARD
Rabiu Saanane, au Ben Saanane, mwanaharakati chipukizi wa kisiasa, ametoweka
kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa. Hakuna aliye tayari kufumbua kinywa na kusema
mahali aliko.
Kwa jinsi
mwanasiasa huyo chipukizi alivyo mahiri wa ‘kucheza’ na mitandao ya kijamii,
kwa vyovyote vile mpaka sasa angekuwa amejibu mwenyewe kwamba yuko wapi – awe mapumzikoni
au kazini – kwa sababu siku zote amekuwa mahiri wa ‘kushinda’ kama siyo ‘kukesha’
kwenye mitandao ya kijamii akianzisha hoja mbalimbali.
Ajabu ni
kwamba, hata familia yake haijui aliko na hakuna hata kiongozi mmoja wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo – Chadema, wala mwenyekiti wa chama hicho, Freeman
Mbowe, ambaye kijana huyo alikuwa Katibu Myeka wake, yaani Personal Assistant,
anayezungumzia aliko kijana huyo ambaye mwaka 2015 aligombea ubunge kule Rombo
na kushindwa vibaya kwenye kura za maoni za chama hicho na Joseph Selasini.
Ukimya huu
unaleta tafsiri hasi katika jamii hasa katika kipindi ambacho Chadema, baada ya
kushindwa kwa Operesheni Ukuta, sasa inataka kuja na Opereshenhi Kata Funua ambayo
tunaambiwa ni Ben Saanane ndiye aliyeiandaa kabla ya kupewa ‘likizo’ na Mbowe
kwa ‘kazi nzuri’ aliyoifanya.
Ama tafsiri
iliyopo ni kwamba, huenda Chadema, au viongozi wa Chadema, wanataka kutumia
kutoweka kwa Ben Saanane kama ‘kick’ yao ya kuianzisha Operesheni Kata Funua
kwa kusingizia kwamba kupotea kwake ni hujuma za Serikali ya Chama cha
Mapinduzi – CCM, wakati siyo kweli.
Pengine wanataka
kutumia hiyo kama njia ya kutafuta huruma ya Watanzania ili wawaunge mkono
watakapoanzisha operesheni yao baada ya ‘ukuta wao kubomoka’. Hakuna anayejua.
Kwa kuwa
hakuna anayejua kilichomo katika mkakati wa Operesheni Kata Funua zaidi ya Ben
Saanane mwenyewe na viongozi wa juu wa Chadema, basi ni vigumu kueleza kama
hata kutoweka kwake ni sehemu ya kufanikisha mkakati huo ama ndio ufunguo wa
kuanzisha operesheni hiyo. Hakuna ajjuaye.
Yanasemwa mengi
kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, na Jeshi la Polisi tayari
limepewa taarifa za kupotea kwa mwanasiasa huyo.
Hata hivyo,
binafsi nimeamua kuyabandika maoni ya mdau mmoja kama yalivyo, ambayo yanamtaja
moja kwa moja Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, kwamba anahusika na ndiye
aliyefanikisha ‘mapumziko’ ya Ben Saanane huko Afrika Kusini.
Soma mwenyewe,
halafu pima, tafakari na utapata jibu halisi;
Wadau, amani iwe kwenu.
Nawapa pole ndugu wa Ben Saanane hususan Baba
yake mpendwa, Focus Saanane na mdogo wake Erasto Saanane ambao kwa zaidi ya
wiki sasa wanahangaika kumtafuta mpendwa wao Bernard Rabiu Saanane au Ben
Saanane kama tulivyozoea kumuita ambaye amepotea katika mazingira ya
kutatanisha. Ninasema ni mazingira ya kutatanisha kwa sababu mpaka leo hakuna
anayejua ni lini BEN alipotea na katika mazingira yepi. Pia haijajulikana kama
Ben amepotea ama yupo busy na majukumu ya kikazi.
Kutokana na kupotea kwa Ben Saanane, baadhi ya
wafuasi wa CHADEMA wanaunyooshea vidole vya lawama uongozi wa CHADEMA
hususan Mwenyekiti Freeman Mbowe. Kupitia mijadala mbalimbali wanayoanzisha
hasa kwenye kurasa zao za facebook, kwa hakika nimebaini mambo yafuatayo;
1. Julai 2016, Freeman Mbowe alimteua Ben
Saanane kuwa Msaidizi wake akimpa cheo cha ‘Executive Assistant’ wa Ofisi ya
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa au kama Malisa Godlisten anavyoita Personal
Assistant. Wakati huo huo, Ben Saanane alikuwa na Wadhifa wa Mkuu wa Sera na
Utafiti wa CHADEMA kama Gazeti la Tanzania Daima la Desemba 10, 2016
lilivyobainisha. Kupitia nyadhifa zake hizo, Ben Saanane ameratibu na kusimamia
mikakati na Operesheni kadhaa za chama ambazo ni pamoja na Mkakati wa Siri juu
ya Zitto Kabwe wa mwaka 2013, Operesheni UKUTA ya Septemba 2016 na Operesheni
Kata Funua ambayo utekelezaji wake haujafanyika. Kwa ujumla, Ben Saanane ni
mmoja wa maafisa waandamizi wa CHADEMA ambaye amebahatika kuwa na Siri Kuu za
chama. Ni katika siri hizi ndizo zilizoweka rehani maisha ya Ben Saanane.
2. Agosti Mosi 2016, Ben Saanane alipewa jukumu
maalum la kumuandama Rais Magufuli kwenye mitandao ya kijamii. Lengo la jukumu
hili ni kuuandaa umma uamini kuwa lolote litakalomtokea Ben, watu wataamini
kuwa ni kutokana na maandiko yake kwenye mitandao ya kijamii.
3. Wiki ya pili ya Mwezi Novemba 2016, Freeman
Mbowe alimuandalia Ben Saanane safari ya kwenda Nchini Afrika ya Kusini ambapo
kwa mujibu wa mtu wa karibu na Ben Saanane aitwaye HILDA NEWTON, Safari hiyo
ilipaswa kufanyika Novemba 19. Kabla ya safari hiyo, Ben alipewa na bosi wake
(Mbowe) mapumziko ya wiki moja ili akamilishe andiko la Operesheni Kata Funua
ambalo lilikuwa katika hatua ya mwisho kukamilika. Pia Mbowe alimpa maelekezo
maalum Ben ya kutowasiliana na watu wengine ili apate muda wa kutosha wa
kukamilisha andiko hilo. Aidha, Mbowe alimlipa Ben gharama zote za safari
ambapo haikubainishwa ni kiasi gani na haijulikani alipaswa kuwa Afrika ya
Kusini kwa siku ngapi na kwa majukumu yepi. Ni katika kipindi hicho ndipo
ukimya wa Ben Saanane ulipoanza kuripotiwa.
4. Wakati Ben anaandaliwa kwenda Afrika ya
Kusini, Mbowe na baadhi ya viongozi akiwemo John Mrema wakaandaa safari ya
kwenda Uingereza. Ni ajabu kwa Mbowe kwenda Uingereza bila ya msaidizi
wake wa karibu.
5. Novemba 26, 2016, Hilda Newton
alijitokeza kuwajibu wale wote waliokuwa wanamtumia ujumbe kumuuliza alipo Ben
Saanane. Katika ujumbe huo ambao aliandika kwenye ukurasa wake wa facebook,
Hilda Newton alisema kuwa Ben Saanane yupo Afrika ya kusini na kwamba atarejea
siku chache zijazo. Bado haijafahamika nani alimtuma Hilda kutoa taarifa hiyo
ijapokuwa habari za chini ya kapeti zinasema kuwa ni maelekezo kutoka
ngazi za juu za CHADEMA. Baadhi ya wafuasi wa CHADEMA walihoji sana andiko
hilo. Familia ya Ben Saanane nayo ilishtushwa na andiko hilo kwani haiingii akilini
Ben asafiri bila ya kutoa taarifa kwa familia yake.
6. Familia ya Ben imefanyamawasiliano ya mara
kwa mara kwa uongozi wa CHADEMA kupitia Katibu Mkuu Vincent Mashinji. Hata
hivyo, walijibiwa kuwa Ben yupo salama na anatekeleza majukumu ya kikazi. Hata
hivyo, kadri ziku zilivyosonga, wasiwasi uliwajaa na ndipo Jumanne Desemba
6, 2016 walipoamua kwenda kituo cha Polisi Tabata kutoa taarifa za kupotea kwa
Ben. Hadi wakati huo, chama kiliendelea kuwa na msimamo kuwa Ben yupo salama na
kwamba wasiwe na wasiwasi.
7. Hadi hivi sasa, hakuna kiongozi yeyote wa
CHADEMA aliyetoa taarifa rasmi kwa vyombo vya Habari juu ya ukimya wa Ben
Saanane. Je ni kweli kwamba amepotea au yupo kikazi Afrika ya Kusini kama
baadhi ya viongozi wa chama hicho walivyonukuliwa?
8. Mwenyekiti wa CHADEMA ambaye Ben ndiye Bosi
wake Mkuu mpaka sasa hajatoa tamko lolote. Hii inatia shaka kwani
inaeleweka kuwa kwa taratibu za kiofisi, mtu akikosekana kwa muda wa siku saba
mfululizo bila ya taarifa zozote lazima aandikiwe barua ya kutaka kujieleza kwa
nini asichukuliwe hatua. Mbowe hajafanya hivyo na hii inatujengea imani kuwa
anajua nini kinaendelea. Aidha, licha ya kupata taarifa kuwa msaidizi wake
amepotea, Mbowe anaendelea na ziara zake nchini Uingereza kana kwamba hakuna
kilichotokea. Hajashtushwa kabisa na kupotea kwa Ben. Anajua dhahiri nini
kinaendelea.
9. Jitihada za kumtafuta Ben Saanane zinafanywa
na ndugu zake tu pamoja na marafiki zake wa karibu. Hii inazua mashaka mengine
juu ya mfumo wa uendeshaji wa CHADEMA.
10.Gazeti la Tanzania Daima kwa mara ya kwanza
limeandika taarifa juu ya kupotea kwa Ben Saanane Desemba 10, 2016. Hili ni
gazeti linalomilikiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA. Ukimya wa gazeti hilo kwa
hakika unazua mjadala mwingine.
Comments
Post a Comment