Featured Post

CHADEMA, MBOWE WASIPOMRUDISHA BEN SAANANE WATANZANIA WATAWAHUKUMU!




Na Daniel Mbega
BERNARD Rabiu Saanane, au Ben Saanane, mwanaharakati chipukizi wa kisiasa, ametoweka tangu Novemba 18, 2016 na hajulikani aliko.
Kwa jinsi mwanasiasa huyo chipukizi alivyo mahiri wa ‘kukesha’ kwenye mitandao ya kijamii, kwa vyovyote vile mpaka sasa angekuwa amejibu mwenyewe kwamba yuko wapi – awe mapumzikoni au kazini.
Hata baada ya familia yake kuamua kufungua kesi ya ‘kupotea’ kwa ndugu yao katika Kituo cha Polisi Tabata jijini Dar es Salaam Desemba 5, 2016 na kupewa RB namba TBT/RB/8150/2016, bado viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho Ben ni kiongozi na Katibu Myeka wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, hakikuweza kutoa tamkoa lolote.

Katika mazingira ambayo yanayonyesha kwamba huenda viongozi wa Chadema walikuwa ‘wakitafuta uongo’ wa kuwaeleza Watanzania, hawakuweza kusema lolote hadi Jumatano, Desemba 14, 2016 – yaani siku 9 tangu familia ilipotoa taarifa polisi – ndipo wakatoa tamko.
Tamkoa la Chadema, ambalo lilitanguliwa na tamko la wanaharakati wa Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania (UTG) lililotolewa na mwenyekiti wake Malisa Godlisten (mfuasi wa Chadema pia), linatia walakini kwa sababu halijajibu hoja za msingi na linaonekana kama kuna maigizo ya wazi.
UTG iliipa Chadema saa 72 kutoa taarifa za kupotea kwa Saanane aliyeondoka nyumbani kwake Novemba 18, 2016 na mpaka sasa hajaonekana wala taarifa zake kutolewa sehemu yoyote.
Katika tamko lao, badala ya kujibu hoja za msingi kutokana na mijadala inayoendelea, Chadema wanaitaka eti Serikali kutumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kumtafuta Ben Saanane.
Katika kile ambacho kinaonekana kupotosha ukweli, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema ati katika siku za karibuni, Saanane amekuwa akiongoza kampeni kwenye mitandao ya kijamii, kuhusu kuhakikiwa kwa shahada za uzamivu (PhD) kwa baadhi ya viongozi kwamba huenda ikawa ndiyo chanzo cha kutoweka kwake.
Lissu akasema ati wakati fulani (bila kutaja ni lini – pengine huenda miaka 10 iliyopita) Saanane alitumiwa ujumbe wa maneno kupitia simu yake ya kiganjani akitishiwa kuacha kuikosoa Serikali.
“Nanukuu maneno aliyotumiwa: “Ben Saanane unachokitafuta ndani ya Serikali hii utakipata, kwa elimu na uwezo wako hatukutarajia ungefikia hatua ya ajabu kwa namna ulivyofikia, hujiulizi kwanini upo huru hadi muda huu.
“You are too young to die. Tunajua utaandika na hili, andika lakini the next post hutaandika ukiwa na uhuru wa kutosha, andika but your days are numbered.
“Unajua kuna rafiki yako alipuuza na hutaki kuandika kuhusu yeye, labda kwa kuwa alitangulia, andika Ben, andika sana, ongea, sema lakini utajikuta mwenyewe na chatu,” alinukuu Lissu.
Kuhusu taarifa ambayo imesambaa katika mitandao ya kijamii kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe anajua aliko Saanane, Lissu alisema: “Mara ya mwisho Ben amewasiliana na mwenyekiti Novemba 14 mwaka huu akiwa Dodoma na huwa hawaongozani, bali Ben anafanyia kazi zake makao makuu ya chama.”
Kitu pekee ambacho Lissu, Mbowe na Chadema hawakijui ni kwamba, kupotea kwa Ben Saanane siyo suala la itikadi wala kisiasa, bali ni suala la kitaifa na linawahusu Watanzania wote bila kujali ni wafuasi wa chama gani cha siasa wala imani gani ya dini.
Kueleza kirahisi rahisi tu kwamba Serikali ndiyo yenye wajibu wa kulinda hata mipaka ya nchi ni kukwepa hoja kwa mkusudi kabisa wakati wanafahamu fika wanacheza na uhai wa mtu.
Binafsi sijaridhika na tamko la Tundu Lissu wala ujumbe huo wa maandishi kwenye simu ambao unaweza pia ukawa wa kutungwa ili kuirushia serikali lawama kwamba inahusika na utekaji wa watu na kuua wananchi wake, jambo ambalo halipo.
Chadema na Lissu wanashindwa kusema ukweli kwamba suala la kutoweka kwa Saanane, ambaye mwaka 2015 aligombea ubunge kule Rombo na kushindwa vibaya kwenye kura za maoni za chama hicho na Joseph Selasini, ni la kimkakati zaidi ndani ya chama kama ambavyo taarifa mbalimbali zimekuwa zikitarai kwenye mitandao ya kijamii.
Ukimya na usiri huu unaleta tafsiri hasi katika jamii hasa katika kipindi ambacho Chadema, baada ya kushindwa kwa ‘Operesheni Ukuta’, sasa inataka kuja na ‘Operesheni Kata Funua’ ambayo tunaambiwa ni Saanane ndiye aliyeiandaa kabla ya kupewa ‘likizo’ na Mbowe kwa ‘kazi nzuri’ aliyoifanya.
Kwa msingi huo basi, Chadema, au viongozi wa Chadema, wanataka kutumia kutoweka kwa Saanane kama ‘kick’ yao ya kuianzisha ‘Operesheni Kata Funua’ kwa kusingizia kwamba kupotea kwake ni hujuma za Serikali ya Chama cha Mapinduzi – CCM, wakati siyo kweli.
Pengine wanataka kutumia hiyo kama njia ya kutafuta huruma ya Watanzania ili wawaunge mkono watakapoanzisha operesheni yao baada ya ‘ukuta wao kubomoka’. Hakuna anayejua.
Kwa kuwa hakuna anayejua kilichomo katika mkakati wa Operesheni Kata Funua zaidi ya Saanane mwenyewe na viongozi wa juu wa Chadema, basi ni vigumu kueleza kama hata kutoweka kwake ni sehemu ya kufanikisha mkakati huo ama ndio ufunguo wa kuanzisha operesheni hiyo. Hakuna ajuaye.
Kama hayo hayako kwenye mikakati hiyo, basi ni wakati wa wao kusema wazi aliko Saanane, vinginevyo jamii itaamini kwamba chama hicho ni cha kuteka na kuwatesa wanachama na wafuasi wake kama ilivyopata kutokea kwa aliyekuwa mlinzi binafsi wa Katibu Mkuu, Khalid Kagenzi, mwaka 2015
Watu hawatawaelewa kwa sababu watakumbushia pia ajali ya utata ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Chacha Zakayo Wangwe, iliyotokea mwaka 2008.
Na hawatawaelewa kutokana na mwenendo wa uongozi wa mwenyekiti wa chama hicho, Mbowe, kuwaona wale wote wenye mtazamo chanya na wanaokubalika ni adui zake.
Hakuna anayeweza kuwaelewa kwa sababu kati ya yanayosemwa kwenye mitandao ya kijamii, yapo mengi yana ukweli kwa asilimia kubwa.
Ben Saanane ameandaa operesheni nyingi ndani ya Chadema, ambapo ukiachilia mbali ‘Operesheni Kata Funua’ ambayo haijaanza, lakini pia aliratibu na kusimamia mkakati wa siri juu ya Zitto Kabwe mwaka 2013 pamoja na Operesheni Ukuta.
Chadema waseme kuhusu madai kwamba, mnamo Agosti Mosi, 2016 Saanane alipewa jukumu maalum la kumuandama Rais John Magufuli kwenye mitandao ya kijamii. Je, hii haikuwa mkakati wao mahsusi wa kutimiza malengo yao kwamba ikitokea jambo lolote likampata Saanane, basi jamii ielewe ni kwa sababu ya maandiko yake kwenye mitandao ya kijamii?
Tamko la Lissu linakinzana na taarifa zilizosambaa kwamba kabla ya kutoweka kwake, Saanane alikuwa amepewa likizo ya wiki moja na bosi wake, Mbowe, hivyo hata kama waliwasiliana Novemba 14, ilikuwa ni katika kipindi ambacho alikuwa likizo kabla ya kuianza safari yake ya kwenda Afrika Kusini ‘kupumzika’ na kwamba katika kipindi hicho cha likizo ya wiki moja alikuwa ameagizwa na Mbowe kutowasiliana na watu wengine ili apate muda wa kutosha wa kukamilisha andiko la ‘Operesheni Kata Funua’.
Inaelezwa kwamba kumbe hata gharama gharama zote za safari kwenda huko Afrika Kusini zililipwa na Mbowe.
Wakati Saanane anaandaliwa safari kwenda Afrika ya Kusini, Mbowe na baadhi ya viongozi akiwemo John Mrema wakaandaa safari ya kwenda Uingereza.
Lakini wakati familia ya Saanane ikiwa haijui aliko ndugu yao, Novemba 26, 2016 akajitokeza mwanachama wa Chadema, Hilda Newton, kupitia ukurasa wake wa Facebook akiwajibu wale wote waliokuwa wanamtumia ujumbe kumuuliza alipo Ben Saanane, yeye akawajibu kwamba Saanane yuko Afrika Kusini na kwamba atarejea siku chache zijazo.
Haijafahamika nani alimtuma Hilda kutoa taarifa hiyo japokuwa habari nyingine zinadai kuwa ni maelekezo kutoka ngazi za juu za Chadema.
Hapa kuna walakini na Chadema waseme ukweli, vinginevyo Watanzania watawahukumu kwa hili.

Comments