Featured Post

KUKAMATWA MENO 50 YA TEMBO + ZIARA YA MAGUFULI MALIASILI = KUTUMBULIWA KWA DCI DIWANI ATHUMANI MSUYA





JUMAMOSI, Oktoba 29, 2016, Dk. John Magufuli alitimiza miaka 57 ya kuzaliwa kwake, lakini badala ya kukaa nyumbani kula keki, Rais huyo wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya mambo makubwa mawili yaliyoacha simulizi.
Kwanza alizuru ghafla katika Wizara ya Maliasili na Utalii katika kilichoelezwa kwamba alikuwa anafuatilia utekelezaji wa operesheni ya kukabiliana na ujangilii inayofanywa na Kikosi Kazi cha wizara hiyo.

Lakini pili, mara baada ya ziara hiyo, ikatolewa taarifa ya kutenguliwa kwa uteuzi wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai – DCI, Kamishna wa Polisi Diwani Athumani Msuya, aliyeishikilia nafasi hiyo kwa muda wa mwaka mmoja, miezi mitano na siku 26 tangu alipoteuliwa Mei 3, 2015.
CP Diwani Athumani Msuya aliteuliwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete (sasa mstaafu) kushika nafasi hiyo iliyoachwa wazi na CP Robert Manumba aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.
Kabla ya uteuzi huo CP Diwani alikuwa Kaimu Kamishna wa Kamisheni ya Intelijensia ya Jinai, ambayo wakati huo ilijazwa na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Valentino Mlowola (sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa - Takukuru).
Siyo jambo la ajabu hata kidogo katika serikali hii kuamka asubuhi na kusikia watu wawili ama watatu ‘wametumbuliwa’ kwa siku moja, hasa kutokana na utendaji kazi wa Rais Magufuli, ambaye inaonekana wazi kwamba, ule utaratibu wa zamani wa ‘kuleana’ wakati makosa yanapofanyika, au kusubiri kuundwa kwa ‘tume’ zisizokuwa na matokeo halisi, umekuwa ukimkera na ndiyo maana ameamua kuchukua hatua mara anaporidhika kwamba ofisa amekiuka viapo vya utumishi wa umma.
Hakuna sababu zilizotolewa, na hakuna ulazima wa kuhoji, lakini daima jibu la hesabu linaweza kuwa sahihi kwa kadiri mtu anavyoitafsiri hesabu yenyewe. 1 + 1 = 2, lakini yaweza pia kuwa 11. Hivyo basi, kutenguliwa kwa uteuzi wa DCI Diwani Athumani kuna kila dalili kwamba kunaendana na kukamatwa kwa meno ya tembo 50, tukio lililotokea Oktoba 30, 2016, yaani siku moja kabla ya Rais Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza Maliasili.
Kikosi Kazi cha Idara ya Wanyamapori kina wajibu wa kukamata wahusika, lakini ni Jeshi la Polisi ndilo lenye mamlaka kwa mujibu wa sheria kuandaa mashtaka dhidi ya wahusika, kazi ambayo inafanywa chini ya Idara ya DCI.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi pamoja na Idara ya Wanyapori, vinaeleza kwamba uhusiano wa matukio hayo ni mkubwa hasa kutokana na ukweli kwamba kesi nyingi za ujangili nchini zimekuwa zikizimika ama wakati mwingine baadhi ya wahusika wakiangaliwa bila kuguswa kwa sababu ambazo hazijulikani.
Wanasema, iwe ni kwa kuwajibishwa kwa kushindwa kuwajibika au la, lakini kuna dalili ambazo zinaonyesha uhusiano wa 'kutumbuliwa' kwa CP Diwani.
Na hii inajidhihirisha baada ya kukamatwa kwa wahusika wa meno hayo ya tembo pamoja na tukio jingine lililotokea siku tatu baadaye baada ya Kikosi Kazi cha Idara ya Wanyamapori, ambacho kinawahusisha maofisa kutoka idara mbalimbali za serikali, kukamata jumla ya bunduki 11 nyumbani kwa mbbunge mmoja wa Chama cha Mapinduzi ambazo inadhaniwa kwamba zimekuwa zikitumika katika vitendo vya ujangili.
Wakati alipozuru Maliasili, Dk. Magufuli alionyeshwa magari yaliyokamatwa yakiwa yamebeba pembe hizo na watuhumiwa nane wanaodaiwa kujihusisha na mtandao wa biashara haramu ya pembe za ndovu.
Na kwa dhati kabisa, akawapongeza askari wote waliopo katika Kikosi Kazi cha kudhibiti na kupambana na biashara haramu ya pembe za ndovu pamoja na raia wema wote wanaotoa ushirikiano katika operesheni hiyo na akawahakikishia kuwa anatambua kazi kubwa wanayoifanya na anawaunga mkono.
“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya na ninawahakikishia kuwa ninawaunga mkono, chapeni kazi, wakamateni wote wanaojihusisha na biashara hii haramu, hakuna wa kumbakiza, awe mkubwa au nani, kamateni, wala msijali cheo chake, umri wake, dini yake, kabila lake, umaarufu wake, sheria ni msumeno, watafuteni wote mpaka watu wakiona tembo wawe wanakimbia wenyewe ili tuokoe wanyama wetu ambao wanaendelea kutekelezwa.
“Hapa mmekamata pembe 50 maana yake tembo 25 wameuawa, haiwezekani maliasili yetu ikawa inapotea hovyo hovyo kwa sababu ya watu wachache wenye tamaa ya kutaka utajiri wa haraka haraka,” akasisitiza Rais Magufuli.
Huu ndio mtazamo wangu.

Comments

  1. duh ! stori nzuri lakini edit hyo tarehe juu kabisa mbona tarehe 29 Novemba 2016 bado,na rais alizaliwa oktoba 29 siyo Novemba

    ReplyDelete

Post a Comment