Featured Post

YANGA KUIBOSHOA TENA JKT RUVU KATIKA MECHI YAO YA 28!



Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
LABDA kuwe na miujiza, lakini ukweli ni kwamba, JKT Ruvu Stars ni vibonde wa Yanga tangu mwaka 1976, na Oktoba 26, 2016 wanapambana katika mechi yao ya 28 kwenye Ligi – hii ikiwa ni pamoja na Ligi ya Ilala na Ligi ya Taifa ambayo ndiyo Ligi Kuu ya sasa. Kama ulikuwa hujui ndiyo nakupasha sasa!
Na katika mechi 27 zilizopita, Yanga imeshinda 17 na kutoka sare 9 huku JKT Ruvu ikiambulisha ushindi wa mechi moja tu. Yanga imepachika mabao 52 wakati imekubali nyavu zake kutikiswa mara 16.

Mwandishi wa Makala haya, ambaye ni mchambuzi na mtafiti wa masuala ya michezo na burudani nchini Tanzania, anakuletea takwimu zote za mechi baina ya Yanga na JKT Ruvu Stars ili kuondoa mashaka yako, kwani wengi wanahoji imekuwaje takwimu hizo ama zina ukweli kiasi gani.
Utafiti uliofanywa na mwandishi wa Makala haya, ambaye anaandaa kitabu cha Ubingwa wa Soka Tanzania kilicho katika hatua za mwisho kabla ya kuchapwa, unaonyesha kwamba, JKT Ruvu Stars ilianza kushiriki Ligi ya Taifa (wakati huo ambayo sasa ndiyo Ligi Kuu) tangu mwaka 1976, ambapo mwaka huo kulikuwa na timu za Pamba ya Mwanza, iliyokuwa na wachezaji kama Joseph Ngowela na Abuu Juma, Pemba SC ya Pemba, JKT Mafinga, Kurugenzi Arusha, Mseto ya Morogoro ambayo ilikuwa bingwa mtetezi, Maji Dodoma, Imara, Elimu Ruvuma, Ruvu Stars, Coastal Stars ya Bagamoyo, Mori FC ya Mara, Ujenzi Rukwa, Ufundi Kigoma, Balimi ya Kagera, Mwenge ya Mbeya,  Nyota Mtwara, Mwadui na TPC ya Kilimanjaro ambayo iliyokuwa na mchezaji hatari Gullam Hussein.
Simba na Yanga nazo zilikuwepo kwenye kinyang’anyiro hicho lakini itakumbukwa kwamba mwaka huo ndio ulishuhudia migogoro mikubwa kwenye timu hizo mbili kongwe kiasi cha kugawanyika. Yanga walikuwa wamegawanyika na kuzaliwa Pan African na Simba waligawanyika na kuzaliwa Nyota Nyekundu.
Mgogoro wa Yanga ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na timu hiyo kushindwa kutetea ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mjini Mombasa, Kenya, wachezaji waandamizi wakaleta mgomo ikabidi uongozi uwafukuze wachezaji 22 wakiwemo akina Gibson Sembuli, Leodgar Tenga, Sunday Manara, Boi Idd 'Wickens', Ally Yusuf, na wengineo.
Baada ya kuwafukuza wachezaji hao, mashabiki wakashuhudia tena matukio mawili makubwa yakifanywa na serikali, ambapo kocha wa Yanga Tambwe Leya kutoka Zaire na yule wa Simba Nabi Camara kutoka Guinea, waliamriwa waondoke nchini haraka kwa kile ambacho kilitafsiriwa kwamba ni sababu za kiusalama. Wapo watu waliodai kwamba makocha hao wawili walikuwa majasusi.
Baada ya kuwafukuza wachezaji hao, Yanga ikaanza kujijenga upya ambapo ilikuwa na wachezaji kama Bernard Madale, Boniface Makomole, Selemani Said Sanga, Charles Mwanga, Sam Kampambe, Mrisho Karaby, Ezekiel Greyson 'Jujuman' (baba yake mwigizaji Aunt Ezekiel), Mwinda Ramadhani ‘Maajabu’, Yanga Fadhila Bwanga, Rashid Tangale, Habibu Kondo, Charles Boniface Mkwasa (kutoka Mseto), Selemani Jongo, Rashid Idd Chama, Ayubu Shaaban, Juma Mkambi, Ahmed Omari, Hashimu Shaaban Kambi 'Ramsey' (kutoka Tumbaku Morogoro), Shaaban Katwila, Gossage Mrisho (Tumbaku Morogoro), na wengineo.
Simba nayo iliundwa na Daudi Salum 'Bruce Lee', Omari Mahadhi, Mohmmed Kajole, Filbert Rubibira, Mohammed Bakari 'Tall', Abbas Said Kuka, George Kulagwa, Nico Njohole, Adamu Sabu, Aballah Mwinyimkuu, Abdallah Hussein ‘Kibadeni’, Abbas Dilunga, Martin Kikwa, Hussein Tindwa, Daniel Mwalusamba, Thuwein Ally, Isihaka Kibene, Yusuf Kaungu, Kihwelu Musa, Mohammed Kajole, Willy Mwaijibe, Aloo Mwitu, Jumanne Hassan ‘Masimenti’, Lucas Nkondola, Kassim Mensah, Abdulkarim Salum 'Johan' na wengineo.
Mseto, mabingwa watetezi walikuwa na kikosi chao cha mwaka uliopita ingawa walikuwa wameongoza wengine. Iliundwa na Said, Hamdan, Mkude, Matola, Aluu Ally, Shiwa Lyambiko, Shilingi, Omari Hussein ‘Keegan’, Manyanga, Spencer, Jumanne, na wengineo.
Nyota Afrika ndiyo ilikuwa imejiimarisha kwa kuwachukua wachezaji wengi kutoka Yanga na iliundwa na Athumani Mambosasa, Juma Shaaban, Ali Yusuf, Boi Iddi, Leodgar Tenga, Omari Kapera, Jella Mtagwa, Muhaji Mukhi, Juma Matokeo, Noah Mikidadi, Sunday Manara, Gibson Sembuli, Edward, na wengineo.
Navy Zanzibar  ilikuwa na wachezaji kama Ali Zaid, Mtumwa, Hamisi, Abddallah, Rajab, Kapenta, Ali, Salhina, Mtwango, Shabani, Kidevu, Saidi, na wengineo, wakati Kilimali ya Singida ilikuwa na akina Yona, Kaiser, Jumanne, Shirz, Elibariki, Mwakipesile, Kassim, Mbaya, Edward, Mohammed, Lupindu na Kessy. Vita ya Tabora ilikuwa na akina Jumanne, Kigozi, Chuma, Peter, Anyelwisye, Leonard, Mansour, Mwenge, Kibonge, Sunday, Oswald, Mkwawa, Mussa, Juma, Mwalekema, Ngalula na wengineo.
Nimejaribu kuwapa historia kidogo ili twende sawa. Sasa tuangalie matokeo ya mechi za Yanga na JKT Ruvu:

Mwaka 1976
Yanga na JKT Ruvu zilipambana Februari 19, 1976 kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam zikianzia kwenye Ligi ya Wilaya ya Ilala. Kwa taarifa yako tu msomaji, ni kwamba utaratibu mzuri wa ligi ya mechi za nyumbani na ugenini ulianzishwa mwaka 1977 na mwanariadha Chabanga Hassan Dyamwale aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), lakini huko nyuma kabla ya kufika hatua ya fainali, timu zililazimika kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa hadi taifa.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda kwa bao 1-0 ambalo lilifungwa na nahodha Mwinda Ramadhan ‘Maajabu’ katika dakika ya 59. Kikosi cha Yanga cha siku hiyo kilikuwa na kipa Isega Isindani, Sudi Pipino, Jaffar Abdulrahman, Selemani Said Sanga ‘Totmund Wanzuka’, Ezekiel Grayson, Selemani Jongo, Ahmad Omar, Ramadhan Mwinda na wengineo.

Mwaka 1977
Michuano ya awali kabla ya hatua ya mwisho ilipangwa kuchezwa kwa kanda. Viwanja vilivyoteuliwa vilikuwa Mkwakwani (zamani Manispaa) - Tanga, Sheikh Amri Abeid - Arusha, Nyamagana - Mwanza, Saba Saba - Iringa, Mapinduzi - Mbeya, Uwanja wa Taifa - Dar es Salaam, na Uwanja wa Amaan - Zanzibar.
Awali katika Ligi ya Ilala, Yanga ilipambana na JKT Ruvu Stars Aprili Mosi, 1977 na kuibanjua mabao 6-1 pale Karume. Mabao ya Yanga yalifungwa na Yanga Bwanga 2’, 78’ pen., na 87’, Ezekiel Grayson 15’, Burhani Hemed 22’, Ramadhan Mwinda 46’ wakati bao la JKT lilifungwa na Silas Wega dakika ya 40.
Kikosi cha Yanga siku hiyo kilikuwa na kipa Said Mzingi, Selemani Said Sanga, Twaha Shaaban ‘Ufunguo’, Ramadhan Mwinda, Ezekiel Grayson, Burhani Hemed, Yanga Bwanga, Shaaban Katwila, Stephen, Ngoye, na Ahmad Omar.
Katika hatua ya Kanda, Yanga na JKT Ruvu zilikuwa katika Kanda ya Mashariki katika kituo cha Morogoro ambapo mechi yao ya Mei 19, 1977 ilishuhudia timu hizo zikifungana bao 1-1. Mwinda Ramadhan ndiye aliyeifungia Yanga bao la kuongoza dakika ya 73 kabla ya Salu Sammy kuisawazishia JKT dakika ya 75.

Mwaka 2005.
Tangu mwaka 1977 JKT Ruvu ilipotea kwenye Ligi ya Taifa hadi mwaka 2002 iliporejea tena, lakini haikukutana na Yanga hadi mwaka 2005. Hii ilitokana na utaratibu wa makundi ambao ulishuhudia timu hizo kila mara zikipangwa makundi tofauti na JKT Ruvu haikuwahi kufuzu kwa hatua ya Nane Bora ambayo ndiyo ilikuwa ya fainali.
Katika mechi ya kwanza iliyofanyika Mei 25, 2005, timu hizo zilifunga bao 1-1 na ziliporudiana Septemba 3, 2005, Yanga ikafunga mabao 2-0 kupitia kwa Salum Athuman na Gula Joshua.

Mwaka 2006
Timu hizo zilipambana Machi 12, 2006 katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ambapo Gaudence Mwaikimba aliipatia Yanga bao pekee na la ushindi katika dakika ya 69 huku mwamuzi Thomas Mkombozi wa Kilimanjaro akiwazawadia kadi nyekundu Nadir Haroub wa Yanga na James Chirwa wa JKT baada ya kurushiana Makonde katika dakika ya 55. Vikosi siku hiyo vilikuwa: Yanga: Ivo Mapunda, Shadrack Msajigwa, Ramadhan Wasso, Nadir Canavaro, Fred Mbuna, Yusuf Hamis, Amri Kiemba, John Barasa, Said Maulid, Benny Mwalala na Gaudence Mwaikimba. JKT Ruvu: Abdallah Ngachuma, Rashid Matambo, Kessy Muhsin, Shaibu Athumani, George Minja, Boniface Simon, Amos Mgisa, Sostenes Manyasi, Bakari Kondo, James Chirwa na Greysin Kundakila.
Katika mechi ya marudiano Julai 25, 2006, timu hizo zilifungana 1-1 ambapo Aziz Kwayu aliipatia JKT bao la kuongoza dakika ya 47 na Hamisi Shabani akaisawazishia Yanga kwa penalty dakika ya 75, mchezo ambao pia ulichezeshwa na Thomas Mkombozi. Vikosi vilikuwa: JKT Ruvu: Abdallah Ngachemwa, Rashid Matambo, Kessy Muhsin, Shaibu Nayopa, Azish Kwayu, Boniface Simon, Grayson Haule, Sostenes Manyasi, Amos Mgisa, James Chirwa/Tambwe Akilimali (85) na Oscar Sangupina/Andrew Tryphon (85).  Yanga: Benjamin Haule, Shadrack Nsajigwa, Fred Mbuna, Lulanga Mapunda/Mohamed Banka (58), Hamis Shaaban, Edwin Mukenya, Kudra Omary, Amri Kiemba, Said Maulid 'SMG', Gaundence Mwaikimba/John Barasa (46) na Abuu Mtiro/Abuu Ramadhani (46).

Mwaka 2007
Mwaka huo, kutokana na utaratibu mpya wa Ligi Kuu kuanza Agosti, ilibidi kuanzisha ligi ndogo ili kuwapata mabingwa na wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa mwaka 2008. Katika ligi ndogo hiyo iliyokuwa katika makundi matatu yaliyokuwa Arusha, Dodoma na Morogoro, Yanga ilikuwa Kundi A huko Arusha pamoja na Arusha FC, Polisi Morogoro na Moro United, wakati JKT Ruvu ilikuwa Kundi C mjini Dodoma pamoja na Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Pan African na ndugu zao Ruvu Shooting Stars.
Timu hizo mbili zilikutana kwenye hatua ya Sita Bora katika Kundi A mjini Arusha ambalo pia lilikuwa na Mtibwa Sugar. Yanga na JKT hazikupata mbabe katika mechi zote mbili – kwanza Juni 27, 2007 zilitoka suluhu, ziliporudiana Juni 30, 2007 zikafungana 1-1, bao la JKT likifungwa na Grayson Haule dakika ya 54 akisawazisha lile la Yanga lililofungwa na Abdi Kassim dakika ya tatu.

Msimu wa 2007/08
JKT Ruvu na Yanga zilikutana katika raundi ya 11 Oktoba 28, 2007 ambapo Mkenya Maurice Sunguti aliipatia Yanga bao la ushindi dakika ya 13 na ziliporudiana Aprili 17, 2008 zikatoka suluhu.

Msimu wa 2008/09
Katika msimu huo Yanga ilianza kukutana na JKT Ruvu Agosti 28, 2008 na ikashinda 2-1 kwa mabao ya Wakenya Boniface Ambani aliyefunga kwa penalty dakika ya 9 na Ben Mwalala dakika ya 41 wakati la JKT lilifungwa na Bakari Kondo dakika ya 40.
Ziliporudiana Januari 17, 2009 Shamte Ally ‘Mgosi’ akaifungia Yanga bao pekee dakika ya 67.

Msimu wa 2009/10
Katika msimu huo, JKT Ruvu iliigomea Yanga kwa sare ya 2-2 ambapo wafungaji wa mabao hayo walikuwa wawili tu. Kigi Makasi aliifungia Yanga mabao yote dakika ya 41 na penalty dakika ya 90+5 wakati Hussein Bunu aliifungia JKT dakika za 65 na 79.
Ziliporudiana Februari 3, 2010, Mrisho Ngassa akaipatia Yanga bao la mapema na la ushindi katika dakika ya kwanza.

Msimu wa 2010/11
Katika msimu huo, mechi ya zote mbili zilishuhudia timu hizo zikitoka suluhu. Kwanza zilitoka suluhu Oktoba 21, 2010 halafu zikashindwa kufungana Machi 12, 2011.

Msimu wa 2011/12
Ushindi pekee ambao JKT Ruvu iliupata dhidi ya Yanga ilikuwa katika mechi ya Agosti 20, 2011 ambapo penalty ya dakika ya 22 ya Kessy Mapande ilitosha kuipa timu hiyo ya jeshi ushindi wa bao 1-0. Ziliporudiana Januari 28, 2012 Yanga ikaishindilia JKT mabao 3-1 JKT ambapo Hamisi Kiiza alifunga mawili na Stephano Mwasika bao moja na Amos Mgisa aliifungia JKT bao la kufutia machozi.

Msimu wa 2012/13
Msimu wote – kama misimu mingine iliyofuata – Yanga iliitandika JKT kadiri ilivyotaka. Kwanza Septemba 22, 2012 ilikung’uta mabao 4-1 ziliporudiana Aprili 21, 2013 ikashinda 3-0.

Msimu wa 2013/14
Novemba Mosi, 2013 Yanga iliichapa JKT Ruvu 4-0, ziliporudiana Aprili 6, 2014 ikashinda 5-1.

Msimu wa 2014/15
Oktoba 5, 2014 Yanga iliifunga JKT 2-1, ziliporudiana Machi 25, 2015 ikaifunga tena 3-1.

Msimu wa 2015/16
Katika mchezo wa kwanza wa msimu huo baina ya timu hizo Septemba 19, 2015 Yanga iliiboshoa JKT mabao 4-1, na katika mechi ya marudiano Februari 7, 2016 ikaifunga tena 4-0.
Swali ni, je, JKT Ruvu Stars imepata dawa ya kuizuia Yanga?


Comments