Featured Post

UDIKTETA, USULTANI ULIINGIA CHADEMA MWAKA 2006 WALIPOFUTA UKOMO WA MADARAKA KWENYE KATIBA




Na Daniel Mbega
FREEMAN Aikaeli Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alikuwa anahamaisha wanachama wake wafanye maandamano Septemba Mosi, 2016 (ambayo yameahirishwa) kwa kile anachokiita ni ‘Operesheni ya Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta)’.
Anasema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli inaendeshwa kidikteta hasa baada ya majaribio yao ya kuitikisa kwa kususia vikao vya Bunge kushindwa huku serikali ikipiga marufuku mikutano yote ya siasa na kuwahamasisha wananchi wafanye kazi za maendeleo.

Mbowe amekwenda mbali zaidi baada ya kuwatisha viongozi wa chama hicho kwamba yeyote ambaye hatashiriki maandamano aliyoyapanga yeye na kuwashawishi viongozi wenzake wayakubali, basi atakuwa amejitoa kwenye uongozi kwa sababu ni ‘msaliti’.
Niliandika hivi karibuni kwamba, lingekuwa jambo la busara sana kama Chadema wangeanza kwanza na Operesheni ya Kupambana na Udikteta ndani ya Chadema (Ukucha) kabla ya kuanzisha Ukuta, lakini baadhi ya watu walinikosoa.
Leo nataka kueleza kwamba, ingawa viongozi wa Chadema wamekuwa na kawaida ya kukanusha kwa nguvu zote huku wafuasi wao wasiopenda kujiongeza kwa kutafakari mara mbili wakiunga mkono, lakini udikteta umeshamiri ndani ya chama hicho na zaidi kuna usultani uliotamalaki.
Udikteta na usultani ndani ya Chadema uliingia rasmi Agosti 13, 2006 pale kwenye Ukumbi wa PTA, kwenye Viwanja vya Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa (Saba Saba) wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa kupitisha Katiba mpya ya chama hicho.
Japokuwa wapo wanachama wa Chadema waliowahi kuthubutu kulisemea hilo lakini wakaitwa ‘wasaliti’, ‘wanatumiwa’ na majina mengine kama hayo, lakini ukweli bado ungali pale pale kwamba kuna udikteta na usultani, ambao daima huwa hauna kikomo cha madaraka.
Demokrasia ya kweli huonyesha ukomo hata wa madaraka, lakini Chadema ambayo inajinasibu kwamba ni chama cha kidemokrasia haina ukomo wa madaraka kwenye katiba yake ya mwaka 2006, kipengele ambacho kiliondolewa makusudi ili kujenga himaya ya udikteta, tofauti na waasisi wa chama hicho – akina Edwin Mtei, Bob Makani na wenzao walivyokuwa wameazimia.
Katiba ya mwaka 2006 inaeleza tu kwamba muda wa uongozi utakuwa wa miaka mitano mitano, lakini haielezi ukomo wa uongozi, kwamba mtu anaweza kushika nafasi hiyo kwa vipindi vingapi.
Ndiyo maana Mbowe ameendelea kukaa madarakani kwa kipindi cha tatu sasa, na huenda akaendelea mpaka atakapoamua mwenyewe kung’atuka, kwa sababu katiba inamruhusu au iko kimya kuhusu ukomo wa kuongoza. Huu ni usultani!
Sasa wanapata wapi ujasiri wa kuikosoa CCM kwamba ina udikteta wakati chaguzi zake, pamoja na kuwepo kwa mapungufu ya hapa na pale yanayowahusu watu binafsi, zimeendelea kufanyika kidemokrasia na ukomo wa uongozi unajulikana?
Ibara ya 6.3.2 ya Katiba ya Chadema ya 2006 kuhusu Muda wa Uongozi inasomeka hivi: (a) Kila uongozi uliochaguliwa au kuteuliwa wakati wa uchaguzi mkuu wa Chama utashika wadhifa wake kwa kipindi cha miaka mitano; (b) Kiongozi aliyechaguliwa au kuteuliwa baada ya uchaguzi mkuu atashika wadhifa wake hadi kipindi cha uchaguzi mkuu kinachofuata; (c) Kiongozi aliyemaliza muda wa uongozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena mradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi; (d) Muda wa uongozi unaweza kufupishwa kama mamlaka iliyochagua au kuteua itaamua hivyo; (e) Ibara hii itahusu pia viongozi wa Mabaraza ya Vijana, Wanawake na Wazee wa CHADEMA.
Katika umri wake wa miaka 24, Chadema imekwishakuwa na Katiba tatu – ile ya mwaka 1992 na ya 2004 pamoja na hii ya mwaka 2006, ambayo ilibadilishwa wakati wa uenyekiti wa Mbowe mwenyewe kwa mara ya pili tangu alipoingia madarakani mwaka 2003 kuchukua nafasi ya Wakili Bob Makani, ambaye kama Mtei, aliongoza kwa kipindi kimoja tu.
Katiba za kwanza mbili – ya 1992 na 2004 – zilikuwa na kipengele cha ukomo wa madaraka na hili lilizungumzwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, lakini akaitwa msaliti na kadhalika.
Mwigamba, akitumia jina la Maskini Mkulima katika mtandao wa Jamii Forums hasa katika kipindi cha mwaka 2013 wakati Zitto Kabwe akiwa anataka kuwania uenyekiti, alisema: “Wakati tukifanya mabadiliko ya katiba mwaka 2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Lakini wakati katiba inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela. Mambo yanayotokea hivi leo yanaonyesha dhahiri kipengele hicho kiliondolewa kwa makusudi kwa maslahi na kwa faida ya viongozi waliopo madarakani kwa sasa. Hiki kinaweza kuchukuliwa kama kitendo kidogo lakini kama viongozi wetu wanaweza kutokuwa waaminifu katika jambo kama hili, ni dhahiri hawawezi kuaminika na wanaweza kufanya mambo mengine makubwa na yenye athari zisizomithirika kwa chama.
“Ni muhimu wanachadema mkafahamu kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho kinacholeta mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania uenyekiti. Kama kingekuwepo leo Mbowe alikuwa anakatazwa na katiba kugombea kipindi cha tatu na hivyo vita iliyopo kati yake na Zitto isingekuwepo na chama kingekuwa imara zaidi. Ni dhahiri Mbowe aliondoa kipengele hicho kwa makusudi ili aweze kuendelea kugombea bila mwisho na huu ni udikteta kama ule tu wa akina Lyatonga Mrema, John Cheyo na wengineo, na wanachadema hatupaswi kuuruhusu si kwa Mbowe tu bali kwa yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa chama chetu.”
Mwigamba, ambaye alikuwa Katibu Mkuu mwanzilishi wa Chama cha ACT-Wazalendo kabla ya kwenda masomoni Nairobi hivi karibuni, alisema wakati huo kwamba, Katiba ya mwaka 2004 ipo wazi kabisa katika hoja ya ukomo wa madaraka ambapo Ibara ya 6.3.2 kipengele cha (c) kinasema ifuatavyo; ''Leaders who finish their term of office can be eligible for re-election provided he qualifies but no leader can hold the same post at the same level of the party structure for more than two terms.”
Licha ya ufafanuzi huo, bado viongozi wa chama hicho wakati huo walisimama kidete kukanusha, huku aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa, akinukuliwa ndani ya mtandao huo akisema: “WanaJF, Nataka kuwahakikishia wanachadema wote, kuwa nilikuwepo nimekuwa ndani ya Chadema kuanzia 1998 ambapo nilikuwa Makamu Mwenyekiti Bara, na baadaye 2003 Kaimu Katibu Mkuu, na hatimaye Katibu Mkuu. Hivyo nimeshiriki kikamilifu kuandaa Katiba ya 2004 na pia Katiba ya 2006 baada ya Rebranding ya Chama. Nataka niwahakikishie wanachadema, hakuna toleo lolote la Katiba ndani ya Chadema imeweka "muda wa Uongozi kuwa vipindi viwili tu", kuanzia Katiba aliyoiasisi Mzee Mtei na kupitishwa na Mkutano Mkuu, wala si ya 2004 au ya 2006. Kama kuna mtu anasema ilikuwepo na imeondolewa kinyemela, basi aonyeshe kifungu hicho kwenye Katiba yeyote ile, au miniti za kikao chochote kile.”
Lakini kauli hiyo ilipingana na kauli ya Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika, ambaye naye katika mjadala huo alijitokeza na kusema kwamba kipengele cha ukomo wa uongozi kilikuwemo kwenye Katiba ya 2004 lakini hakikuingizwa kwenye katiba ya 2006.
Mnyika alinukuliwa akisema: “Kuhusu Katiba, nina nakala mango (hard copy) tu ya katiba ya 2004, ilikuwa na kipengele cha vipindi viwili vya nafasi ile ile. Hata hivyo, katiba mpya iliyoandikwa mwaka 2006 haikuwa na kipengele hicho. Hivyo, sio kwamba kimeondolewa kinyemela ila hakikuwepo kwenye katiba mpya. JJ”
Hii maana yake ni kwamba, hata Dk. Slaa kama Katibu Mkuu, alisema uongo kwamba hakukuwa na kipengele cha ukomo wa madarakani, hii inaonekana kwamba kuna jambo ambalo limefichikia kuanzia katika uandaaji wa katiba ya 2006 mpaka jinsi walivyoipitisha.
Taarifa zinaeleza kwamba, Mkutano Mkuu Maalum wa mwaka 2006 ulikuwa na agenda nne tu ambazo ni Mosi, Kufungua Mkutano; Mbili, Maboresho ya Katiba; Tatu, Maazimio juu ya Katiba Mpya; na Nne, Kufunga Kikao.
Inaelezwa kwamba, mkutano huo ulijadili vifungu 10 ambavyo vilifanyiwa marekebisho kutoka kwenye katiba ya 2004, lakini kati ya vipengele hivyo, kipengele cha ukomo wa madaraka hakikuwemo na hii ni kusema kuwa hoja hiyo haikuwa na marekebisho.
Wapo wafuasi wa Chadema, hususan ambao daima ni watiifu kwa uongozi na hutetea hata kama kuna uozo, wanaodai kwamba katiba ya sasa ni ya wanachama, lakini pia wapo baadhi yao ambao wanasema katiba hiyo inaakisi matamanio ya viongozi waliotangulia, jambo ambalo linaleta mshangao.
Hoja hii, ambayo imewahi kujadiliwa kwa mapana huko nyuma katika mitandao ya kijamii, bado ina mantiki katika kipindi hiki, kwani ni Dhahiri usultani na udikteta upo ndai ya chama hicho na ndiyo sababu kabla Zitto hajaondoka, kila alipotaka kugombea aliwekewa vizingiti kwa kuwa waliamini angeweza kumng’oa Mbowe madarakani.
Kwamba, hata sasa akitokea mpinzani wa kweli ndani ya Chadema ataonekana ni adui na kupewa sifa mbaya mbele ya wanachama na wananchi kwa ujumla kwa kuwa kumruhusu mtu wa aina hiyo itakuwa ni kuukomesha usultani.
Leo hii, kwa sababu ya nguvu kubwa waliyopewa viongozi na upungufu wa kikatiba uliopo, lolote litakalosemwa na Mwenyekiti na kuvikwa kofia ya ‘Uamuzi wa Kamati ya Utendaji’ litapigiwa makofi na wafuasi wao hata kama lina walakini, kama tunavyoshuhudia suala la Ukuta.
Mbowe ndiye Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, lakini kwa kofia yake ya uenyekiti wa Chadema, wakati alipoinuka Bungeni na kususia vikao, wabunge wote wa chama hicho waliamua kutii hata kama wao binafsi waliona hakuna sababu.
Ndiyo. Inawezekana mtu anasukumwa na hisia zake binafsi, lakini kwa demokrasia feki iliyopo ndani ya Chadema, hata wabunge nao wamekuwa wakifuata mkumbo huo kwa kuhofia ‘kuanzisha bifu na uongozi’ japokuwa waliowatuma waende Bungeni ni Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao.
Katika Kata au Majimbo waliyoshinda, Chadema hawana idadi kubwa ya wanachama kama waliowachagua, bali wengine walitoka katika vyama vingine ikiwemo CCM yenyewe, hilo hawawezi kulikanusha.
Kwa hiyo basi, ni vyema Chadema wakakomesha udikteta na usultani kwa kuweka ukomo wa uongozi ndani ya katiba yao ili waonekane wanafuata demokrasia, kinyume chake hawana tofauti na viongozi wengine wanaong’ang’ania kukaa madarakani kwa kuwa tu ‘wamezichezea’ katiba zao.

Comments

  1. In politics, what is logical is not always practical; what is practical is not always right; what is right is not always ethical; what is ethical is not always desired; and what is desired is not always logical!

    ReplyDelete

Post a Comment