Featured Post

UBINGWA WA SOKA TANZANIA ULIPOKWENDA NJE YA DAR KWA MARA YA KWANZA 1975



Kikosi cha Mseto FC kilichotwaa ubingwa mwaka 1975. Charles Mkwasa ni wa tano kutoka kulia waliosimama.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
MWAKA 1974 Yanga iliifunga Simba mabao 2-1 katika mchezo wa fainali kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, ukiwa ndio mchezo wao wa pili katika historia yao kufanyika nje ya Dar es Salaam baada ya ule wa kirafiki uliofanyika mwaka 1959 mjini Dodoma na Simba (wakati huo ikiitwa Sunderland) ikafungwa mabao 3-1 mbele ya Malimu Julius Kambarage Nyerere, Mwenyekiti wa Chama cha TANU kilichokuwa kikipigania uhuru wa Tanganyika wakati huo.

Michuano ya Ligi ya Taifa mwaka 1975 ilishuhudia Simba wakishindwa kuingia hatua ya fainali, kwa sababu wakati huo ilibidi timu zote zianzie ngazi za chini kabisa, yaani Ligi ya Wilaya na Mkoa.
Simba, chini ya kocha wake Nabi Camara kutoka Guinea, ilikuwa na wachezaji wengi wa mwaka uliopita akina John Semainda, Daudi Salum 'Bruce Lee', Omari Mahadhi, Mohmmed Kajole, Filbert Rubibira, Mohammed Bakari 'Tall', Jumanne Hassan ‘Masimenti’ (kutoka Yanga), Abbas Said Kuka, George Kulagwa, Nico Njohole, Adamu Sabu, Aballah Mwinyimkuu, Abdallah Hussein ‘Kibadeni’, Abbas Dilunga, Martin Kikwa, Hussein Tindwa, Thuwein Ally ‘Watakiona’, Isihaka Kibene, Yusuf Kaungu, Kihwelu Musa, Mohammed Kajole ‘Machela’, Willy Mwaijibe, Aloo Mwitu, Shaaban Baraza, Omari Gumbo, Lucas Nkondola, Khalid Abeid, Omari Chogo 'Chemba', Haidari Abeid 'Muchacho', Juma Abeid Mzee ‘360 Degree’, na Emmanuel Albert Mbele ‘Dubwi’.
Yanga nayo, ikiwa inaendelea kunolewa na Tambwe Leya kutoka Zaire, ilikuwa imewasajili tena Elias Michael ‘Spring’, Muhidin Fadhil, Patrick Nyaga, Leodegar Tenga, Omari Kapera ‘Mwamba’, Boi Iddi 'Wickens', Juma Shaban, Jella Mtagwa, Juma Matokeo, Sunday Manara ‘Computer’, Kitwana Manara ‘Popat’, Gibson Sembuli, Muhaji Mukhi, Ally Yusuf, Ali Selemani, Leonard Chitete, Kaburu, Bona Max Mwangu, Ahmed Omari, Hassan Gobbos ‘Wa Morocco’, Athumani Kilambo, Adam Juma, Gilbert Mahinya, Abdulrahman Juma (nahodha), Mohammed Rishard ‘Adolf’, Moshi Hussein 'Dayan', Selemani Said Sanga ‘Totmund Wanzuka’, Adam Juma, na Maulid Dilunga ‘Mzee wa Mexico’.
Timu ya Nyota kutoka Mtwara mwaka huo ilikuwa imara sana na ilikuwa na wachezaji kama Zimbo, Dogoa, Okello, Mohammed Mkandinga, Chohan, Bomba, Kibonge, Namajojo, Joseph, Bhulji, Kwasa, Mchuru, na wengineo, wakati Mseto ya Morogoro iliyokuwa inafundishwa na mchezaji wa zamani wa Yanga, Mohemmed Hussein Hassan 'Msomali' ilikuwa na wachezaji kama Said Ramadhan, Ahmad Rajab, Ahmad Maggid, Miraji Salum, Ramadhan Matola, Athumani Matola, Vincent Mkude, Jaafar Mohammed 'Spencer', Hassan Shilingi, Hussein Ngulungu, Mohammed Manyanga, Omar Hussein, Aluu Ali, Shiwa Lyambiko, na Charles Boniface Mkwasa.
Timu nyingine zilizoshiriki michuano ya mwaka huo zilikuwa ni Miembeni ya Zanzibar, Nyuki ya Kigoma, Pamba ya Mwanza, Kisarawe ya Pwani, Jumuiya ya Arusha, Mwadui ya Shinyanga, TPC ya Kilimanjaro, Maji Dodoma, Balimi ya Bukoba, Usalama Dar es Salaam, Jeshi Zanzibar, Vita Tabora, Kilimali ya Singida, Mazao Iringa, Nchi Yetu Lindi, Elimu Ruvuma, Kilimo Mara, Coastal Stars ya Pwani, Comworks (Ujenzi) Rukwa, na Comworks (Ufundi) Mbeya ambayo ndiyo Tanzania Prisons ya sasa.
Kwa ukiangalia utaona kwamba karibu nyingi kati ya timu hizi zilikuwa za kazini.
Mashindano ya mwaka 1975 yalikuwa ya mtoano na yalifanyika mjini Dar es Salaam. Mashabiki wa soka walikuwa na wasiwasi kwamba ligi ya mwaka huo isingekuwa na msisimko kwa kuwa Yanga na Simba zisingeweza kukutana. Hata hivyo, wasiwasi wao ulitoka baada ya kuibuka timu kutoka mikoani ambazo zilikuwa zinacheza soka la uhakika. Hizi zilikuwa Mseto ya Morogoro na Nyota ya Mtwara ambazo ndizo zilizofuzu kwa fainali.
Timu nyingi, hata zile ngeni, mwaka huo zilionyesha upinzani wa nguvu sana hadi kulazimisha mshindi apatikane kwa njia ya penati baada ya dakika 90 za mchezo kushindwa kutoa mshindi. Kama ingekuwa ligi, ambapo mshindi alipata pointi mbili na pointi moja kwa kila timu zilizotoka sare, ingekuwa afadhali, lakini kwa kuwa ilikuwa ni mtoano, penati hazikuwa na budi kutumika. Mtindo wa ligi kamili ulikuja baadaye kabisa.
Msisimko mwingine ulikuja baada ya michezo kadhaa kurudiwa baada ya malalamiko.
Kwa ujumla timu za nje ya Dar es Salaam zilileta ushindani wa kutosha. Ingawa mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na timu mbili - mabingwa watetezi Yanga na Usalama (Polisi waliokuwa mabingwa wa Mkoa) timu hizo zilifungwa na hazikuweza kufika fainali.
Yanga ilifungwa na Mwadui ya Shinyanga kwa penati 3-2 baada ya kutoka suluhu wakati Usalama ilifungwa mabao 5-3 na Mseto ya Morogoro, timu ambayo ilionyesha maajabu makubwa mwaka huo.
Hadi kufika fainali, kwanza Mseto ililaza Jumuiya Arusha kwa mabao 3-2 katika mchezo uliofanyika Julai 18, 1975 na kuchezeshwa na Gration Matovu ambapo wafungaji wa Mseto walikuwa Omar Hussein (penati dakika ya 10) na Aluu Ali dakika za 35 na 48, wakati mabao ya Jumuiya yalifungwa na Marandu Mkubwa dakika ya 47 na Makula dakika ya 75.
Vikosi vyao siku hiyo vilikuwa: Mseto: Said Hashim, Hamdani, Vincent Mkude, Miraji, Matola, Charles Boniface Mkwasa, Shiwa Lyambiko/Mohammed Manyanga, Shilingi, Omar, Aluu Ali, Jaafar Mohammed ‘Spencer’.
Jumuiya: Tito, Darabu, Makula, Kiluwa/Mkamba, Nyanda, Okwirini, Bukuku, Marand Mkubwa, Mhina/Owino, Focus, na Martin/Joseph.
Katika mechi yao ya pili Julai 23, 1975, Mseto waliitandika Kilimo Mara mabao 2-1 huku mabao ya washindi yakifungwa na Aluu Ali dakika ya 58 na Shiwa Lyambiko dakika ya 70 wakati Mwambeni aliifungia Kilimo bao la kuongoza dakika ya 5.
Kwenye mchezo wa nusu fainali Julai 26, 1975, Mseto iliitoa Usalama Dar kwa penati 5-3.
Kwa upande mwingine, Nyota Mtwara ilianza kwa kuichakaza Mazao Iringa kwa mabao 6-1 katika mechi iliyofanyika Julai 21, 1975. Mabao ya Nyota yalifungwa na Said Dogoa (penati dakika ya 15), Joseph alifunga matatu dakika za 25, 40, na 62, Namajojo akafunga dakika ya 35, na Mahmoud wa Mazao alijifunga dakika ya 75 katika jitihada za kuokoa. Bao pekee la Mazao lilifungwa mapema katika dakika ya 6 na Kessy Kibuda.
Mchezo wao wa pili uliwakutanisha na jirani zao, Nchi Yetu Lindi (zamani ikijulikana Young Africans Lindi), ambapo Nyota walishinda kwa mabao 5-0 hapo Julai 26, 1975.
Katika nusu fainali walikumbana na Balimi ya Bukoba ambapo waliishindilia mabao 4-0 hapo Julai 29, 1975.
Baada ya michezo ya nusu fainali, Nyota Mtwara na Mseto ndizo zilizofuzu kwa fainali, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya ligi hiyo kwa mchezo wa fainali kuzikutanisha timu kutoka nje ya Dar es Salaam.
Pambano hilo lilichezwa Jumamosi Agosti 2, 1975 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Umati wa maelfu ya watazamaji waliohudhuria pambano hilo walishuhudia timu hizo ngeni katika fainali zilivyoonyesha kandanda la kusisimua na kuondoa dhana kwamba ligi hiyo ni ya Yanga na Simba tu.
Vijana wa Morogoro, ambako ndiko liliko chimbuko la vijana wengi wacheza soka kwa miaka mingi, walionyesha wazi kwamba wanaweza kulisukuma gozi baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 3-1.
Bao la kwanza lilipatikana katika dakika ya saba ya mchezo mfungaji akiwa Hassan Shilingi baada ya kuunganisha krosi ya Shiwa Lyambiko. Nyota Afrika hawakukata tamaa na juhudi zao zilizaa matunda baada ya kusawazisha kwa njia ya penati katika dakika ya 18. Omari Hussein, ambaye baadaye alikuja kpachikwa jina la utani la 'Keegan', aliwainua wapenzi wa Mseto baada ya kupachika bao la pili katika dakika ya 30 na hadi timu hizo zinakwenda kupumzika matokeo yalikuwa 2-1.
Mseto walikianza kipindi cha pili kwa kasi ya kulinda lango lao na kutafuta mabao mengine na katika dakika za majeruhi walifanikiwa kupachika bao la tatu lililofungwa na Shiwa Lyambiko kwa mkwaju wa mbali, kama mita thelathini hivi. Shiwa alikuwa anasifika sana kwa kuwa na mashuti makali. Hadi kipenga cha mwisho kinapulizwa Mseto walikuwa 3 na Nyota Mtwara 1.
Wachezaji walioziwakilisha timu hizo katika mchezo huo wa fainali walikuwa: Mseto: Said Ramadhan, Hamdan, Charles Boniface Mkwasa, Vincent Mkude, Ramadhan Matola, Alluu Ali, Shiwa Lyambiko, Hassan Shilingi, Omari Hussein, Mohammed Manyanga, Jaafar Mohammed 'Spencer', na Jumanne Hassan Masimenti.
Nyota Mtwara: Zimbo, Said Dogoa, Okello, Mohammed Mkandinga, Chohan, Bomba, Kibonge, Namajojo, Joseph, Bhulji, na Kwasa/Mchuru.
Taarifa hizi zimenyofolewa katika mswada wa kitabu cha UBINGWA WA SOKA TANZANIA cha mwandishi mkongwe wa michezo nchini Tanzania, Daniel Mbega. Kitabu hicho kipo katika hatua za mwishoni kuingia mitamboni.


Comments

  1. Jumanne Masimenti hakutoka Yanga huyu alitoka Cosmopolitan kwenda Simba

    ReplyDelete
  2. Jumanne Masementi alitokea Cosmopolitan kwenda Simba hakutokea Yanga

    ReplyDelete

Post a Comment