Featured Post

TULIVYOKITELEKEZA KILIMO CHA NAZI, SASA TUNANUNUA TUI VIWANDANI!


Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
MABADILIKO ya tabianchi hayajafagia miti na misitu pekee, bali yamefyeka hata miti ya asili ya matunda ambayo ilikuwa inatoa vyakula bora visivyo na kemikali.
Tunashangaa kuona wazee wetu walikuwa wakiishi umri mrefu tena bila kusumbuliwa na maradhi licha ya kutokuwepo na hospitali kama ilivyo sasa. Siri kubwa ya wao kuishi umri mrefu ni pamoja na ulaji wa vyakula hai, visivyo na kemikali kwa sababu vilichumwa shambani na kupikwa au kuliwa vikiwa vibichi. Hakuna mbolea za kemikali zilizotumika kukuza mazao hayo.
Leo hii hospitali zipo tele lakini magonjwa nayo yameongezeka. Vyakula vya asili vimepotea, au tuseme utandawazi umevipoteza kwani watu wengi wanaoishi mjini – hata baadhi ya waishio vijijini – kula dagaa, mlenda kama ule wa kwetu wa Ugogoni ambao tonge linaweza kuondoka na bakuli au mchunga kama wa ndugu zangu Wadigo wanaona ni ushamba na ufukara.
Tena kuunga mboga kwa kutumia viungo vya asili kama karanga na nazi hawapendi, bora hata sasa wameanza kukimbilia mafuta ya alizeti yasiyo na lehemu (cholesterol) na mafuta ya mawese. Wengine hawataki nazi za kuangua wanakwenda kununua tui la nazi lililotengenezwa viwandani!
Nazi (Cocos nucifera) ni zao ambalo lilipata umaarufu tangu karne ya 16 hasa Visiwani Pemba, Unguja na Mafia wakati wa utawala wa Waarabu ambao ndio walioleta minazi. Wakaisambaza Bara katika kisa kilichozaa jina la Dar es Salaam badala ya Mzizima (nitawaeleza kisa hicho wakati mwingine).
Kwa hiyo kwa muda mrefu minazi ilikuwa ikilimwa katika visiwa hivyo pamoja na miji yote ya mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi kama Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara na Tabora ambako kuna joto na mazingira kama ya Pwani.
Wananchi wengi wa mikoa hiyo walikuwa wakipata faida kubwa kwa kuvuna nazi, huku wale wa Unguja na Pemba wakisafirisha nazi zao kupeleka Arabuni ambako soko ni kubwa. Minazi iliyokuwa ikilimwa zaidi Pemba na Unguja ni aina ya kisamli na kipenda.
Minazi iliyokuwepo mingi ina miaka zaidi ya 100, ilipandwa zamani sana.
Jitihada za wazee wetu kupanda minazi mingine baadaye hazikuwa endelevu na hakuna vijana walio tayari kuingia kwenye kilimo hicho kwa kuwa tu “Minazi inachukua muda mrefu hadi kuzaa!”
Matokeo yake tunashuhudia tui la nazi likiuzwa kwenye pakiti baada ya kutengenezwa viwandani! Ajabu kubwa. Pengine utafika wakati hata maji ya madafu nayo yatatengenezwa viwandani kwa sababu tumekipa kisogo kilimo cha nazi, ambacho mbali ya kuleta kipato kwa maana ya fedha, lakini pia mizizi na matunda yake yana faida kubwa kiafa.
Kama nazi itakunwa na kutengenezwa tui likapikiwa wakati huo huo haina mamdhara ya kuongeza lehemu mwilini, lakini ukiikuna halafu ukalihifadhi tui hilo maana yake unaruhusu lichanganyike na hewa ya haidrojeni na kufanana na mafuta ya viwandani yenye kemikali na lehemu.
Lakini ikumbukwe tu kwamba, nazi ni miongoni mwa vyakula vichache sana duniani ambavyo watu wengi hawana mzio (allergy) navyo kwa sababu ya faida zake nyingi kama kupunguza wingi wa sukari mwilini huku maji yake (maji ya dafu) yakisafisha kibofu cha mkojo.

Mnazi ni nini?
Kitalu cha minazi
Kwa mujibu wa wanasayansi, mnazi au kwa jina la kisayansi cocos nucifera, ni mti jamii ya mipama (palms) kutoka familia ya arecaceae na ndiyo spishi pekee kutoka kwenye jenasi ya Cocos inayokubalika kwa chakula.
Mnazi unaweza kuwa na urefu wa hadi futi 98 (takriban meta 30) huku makalala (matawi) yake yakifikia urefu wa futi 13-20 (meta 4 hadi 6), na makuti yakiwa na urefu wa kati ya futi 60-90.
Katika udongo mzuri wenye rutuba, mnazi mrefu unaweza kuzaa nazi 75 kwa mwaka, lakini uzaaji huo katika sehemu nyingi ni nazi 30 au chini ya hapo kutokana na utunzaji mbovu. Mnazi unaweza kuzaa matunda yake ya kwanza katika kipindi cha miaka sita hadi 10, huku kilele chake cha uzaaji kikiwa katika miaka 15 hadi 20.
Pamoja na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, lakini mnazi unaotunzwa vizuri unaweza kutoa kiasi cha makole matano kwa kila janguo (uzazi mmoja). Kole moja kwa wastani huwa na nazi kumi, hivyo kwa janguo moja unaweza kupata nazi 50.
Mnazi ndio mti pekee duniani ambao una faida kutoka kwenye mizizi, shina, matawi na matunda yake – hakiachwi kitu.
Matumizi ya nazi ni mengi; wengine wanatumia mizizi ya minazi kama dawa ya pumu na tumbo. Mizizi hiyo huchemshwa na mgonjwa hunywa maji yake.
Shina lake hupasuliwa mbao na mbao zake ni imara zisizoliwa na wadudu. Majani yake, yaani makuti, hutumika kuezekea nyua na nyumba. Njiti za majani, yaani chelewa, hutengenezwa fagio, makalala (yale matawi yake) yakikauka huwa kuni.
Tunda changa kabisa huitwa kitale ambalo baadaye hukua na kuwa kidaka, ambacho hukua na kuwa dafu kabla ya kukua tena na kuwa koroma, ambayo hupevuka na kuwa nazi.
 Dafu
Mbata (nazi iliyokomaa na kukauka maji) hutumika kutengeneza mafuta ya kupikia, mafuta ya nywele, sabuni za kuogea na kufulia.
 Mbata
Madafu ni chakula kizuri na maji yake ni kinywaji kitamu. Tui la nazi ni kiungo cha chakula. Machicha ambayo hutokea baada ya kukamuliwa kwa tui, hutengenezwa kashata. Pia hutumika kusafishia mikeka, miswala na makawa. Machicha hayo pia ni chakula kizuri cha mifugo.
Makumbi ya nazi hutumika kwa kuni, kutengeneza kamba, fagio, matandiko, mazuria na vitu vingine vingi. Pia yakisagwa ni mbolea nzuri sana.
Vifuu vyake hutumika kutengenezea vifungo vya nguo, kata, pawa, mapambo na hata hutumika kama kuni.
Kwa ujumla hakuna hata sehemu moja ya mnazi isiyo na thamani na usisahau kwamba mafuta ya nazi ni mazuri kwa kupikia na kujipaka.

Nchi zinazozalisha nazi kwa wingi
Indonesia ndiyo inayoendelea kuongoza kwa uzalishaji wa nazi duniani ikiwa inazalisha asilimia 35.8 ya mbata. Kwa mwaka 2015 nchi hiyo ilizalisha tani milioni 19.5 ikifuatiwa na Philippines ambayo ilizalisha tani milioni 18.3.
India, ambayo pamoja na Indonesia ndiyo inayotajwa kwamba ni asili ya minazi, mwaka 2015 ilishika nafasi ya tatu kwa kuzalisha tani milioni 11.93 za mbata huku Brazil ikiwa ya nne kwa kuzalisha tani 2,820,468.
Katika orodha ya nchi 10 vinara wa uzalishaji wa mbata duniani, Sri Lanka ilishika nafasi ya tano kwa kuzalisha tani milioni 2.2; Vietnam nafasi ya sita kwa kuzalisha tani 1,312,200; Papua New Guinea ilizalisha tani milioni 1.2; Mexico ilizalisha tani milioni 1.1; Thailand ilizalisha tani milioni 1.01; na Malaysia ilizalisha tani 605,000.
Nazi zina soko kubwa duniani kwa sababu mbata inauzwa viwandani ili kutengeneza mafuta.
Tafadhali, endelea kutembelea www.maendeleovijijini.blogspot.com ili kujifunza masuala mbalimbali ya ujasiriamali, kilimo na ufugaji endelevu.

Kwa mawasiliano nipigie au nitumie ujumbe wa whatsapp kupitia namba 0656-331974, au niandikie barua pepe: maendeleovijijini@gmail.com. Twitter @MaendeleoVijiji; Facebook: Rural Development; Instagram #maendeleovijijini. Daima usikose kutembelea: www.maendeleovijijini.blogspot.com.

Comments