Featured Post

SIMBA NA YANGA NANI MBABE? #HAPAKAZITU! KATIKA UTAWALA WA MAGUFULI




Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
JUMAMOSI Oktoba Mosi, 2016 wakati mwanandinga maarufu wa Liberia, George Tawlon Manneh Oppong Ousman Weah, atakata keki ya kutimiza miaka 50, Yanga na Simba watakuwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuchukuana katika mechi ya kwanza ya msimu wa 2016/17 ikiwa ni mechi ya pili ndani ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli.

MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, Weah, ambaye ni Seneta wa Jimbo la Montserrado nchini Liberia kupitia chama cha Congress for Democratic Change – CDC, ataungana na mwanasoka mwingine Julio Cesar Baptista wa Brazil atayekuwa anatimiza miaka 35.
Lakini wanasoka hao wataungana na Rais wa 39 wa Marekani, Jimmy Carter na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, kusherehekea siku ya kuzaliwa. Jimmy Carter atatimiza miaka 92 wakati Theresa May atatimiza miaka 60.
Simba na Yanga zitaingia uwanjani zikiwa katika hatua tofauti katika raundi hiyo ya saba, kwani wakati Simba itaingia ikiwa kileleni mwa ligi hiyo kwa pointi zake 16 baada ya mechi sita, Yanga yenyewe inashika nafasi ya tatu kwa pointi 10 baada ya kushuka dimbani mara tano.
MaendeleoVijijini inajua kwamba, Simba itaingia dimbani ikiendelea kusherehekea ushindi wake mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Maji Maji ya Songea Septemba 24, 2016 huku Yanga ikiwa na jeraha kubwa baada ya kucharangwa panga moja katika Stand ya Shinyanga Jumapili, Septemba 25.
Baada ya kuokota ‘almasi’ 2-0 pale Mwadui, Yanga ilikuwa na uhakika wa kuikaribia Simba endapo ingeshinda kwenye Stand ya Shinyanga, lakini ikajikuta ikichapwa bao hilo la pekee na kuzima ndoto zake.
Swali kubwa lililopo ni kwamba, nani atakuwa mbabe katika utawala wa awamu ya tano wa Rais Magufuli baina ya timu hizo mbili kongwe?
Tumeshuhudia katika mechi ya mwisho ya msimu wa 2015/16 iliyofanyika Februari 20, 2016 wakati Yanga ilipoigaragaza Simba kwa mabao 2-0, lakini hiyo inaweza isiwe kigezo cha kwamba Msimbazi wanaweza kuendelea kuomboleza na Jangwani wanafanya sherehe.
Hii inatokana na ukweli kwamba, mechi baina ya timu hizo mbili huwa haitabiriki hata kama mojawapo ya timu hizo itakuwa inafanya vibaya kuliko nyingine.
Simba inaonekana msimu huu imepania hasa baada ya kukosa ubingwa kwa misimu minne iliyopita tangu ilipoibuka bingwa katika msimu wa 2011/2012.
Kejeli wanazozipata kutoka kwa mahasimu wao ‘Wa Kimataifa’ zimeipa nguvu mpya Simba kurekebisha makossa yake na sasa inaonekana imejiimarisha zaidi na dhamira yake ni kunyakua ubingwa.
Katika kipindi cha awamu ya nne, Simba iliitawala Yanga kwenye Ligi Kuu ikiwemo kuichakaza kwa mabao 5-0 katika mechi ya marudiano ya msimu wa 2011/12, matokeo ambayo bado yanaonyesha kovu kubwa kwa vijana hao wa Jangwani.
Kati ya mechi 20 walizocheza wakati wa awamu ya Jakaya Kikwete, Simba walishinda mechi sita wakati Yanga ilishinda mechi tano tu, huku timu hizo zikitoshana nguvu mara tisa ingawa Yanga ndiyo iliyoongoza kwa kufunga jumla ya mabao 23 dhidi ya 21 ya watani wao wa jadi.
Yanga itatokea Pemba safari hii ambako ilikwenda kutafuta ubani ili iweze kuendelea kuiadhibu Simba kwa mara ya tatu mfululizo wakati Simba wao wako jijini Dar es Salaam wakijiandaa vilivyo na mtanange huo.
Matokeo yao yaliyopita, ambayo MaendeleoVijijini inayo, ni kama yafuatavyo:

Mwaka 2006
Katika msimu huo mechi zote mbili timu hizo zilitoka suluhu. Kwanza Machi 25 na hata ziliporudiana Oktoba 29. Yanga ikaibuka bingwa kwa pointi zake 70 wakati Simba ilishika nafasi ya pili kwa pointi 62.

Ligi Ndogo 2007
Kutokana na mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa ligi, kwamba inabidi ianze mwezi Agosti, mwaka 2007 TFF ililazimika kuendesha ligi ndogo ili kuwapata wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa 2008.
Simba na Yanga zilikwepana kwa kupangwa tofauti katika hatua ya makundi ambayo yalikuwa Arusha, Dodoma na Morogoro n ahata katika hatua ya Sita Bora, bado zilipangwa tofauti.
Yanga iliongoza kundi la Arusha na Simba ikaongoza kundi la Morogoro, hivyo zikakutana fainali Julai 8, 2007 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro mbele ya watazamaji 9,758.
Mechi hiyo iliyochezeshwa na Victor Mwandike ilishuhudia Simba ikipata bao la kuongoza dakika ya pili tu ya mchezo kwa mkwaju wa penalty ya Mkenya Moses Odhiambo, lakini Yanga ikasawazisha katika dakika ya 56 kupitia kwa Said Maulid, matokeo ambayo yalidumu hadi katika muda wa nyongeza hivyo kulazimisha kupigwa mikwaju ya penalty, ambapo Simba ilipata penalty 4 na Yanga ikapata 3, hivyo Msimbazi wakawa mabingwa.

Msimu wa 2007/08
Katika msimu huo, Simba iliifunga Yanga katika mechi ya kwanza Oktoba 24, 2007 kwa bao la Ulimboka Mwakingwe katika dakika ya 32 na ziliporudiana Aprili 27, 2008 zikatoka suluhu.
Hata hivyo, msimu huo Yanga iliibuka bingwa kwa kufikisha pointi 49 wakati Simba ilishika nafasi ya tatu kwa pointi zake 42. Prisons ya Mbeya ndiyo iliyoshika nafasi ya pili baada ya kukusanya pointi 45.

Msimu wa 2008/09
Mechi ya kwanza ya watani wa jadi Oktoba 26, 2008 ilishuhudia Ben Mwalala akiipatia Yanga bao pekee la ushindi dakika ya 16 na ziliporudiana Aprili 19, 2009 zikatoka sare ya 2-2.
Yanga ilitwaa ubingwa msimu huo, lakini ilikuwa imefungiwa na TFF kushiriki michuano yote ya kimataifa kutokana na kitendo chake cha kugombea mechi yake na Simba ya kutafuta mshindi wa tatu wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 2008.

Msimu wa 2009/10
Bao la dakika ya 25 la Mussa Hassan Mgosi liliipatia ushindi Simba Oktoba 31, 2009, na ziliporudiana Aprili 18, 2010, Yanga ikalala tena kwa mabao 4-3. Mabao ya Simba yalifungwa na Uhuru Selemani (dk. 3), Mgosi (dk. 53 na 73), na Hilary Echesa (dk. 90+) wakati ya Yanga yalifungwa na Athumani Idd ‘Chuji’ (dk. 31), Jerry Tegete (dk. 67 na 88pen.).
Msimu huo Simba ndio walioibuka mabingwa kwa kufikisha pointi 62 dhidi ya 49 za Yanga iliyoshika nafasi ya pili.

Msimu wa 2010/11
Jerry Tegete aliipatia Yanga bao pekee na la ushindi katika dakika ya 79 kwenye mchezo wao wa kwanza Oktoba 16, 2010, lakini ziliporudiana Machi 5, 2011 zikafungana 1-1 huku Stephano Mwasika akiipatia Yanga bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalty dakika ya 56 na Mgosi akaisawazishia Simba dakika ya 74.
Msimu huo Simba ilinyang’anywa ubingwa na Yanga kwa tofauti ya wastani wa mabao, kwani timu zote zilikuwa na pointi 49. Hata hivyo, Yanga ilifunga mabao 32 na kufungwa 7 hivyo kuwa na tofauti ya mabao 25, wakati Simba ilifunga mabao 40 na kufungwa 17, kwa hiyo ikawa na tofauti ya mabao 23!

Msimu wa 2011/12
Pengine ulikuwa msimu mbaya kwa Yanga, kwa sababu licha ya kupoteza ubingwa wake, lakini ilikubali kipigo cha mabao 5-0 katika mechi yao ya marudiano na Simba Mei 6, 2012 ambayo ilijawa na hujuma kubwa.
Katika mechi ya kwanza Oktoba 29, 2011 Yanga ilikuwa imeifunga Simba bao 1-0 kupitia kwa Mnyasa Davis Mwape dakika ya 75.
Msimu huo Simba ndio waliotwaa ubingwa kwa kufikisha pointi 62, Azam wakashika nafasi ya pili kwa pointi 56 na Yanga wakashika nafasi ya tatu kwa pointi 49.

Msimu wa 2012/13
Oktoba 3, 2012 Yanga ilinusurika kufungwa baada ya kusawazisha dakika ya 64 kupitia kwa Said Bahanuzi. Simba walipata bao la kuongoza dakika ya tatu kupitia kwa Amri Kiemba.
Ziliporudiana Mei 18, 2013 Yanga ikaibuka na ushindi wa 2-0 na msimu huo ikatwaa ubingwa kwa kufikisha pointi 60 wakati Simba ilishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 45. Azam walishika nafasi ya pili kwa mara nyingine tena wakiwa na pointi 54.

Msimu wa 2013/14
Huu ulikuwa msimu was are baina ya timu hizo. Kwanza zilifungana 3-3 Oktoba 20, 2013, na ziliporudiana Aprili 19, 2014 zikafungana 1-1. Safari hii Azam ndio waliokuwa mabingwa kwa kufikisha pointi 62 wakati Yanga ilishika nafasi ya pili kwa pointi 56. Simba ilikuwa ya nne kwa kukusanya pointi 38 wakati Mbeya City ilishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 49 katika msimu wake wa kwanza.

Msimu wa 2014/15
Oktoba 18, 2014 timu hizo zilitoka suluhu, lakini ziliporudiana Machi 8, 2015 Yanga ikafungwa bao la kizembe mno na Emanuel Okwi ambalo linaendelea kubaki katika kumbukumbu hadi leo. Yanga ilitwaa ubingwa na Azama ikashika nafsi ya pili huku Simba ikishika nafasi ya tatu.

Msimu wa 2015/16
Kwanza Septemba 26, 2015 Yanga iliitandika Simba 2-0, halafu ziliporudiana Februari 20, 2016 ikatoka kipigo kama hicho na ikatwaa ubingwa ikifuatiwa na Azam huku kwa mara nyingine Simba ikishika nafasi ya tatu.
Msimu wa 2016/17 ndio umeanza, tusubiri tuone itakavyokuwa katika mechi ya Jumamosi.
Mechi nyingine za Ligi Kuu zitakazochezwa Jumamosi na Jumapili ni kama ifuatavyo:
Oktoba 1, 2016:  Yanga vs Simba  
Oktoba 2, 2016:  Azam vs Ruvu Shooting       
Oktoba 2, 2016: Kagera Sugar vs Prisons        
Oktoba 2, 2016: Majimaji vs Stand United      
Oktoba 2, 2016: Mbao vs JKT Ruvu Stars      
Oktoba 2, 2016: Mbeya City vs Mwadui 
Oktoba 2, 2016: Mtibwa Sugar vs African Lyon       
Oktoba 2, 2016: Toto Africans vs Ndanda       

Msimamo wa Ligi Kuu
1. Simba               6       5        1        0       12:2  16     
2. Stand U.           6       3       3       0       6:3    12     
3. Yanga               5        3       1        1        8:1     10     
4. Azam                6       3       1        2       8:5    10     
5. Mtibwa            6       3       1        2       7:6    10     
6. Kagera             6       2       3       1        4:3    9      
7. Prisons             6       2       3       1        3:2    9      
8. Mbeya City      6       2       2       2       7:6    8      
9. Mbao               7        2       2       3       9:10  8      
10. Ruvu Shoot.  6       2       2       2       5:7    8      
11. Ndanda           7        2       2       3       6:9    8      
12. African Lyon 6       1        3       2       4:7    6      
13. Ruvu Stars     5        1        2       2       3:3    5       
14. Toto Africans 6       1        2       3       1:3     5       
15. Mwadui           6       1        2       3       3:6    5       
16. Majimaji        6       0       0       6       2:15   0       

Makala haya yameandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com, simu 0656-331974. Kama utayatumia kwa namna yoyote ile ni lazima utoe credit kwa mwandishi Daniel Mbega au MaendeleoVijijini Blog.

Comments