Featured Post

SERENGETI BOYS HAKUNA ‘KIJEBA’ KAMA NURDIN BAKARI, CONGO ISITUZUIE KAMA 2013!



Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
KIKOSI cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, Jumapili Oktoba 2, 2016 kitajitupa uwanjani mjini Brazzaville kupambana na wenyeji Congo katika kutafuta nafasi ya kucheza fainali za 17 za vijana Afrika.
Timu hiyo inaingia uwanjani ikiwa na ushindi wake wa mabao 3-2 ilioupata jijini Dar es Salaam Septemba 18, 2018 ambao kama itaulinda, utakuwa mtaji mzuri wa kushiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo ya vijana ambayo itafanyika Aprili 2017 nchini Madagascar.

Hata hivyo, MaendeleoVijijini inatambua kwamba, Serengeti Boys inakabiliwa na kumbukumbu mbili kubwa katika mashindano hayo.
Kwanza, itakumbukwa kwamba, timu hiyo ilifuzu kwa fainali za mwaka 2005 kule Gambia, lakini ikashindwa kushiriki baada ya kutolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutokana na kumchezesha ‘kijeba’ beki Nurdin Bakari aliyekuwa akiitumikia klabu ya Simba wakati huo.
Katika raundi ya awali iliitoa Rwanda kwa jumla ya mabao 2-1 – kwanza ikitoka sare ya 1-1 mjini Kigali kabla ya kushinda 1-0 jijini Dar es Salaam.
Kwenye raundi ya kwanza iliifungashia virago Zambia kwa kushinda jumla ya mabao 4-1. Ilishinda 2-1 ugenini halafu ikashinda 2-0 nyumbani.
Katika raundi ya pili ikaitoa Zimbabwe kwa jumla ya mabao 4-1 pia – ilishinda 3-1 nyumbani na kisha 1-0 ugenini, mechi ambazo Nurdin Bakari hakucheza kutokana na kutumia kadi mbili za njano.
Wakati ikiwa tayari imefuzu na kutarajiwa kupangwa katika Kundi B pamoja na Nigeria, Afrika Kusini na Ivory Coast, huku maandalizi yakiendelea, hatimaye Januari 28, 2005 CAF ikaiondoa Tanzania kwenye fainali hizo kwa kumchezesha Nurdin Bakari dhidi ya Rwanda na Zambia kutokana na kudanganya umri.
TFF ilieleza kwenye taarifa za wachezaji kwamba Nurdin alizaliwa mwaka 1988, lakini katika orodha iliyotumwa CAF na klabu yake ya Simba kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa, ilionyesha kwamba mchezaji huyo alizaliwa mwaka 1983!
Kwa maana hiyo ukijeba wa Nurdin ukaikosesha Tanzania kushiriki fainali na nafasi yake ikachukuliwa na Zimbabwe ambayo hata hivyo iligeuka kuwa daraja la timu nyingine.
Jambo la pili ni kwamba, Serengeti Boys inakumbuka pia ilivyozikosa fainali za mwaka 2013 kule Morocco baada ya Congo-Brazzaville hao hao kuwafungashia virago katika raundi ya pili.
Baada ya kusonga mbele kwa chee kufuatia Misri kujitoa katika raundi ya kwanza, Tanzania ilikumbana na Congo-Brazzaville kwenye raundi ya pili na mechi yao ya kwanza Novemba 16, 2012 ilishuhudia Serengeti ikishinda 1-0, lakini ziliporudiana mjini Brazzaville Desemba 2, 2012 Serengeti wakakubali kipigo cha 2-0.
MaendeleoVijijini inajua kwamba, haya ni majinamizi ambayo Serengeti inapaswa kukabiliana nayo kwa dhati kuhakikisha inashinda na kufuzu kwa fainali hizo.
Serengeti inahitaji ushindi ama sare ya aina yoyote ili iweze kufuzu kwa mara ya kwanza fainali hizo ambazo kwa ujumla ndizo zimepata kuibua vipaji vya wachezaji wengi nyota wa Afrika waliotamba na wanaoendelea kutamba katika ligi mbalimbali duniani.
Ushindi au sare utasaidia kulinda matokeo yake ya kwanza ya ushindi wa 3-2, wakati Congo wao wanahitaji ushindi hata wa bao 1-0 tu kutokana na kuwa na faida ya bao la ugenini.
Ili kufuzu, Serengeti wanatakiwa kutafuta mabao ya mapema, kuimarisha kiungo pamoja na ngome ili kuvuruga mashambulizi ya wenyeji wao na kutoruhusu kupenya.
Jukumu hilo linaweza kuwa limefanyiwa kazi vizuri na makocha wa timu hiyo ambao wameiongoza vyema katika hatua za awali ambapo kwanza iliitoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0; kwanza ikiifunga 6-0 ugenini na kushinda 3-0 nyumbani, halafu ikaitoa Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-1; ikitoka sare 1-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani.
Timu nyingine ambazo zinawania nafasi saba ili kuungana na wenyeji Madagascar kwenye fainali hizo ni Ghana, Ivory Coast, Niger, Gabon, Mali, Ethiopia, Senegal, Guinea, Sudan, Cameroon, Angola na Comoro.
Katika mechi zilizopita, Ghana iliifunga Ivory Coast 3-1; Niger ikaifunga Gabon 1-0; Mali ikashinda 2-0 dhidi ya Ethiopia; Senegal ikafungwa nyumbani 1-0 na Guinea; Sudan ikailima Cameroon 4-2; na Angola ikaichabanga Comoro 5-0.
Congo ni wazoefu wa mashindano hayo, walikuwa mabingwa wa kwanza mwaka 1985 na wamerudia nusu fainali mara mbili – mwaka 1991 na 2011 – na wameshiriki ubingwa wa dunia wa vijana mara tatu.

Makala haya yameandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com, simu 0656-331974. Kama utayatumia kwa namna yoyote ile ni lazima utoe credit kwa mwandishi Daniel Mbega au MaendeleoVijijini Blog.

Comments