Featured Post

SENSEI MTSHALI (7TH DAN) ATUA KATIKA SEMINA YA KARATE, MITIHANI KUFANYIKA KESHO JUMAMOSI

Sensei Mtshali akirekebisha mkanda wa Sensei Florence Kieti kutoka Mombasa, Kenya.

Sensei Mtshali (kulia) akitoa maelekezo.

Wakati semina ya kimataifa ya Shotokan Karate imeingia katika siku ya tano leo hii hapa kwenye ukumbi wa Don Bosco, Upanga jijini Dar es Salaam, tunashuhudia ujio wa mwalimu mkongwe kabisa wa mchezo huo barani Afrika, Edward Mtshali Sensei (7th Dan) kutoka nchini Afrika Kusini.


Sensei Mtshali (68) amewasili nchini juzi usiku na kuanzia jana amekuwa darasani akiwaonyesha makarateka wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini uzoefu wake katika semina hii ambayo inawahusisha makarateka kutoka Kenya, Uganda, Zambia, Zimbabwe, Tanzania Bara na Zanzibar.

Sensei Mtshali ndiye ameshika darasa kwa leo ambapo zaidi ya makarate-ka 50 wanahudhuria.
Mbali ya Mtshali, lakini pia Mkufunzi Mkuu wa JKA/WF-Kenya, David Mulwa Sensei naye ametua nchini kuhudhuria semina hiyo.
Hii siyo mara ya kwanza kwa walimu hao wawili kuja nchini, kwani wamekuwa chachu kubwa ya maendeleo ya karate kutokana na msaada wao mkubwa kwa vijana wa Tanzania.

Wasifu wake
Edward Mtshali Sensei, au Ed kama anavyoitwa kila mahali, ndiye Mbantu wa kwanza kupewa hadhi ya kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini wa Japanese Karate Association (JKA) World Federation (WF). Pia ni Mbantu wa kwanza kupewa hadhi ya rangi za taifa la Afrika Kusini mara tano mfululizo. Mara ya kwanza ilikuwa alipocheza dhidi ya timu ya Uingereza mwaka 1977. Timu ya taifa ya Afrika Kusini ilikuwa ikichaguliwa kutoka katika timu nne tofauti, Timu ya Wahindi, Machotara, Wabantu na Makaburu (maarufu Springbok) na Sensei Ed alikuwa karate-ka pekee Mbantu kuchaguliwa.
Mwaka 1978, alikuwa mmoja wa wachezaji wa timu rasmi ya Springbok ambayo ilishindana na timu za Ujerumani na Marekani, ambapo timu ya Marekani ilikuwa na mchezaji, ambaye kwa sasa ni maarufu katika filamu, Billy Blanks.
Ilikuwa ni katika kipindi hiki ambapo alianza kucheza akiwa chini ya Sensei Stan, muasisi na Mkufunzi Mkuu wa South Africa JKA, akiwa pamoja na wanandugu wakungwe wa Geyer.
Mwaka uliofuata alikuwemo kwenye timu ya taifa ya Afrika Kusini ambayo ilikwenda Marekani. Katika mashindano hayo, alitwaa tuzo maalum kama mshiriki wa muda mrefu.
Mwaka 2006, katika mashindano ya ShotoCup nchini Australia, Sensei Ed alikuwa Mbantu wa kwanza kutwaa Dan ya 7 akisimamiwa na timu ya majaji Wajapani wote kutoka makao makuu ya Japanese Karate Association (JKA) World Federation (WF). Mpaka sasa yeye ni Mbantu pekee barani Afrika kuwa na rank hiyo ndani ya JKA. Kwa sasa Sensei Ed ndiye anayesimamia JKA/WF katika nchi 26 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alizaliwa Aprili 26, 1948 na mwaka huu ametimiza miaka 68, lakini ukimtazama unaweza kudhani ana miaka 45 kwa jinsi alivyo mkakamavu. Amekuwa akicheza karate kwa miaka 50 sasa na amekumbana na changamoto nyingi.
Mwaka 1968, mkufunzi wake wa kwanza alikuwa Samuel Maimane, ambaye alikuwa na mkanda wa bluu ambapo walikuwa wakicheza Shotokan karate. Sababu ya kusema kwamba alifahamu hiyo ni Shotokan ni kwa vile kitabu walichokuwa wanakitumia kilikuwa kile kilichoandikwa na Sensei Nishiyama. Ilikuwa ni vigumu wakati huo kwa Wabantu kupata ujuzi na kupata waalimu wa kuwapandisha madaraja.
Huyo ndiye Sensei Mtshali, japo kwa ufupi tu.


Imeandaliwa na mtandao wa www.maendeleovijijini.blogspot.com

Comments