Featured Post

PROF. MBARAWA AAGIZA UJENZI WA BARABARA YA JUU KUKAMILIKA KWA WAKATI

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Eng. Patrick Mfugale(Wa kwanza kulia) akitoa maelezo ya ramani ya Ujenzi wa barabara za maingiliono (Tazara Flyover) kwa  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa( Wa kwanza kushoto) wakati alipokagua ujenzi  huo Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Wa pili kushoto) akitoa maelekezo kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Eng. Patrick Mfugale (Kulia kwake) wakati alipokagua ujenzi wa barabara za maingiliono (Tazara Flyover, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Katikati), akifafanua jambo mara baada ya kukagua daraja la wapiti kwa miguu lilopo Buguruni Jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Eng. Patrick Mfugale na Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa barabara wa Wizara Eng. Light Chobya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akisalimiana na Wananchi  mara baada ya kumaliza kukagua daraja la wapiti kwa miguu lililopo Buguruni Jijijni Dar es salaam.
Picha na Benjamin Sawe -Maelezo
  
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa  ameitaka Kampuni ya kikandarasi ya Sumitomo Mitsui inayojenga mradi wa ujenzi wa barabara ya juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara kumaliza ujenzi huo kwa wakati mradi huo ili kusaidia kupunguza tatizo la msongamano.
Akizungumza mara baada kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo jijini Dar es salaam, Profesa Mbarawa amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutajenga historia  nchini kutokana na kuwa ni wa mwanzo kujengwa.
“Nimefurahi kuona mradi huu upo katika hatua nzuri, naomba mkamilishe mradi huu unakamilika kwa ubora na kwa wakati ili tatizo la msongamano lililopo katika maeneo haya kupungua au kuisha kabisa”, amesema Waziri Mbarawa.
Profesa Mbarawa amemtaka Mkandarasi kuhakikisha kuwa anafanya kazi kwa  umakini na kwa uangalifu wakati wa kipindi chote cha ujenzi ili kuitokuweza kusababisha foleni katika eneo hilo.
Aidha, Waziri Mbarawa amewataka wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi huyo ili kurahisisha kazi za ujenzi huo kukamilika kwa wakati na kupata matokeo chanya.
“Nawaomba watanzania wenzangu kuwa wavumilivu na usumbufu wowote utakaojitokeza katika kipindi hiki chote, kwani ukamilifu wa mradi huu utasaidia kupunguza tatizo la msongamano katika barabara hizi”, amefafanua Waziri Mbarawa.
Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa amekagua daraja la watembea kwa miguu eneo la Buguruni Sheli na kuwataka wananchi wa maeneo hayo kulitunza daraja hilo ambalo uwepo wake umesaidia kupunguza ajali katika maeneo hayo.
“Ni matumaini yangu sasa wakazi wa maeneo  haya mtavuka kwa amani kupitia daraja hili, na ajali zilizokuwa zikitokea maramara hazitakuwepo tena”’, amesema Profesa Mbarawa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Eng. Patrick Mfugale amemuahidi Waziri huyo kumaliza kwa wakati ujenzi huo na kumhaakikishia Waziri kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakuwa na viwango vilivyo bora.
Mradi wa Tazara Flyover ni msaada kutoka Serikali ya Japan ambao umegharimu shilingi bilioni 93.4 na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka 2018.
Imetolewa na Kitengo cha Mawsiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.


Comments