- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
TAKRIBAN Shs. 1.7 bilioni na Zaidi ya mifuko 2,800 ya saruji
vimechangwa leo hii Ikulu jijini Dar es Salaam na wafanyabiashara pamoja na
mabalozi wanaowakilisha mataifa mbalimbali nchini ili kusaidia wahanga wa
tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Kanda ya Ziwa (Mwanza na Kagera) na
kusababisha vifo vya watu 17 na majeruhi 166 mwishoni mwa wiki.
Katika tukio hilo lililosimamiwa na Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, jumla ya Shs. 646 milioni, Dola 10,000 na Euro 10,000 taslim
zimepatikana wakati ahadi ni Shs. 705 milioni.
Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, akizungumza
kwa niaba ya wafanyabiashara na wadau wa sekta binafsi, ameihakikishia serikali
kwamba wako bega kwa bega katika janga hilo na kwamba misaada ya kwanza itatoka
kwao wafanyabiashara.
Katika orodha ya waliochangia leo hii ikiwa ni pamoja na kutoa
ahadi, watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje wamechangia Shs. 10 milioni wakati
jumuiya ya raia wa China waishio nchini imechangia jumla ya Shs. 200 milioni.
Kampuni ya Mohamed Enterprises imechangia Shs. 100 milioni, TBL
imechangia Shs. 100 milioni, Azania Group wametanguliza Shs. 20 milioni,
wafanyabiashara wa mafuta ya rejareja wameahidi kukusanya Shs. 250 milioni
ambazo zitakabidhiwa Ijumaa hii, wakati kiwanda cha sukari cha Kagera Sugar
kimetoa Shs. 100 milioni pamoja na tani 10 za sukari.
Wahisani wengine waliochangia na viwango vyao kwenye mabano ni
Pepsi Cola (Shs. 50 millioni), Reginald Mengi (Shs. 110 milioni), Protas
Ishengoma (Shs. 5 milioni), Puma (Shs. 50 milioni), Augusta Tanzania (Shs. 10
milioni), Tipper (Shs. 20 milioni), Oryx (Shs. 50 milioni), Sahara Tanzania
(Shs. 20 milioni) na Waislamu wa madhehebu ya Al-Shafy, Ijumaa na Adhuhuri wamechangia
shilingi milioni 1.
Aidha, Kampuni ya Serengeti Breweries Limited imetoa mifuko
800 ya saruji, Camel Oil ambao pia wanatengeneza saruji ya Camel Cement wametoa
mifuko 1,000 ya saruji na kampuni za GBP, MOIL na OILCOM wameahidi kujenga
shule mbili (Ihungo na Nyakato) zilizoharibiwa vibaya.
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa amesema kwamba, licha ya
harambee hiyo, lakini wangependa kujua kila tathmini inayofanyika katika eneo
la Bukoba na akasikitika kuwa wana mawakala wa UN wachache nchini Tanzania.
Hata hivyo, ameahidi kwamba Jumamosi watawasilisha msaada wao
wa hali na mali.
Ubalozi wa Kuwait nchini wametoa fedha taslimu katika viwango
vya Dola, Euro na Shilingi za Kitanzania ambazo hazikuweza kufahamika idadi
yake mara moja.
Balozi wa Kenya amesema licha ya michango ambayo tayari
wamekwishaitoa, lakini wataongeza mablanketi, vifaa vya ujenzi na afya kwani
wananchi hao wanahitaji malazi na huduma nyingine za kiutu.
Balozi nyingine pamoja na wafanyabiashara wa sekta ya mafuta wamemahidi
kutoa misaada yao wakati wowote.
Katika hatua nyingine, Wizara ya Mambo ya Nje wameahidi kufanya
matembezi ya hisani ili kuhamashisha uchangishaji wa fedha na wataanzia Polisi
Oysterbay.
Comments
Post a Comment