Featured Post

EMORO HALISI NI HUYU HAPA TUMBA AYILA, MCHEZA SHOO WA PEPE KALLE ALIYETAMBA KWENYE FILAMU YA ‘MAISHA MATAMU!’



 Tumba Ayila 'Emoro'
Emoro akifanya vitu vyake stejini
  
Pepe Kalle na Emoro katika poicha ya jalada la albamu.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
NENO au jina la ‘Emoro’ limekuwa maarufu sana Tanzania, pengine na ukanda wote wa Afrika Mashariki. Ukisikia neno hilo linatajwa, basi ujue kwamba watu wanazungumzia mtu au kitu kifupi sana – mbilikimo!

Lakini walio wengi wanatolea mfano wa Emoro bila hata kujua asili yake – wengi, wa kizazi cha sasa na kilichotangulia kidogo.
Ni sahihi wanapofananisha mtu au kitu kifupi na ‘Emoro’, lakini ukweli ni kwamba, Emoro mwenyewe ni mtu maarufu ambaye enzi zake alitamba sana katika tasnia ya muziki na filamu, ingawa alicheza filamu moja tu!
Wale vijana wenzangu wa zamani wanamkumbuka. Alikuwa mcheza shoo wa bendi maarufu ya Empire Bakuba iliyokuwa ikiongozwa na jitu la kimakwelini, jitu la miraba sita – Kabasele Yampanya au Pepe Kalle.
Wanakumbuka vituko vyake alipokuwa stejini jinsi alivyokuwa na uwezo wa kukata nyonga na kubiduka sarakasi kadiri apendavyo, huku akicheza kichwa chini miguu juu.
Naam. Jina lake halisi ni Tumba Ayila, na Emoro ni jina la utani alilopewa enzi zake.
Mimi nilianza kumuona kupitia kwenye video mwaka 1988, siyo akicheza muziki jukwaani, bali katika filamu moja matata ya La vie est belle, au ‘Maisha Matamu’ na Waingereza wakatafsiri – ‘Life is beautiful’ au ‘Life is rosy’.
Mhusika mkuu wa filamu hiyo alikuwa Jules Shungu Wembadia Pene Kikumba, ambaye wengi walimfahamu kama Papa Wemba. Lakini humo ndani kuna watu wengine maarufu, akiwemo Pepe Kalle ambaye alicheza kama rafiki mwanamuziki wa Papa Wemba aliyecheza kama Kourou, kijana kutoka kijijini aliyekwenda mjini Kinshasa kutafuta maisha ya muziki.
Ukiitazama unaweza kusema ni kama zile filamu mfulilizo za The gods must be crazy kwa jinsi ilivyo na vituko humo ndani.
Tumba Ayila, au Emoro, ndiye anayetamka mara nyingi maneno ya La vie est belle ndani ya filamu hiyo, ambamo Papa Wemba, akicheza kama Kourou, alijua kwamba akienda mjini atakuta maisha rahisi tu, lakini badala yake ikabidi apitie changamoto nyingi hadi kufanikiwa.
Emoro huyu, akicheza pamoja na rapa mashuhuri wa Empire Bakuba, Bileku Jean-Pierre Matonet ambaye alifahamika zaidi kama Bileku Mpasi au Djouna Mumbafu, ndio waliofanikiwa kubadilisha shoo za bendi hiyo ambazo ziligeuka kuwa kama maonyesho ya sarakasi.
Ukitazama video za albamu za Livre d'or, Dans Masassi calculé à Abidjan, Adieu Dr. Nico, Obosini Kisomele, Allah, Bakuba Show, Sombokila, Blanche neige, Nzoto ya chance / 8000 km, maarufu kama Kwassa Kwassa, Joe Dikando, Pon Moun Paka Bougé, Moyibi, Ya Moseka de l'Empire Bakuba, Show times, Cé Chalé Carnaval, Feux d'artifice na nyinginezo utaona utukutu wa Emoro ambaye aliwaacha mashabiki wengi midomo wazi.
Empire Bakuba wakati huo ilikuwa na wanamuziki mahiri kama Jojo Ikomo, Dilu Walumona na Matolu Dode ambaye wengi walimfahamu kama Papy Tex. Hawa pamoja na Pepe Kalle ndio walioanzisha Empire Bakuba mwaka 1972. Lakini pia walikuwepo wapiga solo mahiri kama Kinanga Nanzao maarufu kama ‘Boeing 737’ na Ebuya Lange au ‘Doris’.
Wakati Empire Bakuba ilipokuja nchini Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka mwaka 1990, nakumbuka nilikuwa shule pale Pugu sekondari. Siku na fedha ya kiingilio kwenye onyesho lake la Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) zaidi ya nauli yangu shilingi 10 na shilingi 5 ya barafu. Usishangae, wakati huo nauli ya mwanafunzi ilikuwa shilingi 5 tu, hivyo nilikuwa na nauli ya kwenda na kurudi.
Nilikwenda mapema kama saa tatu nilikuwa nimefika pale. Ingawa wakati huo bendi hiyo ilikuwa ikitamba na albamu yake ya Pon Moun Paka Bougé, lakini kama ilivyokuwa kwa mashabiki kwa maelfu waliofurika uwanjani siku hiyo – ninaamini – lengo langu lilikuwa kuangalia vitu viwili tu – kumuona Pepe Kalle mwenye urefu wa meta 2.1 na uzani wa takriban kilogramu 150 na dansa mbilikimo – Tumba Ayila ‘Emoro’!
Niliingia uwanjani, lakini usiniulize niliingiaje, maana watoto wa kutoka shamba nao wana mbinu nyingi kama hao watoto wa mjini tu.
Nakumbuka wakati wa ziara hiyo ambayo iliratibiwa na kampuni ya African Music Promoters ya homeboy Anania Sangula ambaye ndiye aliyewaleta wanamuziki wengi wa Zaire kama Tshala Muana na wengine, ilibidi Emoro atafutiwe mbilikimo mwenzake wa hapa nchini, nakumbuka jina lake aliitwa Khadija kutoka Dodoma, ambaye naye alikuwa na uwezo wa kucheza vilivyo jukwaani.
Pepe Kalle aligundua umuhimu wa kumtafuta patna wa Emoro, na ndipo alipompata Jolie Bébé.
Hata hivyo, miaka miwili baada ya ziara hiyo, yaani mwaka 1992, Emoro akafariki ghafla wakati bendi ikiwa ziarani Ulaya. Pepe Kalle alilia mno kwa kifo cha kipenzi chake Emoro na akamtungia albamu maalumu iitwayo Hommage à Emoro.
Baada ya hapo, Jolie Bébé akaongezewa madansa wengine wawili mbilikimo, mtukutu Dokolos na mbonge nyanya Dominique Mabwa, ambaye uchezaji wake ulikuwa ukiwaacha wengi hoi.
Mbilikimo wa Congo
Emoro alitokea katika jamii ya Mbilikimo wa Congo (Congo Pygmies) katika kabila la Bayaka, magharibi mwa Congo DRC.
Mbilikimo hao wa Congo (ambao pia wanajulikana kama Bambenga au Bayaka) wanaishi katika jamii mbalimbali katika nchi za Rwanda, Burundi, Congo DRC, Afrika ya Kati, Cameroon, Guinea ya Ikweta, Gabon, Jamhuri ya Congo, Angola, Botswana, Namibia na Zambia.
Jamii nyingi za Mbilikimo ni wawindaji na walaji matunda wanaotegemea mazao ya misitu yao. Hata hivyo, wao siyo wakulima, lakini hununua chakula kutoka kwa wakulima, kwani wanategemea pia mazao ya chakula ndiyo maana hawawezi kuishi ndani ya misitu ambako hakuna shughuli za kilimo.
Takwimu zinaonyesha kwamba, idadi ya mbilikimo hao ni kati ya 250,000 na 600,000 ambao wanaishi katika misitu ya Congo, ingawa jamii ya Mbilikimo wa Twamay wanaishi kwenye uwanda wazi na kwenye jangwa.
Mbilikimo wako katika jamii mbalimbali, lakini zinazojulikana zaidi ni Wambenga (Waka au Wabaka) walioko kusini mwa Bonde la Congo, ambao wanaongea Kibantu na Kiubangi; Wambuti (waefe) wanaoishi kwenye Misitu Minene ya Ituri ambao wanaongea Kibantu na lugha nyingine za Sudan ya Kati, Watwa wanaopatikana katika Maziwa Makuu hasa Burundi na Rwanda ambao wanaongea Kirundi na Kiga.
Naam. Huyo ndiye Emoro halisi na kwa ufupi tu nimeeleza historia ya Mbilikimo wa Congo. 
Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani Tumba Ayila Emoro. AMEN.

Comments

  1. Aisee umenikumbusha mbali sana. Wakati nasoma hii makala akili yangu ilihama kabisa nyuma miaka hiyo. Aisee hadi nasisimka aisee.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Tunahitaji kuweka kumbukumbu, mambo mengi yanasahaulika kutokana na sayansi na teknolojia

      Delete
  2. Mshana, mambo mengi ya zamani yanasahaulika haraka, hatuweki kumbukumbu na kadiri ulimwengu wa sayansi na teknolojia unavyozidi kusonga tutayasahau mengi.

    ReplyDelete

Post a Comment