Featured Post

BARAKA KITENGE 'ASKARI' WA YANGA ALIYEWAHANGAISHA WASHAMBULIAJI, NDIYE BABA WA MTANGAZAJI MAULID KITENGE



Baraka Kitenge 'Askari au Zagallo'

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
Kuzaliwa: 1942
Mahali: Tabora
Jina la utani: Askari au Zagallo
Nafasi uwanjani: Beki 2
Alianza kucheza soka: miaka 8
Timu: Young Boys (Tabora) 1961 - 1965; Yanga (Dar) 1966 - 1971; Timu ya Mkoa wa Tabora (Western Province) 1963 - 1965; Timu ya Mkoa wa Pwani (Mzizima United) 1966 - 1971.
Mafanikio: Robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika (Yanga) 1969 na 1970; Ubingwa wa Taifa (Yanga) 1968, 169, 1970, 1971.

WAPENZI wa kandanda walimwita 'Askari au Zagallo' wakimfananisha na beki nambari mbili wa Brazil enzi hizo, Mario Jose Lobo Zagallo, kwa uwezo wake wa kumchunga adui barabara uwanjani. Lakini jina lake halisi ni Kitenge Baraka Said, beki nambari mbili wa zamani wa Young Africans aliyeichezea timu hiyo kwa miaka mitano.

Mzaliwa wa Tabora, mwaka 1942, Kitenge Baraka alivua jezi mapema mwaka 1971 baada ya miaka 20 ya uchezaji. Alianza kulisukuma gozi akiwa na miaka nane na aliendelea na ari ya kuupenda mchezo huo wa kandanda alipoanza masomo ya msingi shule Town School hadi sekondari Kazima Sekondari zote za mjini Tabora.
Alishamiri zaidi kimpira wakati bado akiwa mwanafunzi wa sekondari huko Kazima. Kwa kipindi cha miaka minne ya sekondari (kuanzia 1961 hadi 1965), pamoja na kuchezea timu ya hapo shuleni, Kitenge Baraka alikuwa mpenzi na mchezaji wa Young Boys ya Tabora aliyoiwakilisha katika michezo ya ligi. Wakati huo alikuwa akichezea nafasi ya mshambuliaji nambari 9. Nafasi nyingine alizowahi kuchezea ni wingi ya kulia (nambari 7), sentahafu (mkoba - 5) na beki nambari mbili, nafasi aliyoichezea hadi alipostaafu.
Mwishoni mwa 1965 baada ya kumaliza kidato cha nne alikuja mjini Dar es Salaam na kuajiriwa na Shirika la Upakiaji na Upakuaji Mizigo Bandarini (East African Cargo Handling Services, sasa Tanzania Harbours Authority). Mara tu alipowasili Dar es Salaam viongozi wa klabu za soka mjini humo walianza kumshawishi ajiunge na timu zao, kwani hakuwa mgeni kwao. Walikwisha muona akishiriki mashindano ya Sunlight Cup (sasa Taifa Cup) akiwa na timu ya mkoa wa Tabora (Western Province). Lakini chaguo lake likawa Yanga, aliyojiunga nayo mwaka 1966.
Mwaka huo huo alichaguliwa kuunda timu mchanganyiko ya mkoa wa Dar es Salaam (Mzizima United) kugombea Kombe la Taifa. Pamoja naye walikuwemo wanasoka wengine mashuhuri wa nyakati hizo, akina Emmanuel Albert Mbele 'Dubwi', Abrahaman Lukongo, golikipa Kitwana Ramadhan Manara 'Popat' ambaye baadaye alikuja kubadilisha nafasi na kuwa mshambuliaji hatari wa Yanga na Taifa Stars,  Arthur Mambetta, Mustafa Choteka, na wengineo. Hakuwahi kuachwa katika orodha ya Dar-Kombaini (mara nyingine Pwani) mpaka alipoamua kutundika njumu ukutani. Anakumbuka mwanandinga huyo katika mahojiano yaliyofanyika mwaka 1984.
Mwaka 1967 alipata fursa ya kuliwakilisha taifa katika mashindano ya Kombe la Afrika Mashariki (Kombe la Chalenji) na Kombe la Nchi Huru za Afrika (sasa Kombe la Mataifa Afrika), Madagascar na hapa nyumbani na aliendelea kuichezea Taifa Stars kwa miaka mitatu.
"Nilivutiwa sana na mchezaji Ramadhan Abdallah 'Kitumbo' aliyekuwa mshambuliaji wa timu ya Mkoa wa Tabora na timu ya Taifa (Tanganyika), ambapo sifa zake zilinifanya niwe mwanasoka. Kweli nilifanikiwa," alisema Kitenge Baraka.
Mchezo mgumu kuliko yote ambayo Kitenge amewahi kucheza katika historia yake ni baina ya Yanga na Asante Kotoko ya Ghana mwaka 1969 kuwania Kombe la Klabu Bingwa barani Afrika. Katika mchezo huo wa robo fainali timu zilikwenda sare baada ya dakika 210 za mchezo ugenini na nyumbani (Kumasi na Dar es Salaam). Kwa kuwa sheria ya penati tano tano ilikuwa haijaanza kutumika, Asante Kotoko, mabingwa wa Afrika mwaka 1969 na 1970, walipata ushindi wa shilingi. Michezo yote ilikuwa migumu kwa kuwa timu zote zilicheza mtindo unaofanana.
Akizungumzia kuhusu wacheza wa enzi zake, aliwasifu sana Maulidi Dilunga 'Mtoto wa Mexico' na Gilbert Mahinya 'Mashine', ambao alisema kwamba aliwahusudu kutokana na bidii yao uwanjani na uwezo wa kupachika mabao. "Japokuwa Gilbert Mahinya alikuwa mchezaji wa kiungo, lakini aliweza kucheza mbele na nyuma bila kuchoka na kufunga mabao ya pembeni sana (impossible angles) tokea umbali wa mita 30 na zaidi," alisema.
Wachezaji wa miaka ya '80 waliokuwa wakimvutia walikuwa Athumani Juma 'Chama' mchezaji bora kwa mwaka 1983 na 1984 na Hamisi Ramadhani 'Kinye' golikipa wa Yanga na Taifa Stars.
"Kumekuwa na hali ya kuridhisha katika kabumbu hivi sasa kutokana na mbinu za kisasa wanazofundishwa wachezaji wetu na walimu mbalimbali. Isipokuwa wachezaji bado wanashindwa kuzingatia miiko inayotawala mchezo wa mpira hasa nyakati za mashindano makubwa. Fedha zimetawala mawazo ya wachezaji wengi, lakini pamoja na tamaa ya baadhi ya wachezaji hali ya soka imepanda," alipata kusema Kitenge.
Baraka Kitenge ambaye pia ni baba wa mtangazaji maarufu Maulidi Baraka Kitenge alifariki dunia Agosti 20, 2013 akiwa na umri wa miaka 74!

Comments