Featured Post

TUKICHELEWA SIASA, MAENDELEO TUTAYASIKIA KWENYE MITANDAO!



Utumiaji wa zana bora za kiasasa za kilimo kama hizi utakuwa ni ndoto ikiwa tutaendeleza siasa badala ya kuangalia shughuli za maendeleo na kutatua changamoto mbalimbali.

Na Daniel Mbega
NI miezi tisa sasa tangu serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani. Na iliingia katika kipindi ambacho Watanzania walikuwa wanaimba wimbo mmoja tu ‘MABADILIKO’.
Wananchi walikuwa wamechoshwa na umaskini, ukosefu wa huduma za msingi za kijamii kama afya, elimu, maji safi, miundombinu na kadhalika, ambazo zilikuwa ni kilio chao cha miaka mingi bila kupatiwa ufumbuzi.
Kikubwa kilichokuwa kinapigiwa kelele na wananchi ni kero ya rushwa na ufisadi, uzembe, ubadhirifu wa mali ya umma na mambo mengine ambayo kwa kiasi kikubwa yamekwamisha maendeleo kwa kipindi kirefu.

Kero zote hizo hazihitaji siasa ili zipatiwa ufumbuzi, bali zinahitaji utekelezaji wa vitendo bila kujali utekelezaji huo unafanywa na chama gani, kwani maendeleo yatakayopatikana hayabagui watu kwa itikadi zao za kisiasa, kidini, kikabila au rangi.
Na katika kipindi chote ambacho serikali ya awamu ya tano, chini ya utawala shupavu wa Dk. John Magufuli, imekuwa madarakani imeweza kuthibitisha kwa vitendo kwamba kero hizo zinatatulika kwa sababu tayari jitihada zimeonekana katika kuwashughulikia wala rushwa, mafisadi na wakwepa kodi wakubwa pamoja na watendaji wazembe.
Japo elimu haijafikia katika ubora wake, lakini tayari serikali imesafisha njia kwa kuondoa ada na michango kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne, hatua ambayo inawapa fursa watoto kusoma bila bughudha.
Tumemshuhudia Rais Magufuli akipambana kwa vitendo na mafisadi na anajitahidi hata kurejesha mali za umma ambazo ziliingia kiharamu katika mikono ya wachache.
Kimsingi, wananchi wana matumaini makubwa kwamba kuna dalili njema za maendeleo mbele ya safari hasa kama siasa zinawekwa pembeni na utekelezaji unafanywa kwa vitendo.
Suala la kukumbatia siasa kwa kisingizio cha demokrasia ndilo limeifanya Tanzania idumae kimaendeleo huku wengi wakitumia mwamvuli wa demokrasia kutowajibika na kufisidi mali ya umma. Wakiguswa wanakimbilia kupiga kelele kwamba ni kinyume na haki za binadamu na demokrasia inaminywa!
Hili Rais Magufuli analitambua na ndiyo maana ameamua kuliweka kando ili kushughulikia kwa vitendo kero za wananchi na kuwaletea maendeleo, kwa sababu akichelewa siasa ni Dhahiri changamoto hizo haziwezi kwisha.
Karibu nchi zote ambazo zimeendelea duniani kuanzia Marekani, China, Urusi na kwingineko walitanguliza maendeleo kabla ya demokrasia.
Nchi hizo zilianza kutatua kero za msingi katika jamii na ili nchi iweze kupiga hatua kimaendeleo hapana budi kuweka pembeni demokrasia inayotajwa yenye msingi wa kupiga porojo za kisiasa na kuchelewesha maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wa Afrika tulitanguliza demokrasia badala ya maendeleo.
Kwa sasa nchi yenye mafanikio makubwa na inayozidi kupiga hatua ndani ya ukanda wetu wa Afrika Mashariki ni Rwanda. Ukiambiwa miaka ya 1990 kulikuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe hutakubali kwa jinsi inavyokimbia kimaendeleo.
Tunaipigia mfano nchi ya Rwanda kwamba ni ndogo lakini imepiga hatua kimaendeleo lakini tunasahau kujifunza njia zilizotumika kuifikisha hapo.
Rwanda ilipata uhuru siku 23 baada ya Tanganyika. Imekuwa kwenye migogoro kwa miaka mingi, lakini leo hii imesimama imara kiuchumi kiasi cha kupigiwa mfano duniani, tofauti na Tanzania ambayo amani imetawala na watu wanaendelea kuimba maendeleo bila utekelezaji.
Kwanini? Kwa sababu baada ya maafa makubwa ya mauaji ya kimbari yalitokea mwaka 1994, Wanyarwanda – au tuseme serikali ya Rwanda – iliona siyo wakati wa kuendelea kupiga siasa wakati wananchi wakihitaji maendeleo.
Ndani ya Rwanda kuna baba mmoja tu kwa sasa akisema wakalime wanakwenda kulima, akisema rushwa stop! watu wanafunga pochi zao.
Tanzania tumezowea kubembelezana sana, tumekuwa na ruhusa ya kuzurura usiku na mchana kupiga domo tu, kwa miaka yote kumi ya awamu ya nne kila kukicha ni maandamano.
Hebu tulinganishe Libya ya mtu waliyemwita dikteta Muammar Gaddafi na hii ya sasa ambayo kila siku ni maandamano? Ipi yenye maendeleo?
Pamoja na Libya kuwa katika jangwa, Gaddafi alihakikisha wananchi wanapa maji safi ya kunywa kwa kuchimba visima, wananchi wengine maskini walikuwa wakilipwa na serikali kila mwisho wa mwezi, yaani serikali ilikuwa ikiwahudumia.
Alifanikiwa hivyo kwa sababu ya kuhakikisha kila mtu anafanya kazi kwa nafasi yake na mapato yaliyopatikana kwenye uchumi wake ndiyo akayatumia kuwaendeleza Walibya.
Kule Misri nako kuanzia Januari hadi Desemba watu wapo mitaani wakiandamana na kutafutana kwa mitutu ya bunduki wakati Hosni Mubarak waliyemwita dikteta akiwa hayupo madarakani.
Dola zote kubwa zilizokwishawahi kujengwa duniani zilijengwa na watawala kama Dk. Magufuli. Kama unabisha, tafuta dola yoyote ile ya zamani iliyokuwa kubwa halafu tafuta mfumo wa uongozi uliokuwepo.
Changamoto kubwa iliyopo ni umaskini, ambao serikali kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 imedhamiria kuutokomeza na kuifanya Tanzania kuwa yenye jamii ya kipato cha kati.
Lakini pia hiyo ni katika kutekeleza Malengo Endelevu ya Dunia yanayosisitiza kutokomeza kabisa umaskini duniani.
Tukijikwamua kwenye umaskini, basi ujinga na maradhi vitaondoka.
Namna pekee ya kujikwamua kwenye umaskini ni kuchapa kazi. Kila mtu lazima ajizatiti kwa kufanya kazi kwa bidi mahali alipo badala ya kuendelea kulalamika kwamba serikali haifanyi hiki na kile.
Hatuwezi kujiletea maendeleo kwa kutegemea serikali ije itufanyie kila kitu huku tukiwa tumeketi kwenye vijiwe vya kahawa. Tena hatuwezi kupata maendeleo ikiwa kila siku tutakuwa tunashinda majukwaani tukipiga siasa bila utekelezaji.
Wananchi watakapokuwa na uwezo wa kujipatia kipato watakuwa na uamuzi sahihi katika siasa na hivyo demokrasia itakuja bila shaka, lakini kwa sasa taifa linahitaji watu kuchapa kazi kwa bidii.
China ni nchi ya pili kwa uchumi duniani baada ya Marekani. Imepiga hatua kimaendeleo baada ya kuhimiza watu kufanya kazi na kuweka kando siasa na visingizio vya demokrasia.
Vyama vya siasa vinapaswa kuhimiza wananchi kufanya kazi kwa bidi, kwa kifupi vinapaswa kuhimiza maendeleo, siyo kushawishi migomo na maandamano yasiyo na tija.
Wananchi wakiwa na maendeleo na kujipatia kipato watakuwa na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi hata katika siasa, hawataweza kununuliwa kwa vijisenti nyakati za kampeni na uchaguzi na watachagua viongozi wenye uwezo wa kuwaletea maendeleo badala ya wale wanaowapa vibaba vya mchele.
Taifa likiwa na maendeleo hata vyama vya siasa vitakuwa imara, vitakuwa na hoja zenye nguvu na siyo rahisi taifa kuwa na sera mbovu kwa sababu tutahitaji sera zenye kuendeleza pale tulipofikia ili tusonge mbele.
Kwa maana hiyo, huu si wakati wa kupiga siasa kwa sababu tumeshuhudia kwa miaka mingi siasa na mwamvuli wa demokrasia vimedumaza maendeleo ya taifa.
Kama tutaendelea kupiga kelele katika siasa, kamwe tusitegemee kuona maendeleo, bali tutayasikia kwenye mitandao ya kijamii kila siku na kujisifu ujinga kwamba wenzetu wamepiga hatua.
Utaratibu wa maandamano unaotaka kufanywa na Chadema ni njama mojawapo ya kukwamisha juhudi za maendeleo ambazo zinafanywa na serikali, lakini wananchi wanapaswa kutafakari.
Kama kweli viongozi wakuu wa chama hicho wamedhamiria, basi watoke wao na familia zao wakaandamane badala ya kuwashawishi Watanzania maskini wasiojua hata mlo wao mmoja utakuwaje.
Tusidanganyike!
SOURCE: TAZAMA


Comments