Featured Post

SIMBA IMEANZA LIGI KUU NA MOTO WA DIZELI AU MABUA?




Mchezaji wa Simba Fredrick Magnon akiruka juu na golikipa wa Ndanda FC Jackson Chove huku wachezaji wa timu hiyo wakiangalia wakati mchezo huo wa Ligi Kuu ukiendelea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi, Agosti 20, 2016. Simba ilishinda 3-1.
 
SIMBA SC imeanza kwa kuongoza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wake mkubwa wa mabao 3-1 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi, Agosti 20, 2016.
Kasi ya mchezo huo ilikuwa nzuri kwa Simba, ambayo mashabiki wa timu hiyo wanahoji iwapo itaendelea hivyo hivyo na kurejea kwenye ufalme wake au itakuwa kama moto wa mabua unaozima punde.

Pengine kipimo cha kasi ya timu hiyo kitaonekana katika mechi zinazofuata ambapo Jumamosi ijayo, Agosti 27, itakuwa mgeni wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Hiyo itakuwa mechi ya kwanza ya maafande hao ambao wamesalimika kushuka daraja msimu uliopita.
Baada ya hapo Simba itakumbana na maafande wengine wa JKT Ruvu Shooting, ambao nao katika mechi ya kwanza jana Jumamosi walishinda bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar huko Turiani.
Azam FC, ambao kwa miaka ya karibuni wamebadili mwelekeo wa mashindano ya ligi hiyo, wao walinusurika kufungwa katika mechi ya kwanza baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya African Lyon kwenye uwanja wao wa Azam Complex.
‘Wajelajela’ Tanzania Prisons walianza vizuri ligi hiyo kwa ushindi wa bao 1-0 ugenini kwa Maji Maji huku wageni wa Ligi Kuu, Mbao FC ya Mwanza wakilazimisha kwenda suluhu na Stand United mjini Shinyanga.
Simba ina hasira ya kukosa mashindano ya kimataifa kwa miaka mitano sasa huku ubingwa wa Tanzania Bara ukibaki kwa Azam na Yanga ambazo zinapokezana kwa misimu minne.
Katika mchezo wake na Ndanda FC ambao ulichezeshwa na mwamuzi Emmanuel Mwandembwa wa Arusha, hadi zinakwenda kupumzika timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.
Simba SC ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji raia wa Burundi, Laaudit Mavugo katika dakika ya 20 ambaye alimalizia pasi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Hata hivyo, mshambuliaji chipukizi wa Ndanda FC, Omary Mponda aliisawazishia timu yake kwa kichwa katika dakika ya 37 akimalizia krosi ya nahodha Kiggi Makassy.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mcameroon wa Simba, Joseph Marius Omog kipindi cha pili akiwatoa Jamal Mnyate na Ibrahim Hajib na kuwaingiza Mwinyi Kazimoto na Frederick Blagnon yaliiongezea uhai Simba na kuvuna mabao zaidi.
Mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Blagnon aliifungia Simba bao la pili dakika ya 73 kwa kichwa akimalizia kona ya Tshabalala ambaye pia kona yake nyingine iliyopanguliwa na kipa wa Ndanda Jackson Chove ilizaa bao la tatu na la ushindi baada ya winga Shizza Ramadhani Kichuya kuusukumia wavuni mpira huo.
Katika mechi hiyo, Simba iliwakilishwa na: Vincent Angban, Hamad Juma, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shizza Kichuya/Mohamed Ibrahim dk84, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo, Ibrahim Hajib/Frederick Blagnon dk62 na Jamal Mnyate/Mwinyi Kazimoto dk69.
Ndanda FC: Jackson Chove, Azizi Sibo/Bakari Mtama dk65, Paul Ngalema, Kiggi Makasi, Hemed Khoja, Salvatory Ntebe, Forahim Isihaka, Bryson Raphael, Salum Telela, Omary Mponda na Shija Mkina/Nassor kapama dk65.
Kwa upande mwingine, nahodha wa Azam FC, John Raphael Bocco aliinusuru timu yake isifungwe na African Lyon baada ya kufunga bao la kusawazisha katika dakika ya 93. Bocco alifunga bao hilo lililokuwa likisubiriwa kwa hamu akimalizia pasi nzuri ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Lyon walitangulia kwa bao lililofungwa na Mganda Hood Abdul Mayanja dakika ya 46 baada ya kuchonga kona iliyoingia moja kwa moja wavuni.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa na: Aishi Manula, Ismail Gambo/Mudathir Yahya dk46, Bruce Kangwa, Himid Mao, David Mwantika, Jean Mugiraneza, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Francesco Zekumbariwa dk64, Shomary Kapombe, Frank Domayo/Kipre Balou dk63, John Bocco na Shaaban Idd.
African Lyon: Youthe Rostand, Baraka Jaffar, Khalfan Twenye, Hamad Waziri, William Otone, Omar Salum, Hamad Manzi, Mussa Nampaka, Omar Abdallah/Abdul Hilal dk86, Hood Mayanja na Tito Okello.

Comments