- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST), Dk. Gozbert Kamugisha, akimwelekeza jambo mgeni rasmi Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, kabla ya kuanza kutembelea maonyesho ya sayansi ya wanafunzi ambayo yamefanyika kwa mwaka wa tano.
Christina Godfrey Mongi (aliyetazama kamera), mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya sekondari Bwiru Girls ya jijini Mwanza, akiwaelekeza watu mbalimbali kuhusu utafiti wao juu ya kuweka mazingira bora na salama ya kujifunzi kwa wanafunzi wenye albinism.
Maonyesho yakiwa yanaendelea.
Mbali ya maonyesho, wanafunzi pia walipata fursa ya kutengeneza marafiki wapya kama wanavyoonekana hapa wakijadiliana mambo mbalimbali.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, akisikiliza maelekezo kutoka kwa wanafunzi wakati alipofunga na kutoa zawadi kwa washindi katika maonyesho ya tano ya sayansi.
Mkurugenzi Mtendaji wa YST, Dk. Gozbert Kamugisha (katikati) akimtambulisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kwa Mwambata wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, Moller Mathieu.
Walimu wa shule mbalimbali zilizoshiriki maonyesho ya tano ya sayansi kwa wanafunzi wakifurahia jambo nje ya ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana.
Wanafunzi wakiwa kwenye maonyesho hayo.
Na Daniel Mbega
WAZIRI wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amesema serikali
itaandaa mazingira ya kuwaendeleza watoto na vijana wanajihusisha na ubunifu
katika masomo ya sayansi na kushauri mashindano ya sayansi kwa wanafunzi
yafanyike kila wilaya, mkoa na taifa.
Akizungumza wakati
wa utoaji wa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye Mashindano ya Tano ya
Young Scientists Tanzania 2016 katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere
(JNICC) jijini Dar es Salaam jana, Profesa Ndalichako alisema hatma ya Tanzania
iko mikononi mwa wanasayansi na kwamba vijana hao chipukizi ndio msingi mkubwa
wa kuhimiza ushiriki wa wengi na kuibua vipaji vitakakvyolisaidia taifa.
“Huu ni
ulimwengu wa sayansi na teknolojia, ili Tanzania iendelee ni lazima tujikite
kwenye sayansi na kwa maana hiyo mimi kama waziri mwenye dhamana naahidi kwamba
tutawajengea mazingira mazuri zaidi watoto wetu kwa ajili ya kujifunzia pamoja
na kuendeleza vipaji vyao,” alisema.
Akaongeza: “Tunaomba
wadhamini waliofanikisha maonyesho haya waendelee kudhamini lakini wajitokeze
wengine ili kuhakikisha mashindano yanafanyika kuanzia ngazi ya wilaya, mikoa
na hatimaye taifa na hapo ndipo tutakuwa tumejenga msingi imara wa kuibua
wanasayansi wengi.”
Hata hivyo,
aliwapongeza wanafunzi wote walioshiriki maonyesho ya mwaka huu na kuwataka
waendelee na ubunifu huo kwa vile serikali imedhamiria kuwaendeleza.
“Dira ya
Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 inasisitiza, pamoja na mambo mengine, suala la
sayansi na ubunifu, na Tume yetu ya Sayansi na Teknolojia (Costech) itasimamia
kuhakikisha hawa watoto wanaendelezwa,” alisema.
Jumla ya
shule 150 kutoka mikoa yote ya Tanzania zimeshiriki mwaka huu na kushuhudia
wanafunzi 300 wakionyesha ubunifu wao, likiwa ni ongezeko la shule 30
kulinganisha na shule 120 zilizoshiriki mwaka 2015.
Awali,
Mkurugenzi Mtendaji wa YST, Dk. Gozbert Kamugisha, alisema kwamba maonyesho
hayo yanazidi kupanuka tofauti na yalipoanza miaka mitano iliyopita, na sasa
wanashukuru kuona shule nyingi zikishiriki zikiwemo za vijijini.
Alisema,
hata hivyo kwamba, lengo lao ni kuhakikisha wanafanya mashindano hayo kuanzia
ngazi ya wilaya hadi mkoa ili kuwapata washiriki wa kitaifa walio bora Zaidi.
“Hawa wote
ni bora, lakini kama tukifanya mashindano haya kuanzia wilayani tutajenga
misingi imara na kuwahasisha watoto wengi kuyapenda masomo ya sayansi na
kujikita kwenye ubunifu,” alisema Dk. Gozbert.
Naye
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya YST, Profesa Yunus Mgaya, alisema kwamba,
japokuwa si shule zote zenye maabara, lakini sayansi siyo lazima ifanywe ndani
ya maabara bali hata katika masuala mengine ya kijamii.
Alisema kwamba,
sayansi ni maisha ya kila siku na kwamba yako mambo mengi yanayoizunguka jamii
ambayo kama wanasayansi watajikita kuyatafutia ufumbuzi yanaweza kuleta
maendeleo.
“Siyo lazima
kuingia maabara kufanya sayansi, kuna mambo mengi katika jamii ambayo yanaweza
kufanywa na wanasayansi,” alisisitiza.
Kwa upande
wake, Mwambata wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania ambao ndio wadhamini wakuu
wa maonyesho ya YST, Mollar Mathieu, alisema kwamba kupitia shirika la misaada
la Irish Aid, wataendelea kudhamini maonyesho hayo ili kuhakikisha vipaji vingi
vinaibuliwa na watoto wa Tanzania wanajikita kwenye sayansi.
“Sisi kule
Ireland maonyesho haya yamefanyika kwa mwaka wa 51 na yanaendelea kushika kasi
huku tukipata wanasayansi wengi, naahidi kwamba tutaendelea kudhamini maonyesho
haya ili hatimaye Tanzania ipate wanasayansi wengi ambao watasaidia kuleta
mabadiliko,” alisema.
Katika maonyesho
ya mwaka 2015, aliyekuwa mgeni rasmi, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali
Hassan Mwinyi, aliwataka walimu katika shule za msingi na sekondari kutumia
lugha ya Kiswahili kufundisha sayansi, kwani lugha hiyo inaeleweka vizuri.
Alhaj Mwinyi
alisema Kiswahili ni lugha inayoeleweka vizuri, si kwa wanafunzi tu, bali hata
kwa watu wengine, hivyo ni vyema walimu wakaweka mkazo katika kuitumia kwenye
masomo ya sayansi.
“Nimepita
kwenye maonyesho haya, baadhi ya wanafunzi walikuwa wananiuliza ‘tukueleze kwa
Kiswahili au kwa Kiingereza’, nikasema tumieni lugha yoyote tu. Wengine
wamenieleza Kiingereza na wengine Kiswahili.
“Lakini
nataka niwaambie, walionieleza kwa Kiswahili, pamoja na utafiti wao kuwa katika
lugha ya Kiingereza, walifafanua vizuri sana na nikasema ‘aah, kumbe Kiswahili
kinaweza kutumika kufundisha vizuri sayansi,” alikaririwa akisema wakati huo.
Aliongeza
kusema kwamba, yeye wakati anaingia darasa la tano, mwalimu wake wa sayansi
alikuwa rais wa Scotland, lakini alimfundisha sayansi kwa Kiswahili na ndio
msingi wake mkubwa wa kulifahamu vyema somo la sayansi.
Maonyesho ya
mwaka yamechukua mpaka shule za vijijini, zikiwemo za Kata, na yametoa taswira
halisi ya kitaifa.
Orodha ya
shule zote zilizoshiriki maonyesho ya mwaka huu ni kama ifuatavyo:
Arusha (6): Trust St. Patrick, Edmund Rice, Ilboru, St. Jude,
Suye, na Notre Dame.
Dar es Salaam (11): Debrabant, Kinyerezi,
Manzese, Vingunguti, Loyola High, Mugabe, Jamhuri, Jangwani, Malamba Mawili,
Makurumla na Aga Khan Mzizima.
Dodoma (4): Miyuji, Viwandani, Mpunguzi na Makutupora.
Geita (3): Geita, Buseresere na Geita Islamic Seminary.
Iringa (4): Mseke, Idetero, Kwakilosa na Mkwawa.
Kagera (6): Nyaishozi, Ihungo, St. Joseph Kolping, Rugambwa,
Bulyakashaju na Kabanga.
Katavi (3): Mpanda Girls, Misunkulimo na Karema.
Kigoma (4): Masanga, Katubuka, Mwananchi na Gungu.
Kilimajaro (4): St. James’ Junior Seminary, Rau, St.
Amadeus na Same.
Lindi (8): Lindi, Mtama, Mkonge, Ng’apa, Ngongo, Mingoyo,
Angaza na Kilwa.
Manyara (4): Kwaraa, Chiefdodo, Endasak, na Bagara.
Mara (4): Mwisenge, Mara, Songe Girls, na Mwembeni.
Mbeya (6): Mbeya Sekondari, Iyunga Technical, Kalobe,
Loleza, Mwakibete na Nzondahaki.
Morogoro (7): Mzumbe, Kilakala, Sumaye, Morogoro, Asodu
Adrian Mkoba, Ifakara na Kibaoni.
Mtwara (10): Mtwara Technical, Mtwara Girls, Mtandi,
Mahuta, Aquinas, Mayanga, Ndikwa, Chidya, Ndanda na Umoja.
Mwanza (7): Bwiru Girls, Bwiru Boys Technical, Mirongo,
Butimba Day, Mkolani, Pamba na Mnarani.
Njombe (3): Mabatini, Luhololo na Mbeyela.
Pemba (4): Maendeleo, Utaani, Fidel Castro na Shamiani.
Pwani (7): Kibaha, Makurunge, Tumbi, Bagamoyo, Kibiti,
Premier Girls, na Minaki.
Rukwa (5): Matai, Kipande, Miangalua, Kizwite na Uchile.
Ruvuma (3): Songea Boys, Kigonsera High, na Mbinga Girls.
Shinyanga (7): Ngokolo, Chamaguha, Uhuru, Buluba,
Mwasele, St. Francis Of Assisi na Msekelo.
Simiyu (4): Nassa, Mwamanongu, Binza na Maswa Girls High.
Singida (4): Dk. Salmin Amour, Ilongero High, Kijota,
na Mandewa.
Tabora (4): Tabora Girls, Tabora Boys, Puge na Ipuli.
Tanga (7): Old Tanga, Macechu, St. Christina, Popatlal,
Mkwakwani, Mikanjuni na Tanga Technical.
Unguja (7): Lumbumba, Kiembe Samaki, SoS Hermann Gmeiner,
Haile Selassie, Mpendae, Ben Bella na Mwanakwerekwe A.
Comments
Post a Comment