Featured Post

ETI RAIS MAGUFULI ‘AMEWACHOKOZA’ CHADEMA!






Hata watoto hutangulizwa kwenye maandamano ya Chadema kama haya yaliyofanyika mwaka 2011 ambapo mtoto huyu ambaye hakujulikana jina lake mara moja naye alikuwemo.
Eliud Mwamakula
HAK’YANANI Rais John Pombe Joseph Magufuli ‘umewachokoza’ Chadema. Na tayari wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamekaa ‘mguu sawa’ kutekeleza amri ‘tukufu ya kamanda wao’ Freeman Mbowe, ya kufanya maandamano nchi nzima hapo Septemba Mosi, 2015 kupinga kile ambayo kiongozi huyo na chama chake wanakiita ‘Udikteta’ ndani ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Yote haya yanakuja baada ya wewe Mheshimiwa Rais kupiga ‘ban’ mikutano ya kisiasa na maandamano yasiyo na tija tangu mwezi Juni, hasa kutokana na kusudio la Chadema hao hao kutaka kuandamana kupinga walichokiita ‘ubabe’ wa Naibu Spika Dk. Tulia Ackson Mwansasu wakati wa vikao vya Bunge la Bajeti.
Pengine Rais Magufuli huwaelewi Chadema, ama ‘hujatikiswa’ na wanaharakati hao wa kisiasa tangu uapishwe Novemba 5, 2015.
Inawezekana pia hujui kuwa demokrasia ya kweli ndani ya Chadema ilikuwepo katika awamu mbili tu za uongozi wa chama hicho – hasa ya pili – wakati wa uongozi wa mzee wangu Wakili Bob Nyanga Makani kati ya mwaka 1998 hadi 2003 alipong’atuka kama alivyofanya muasisi mwenzake Edwin Mtei.
Kama Mheshimiwa Rais unadhani kwamba chama hiki ni cha kidemokrasia, basi umekosea, kwa sababu tangu kilipoingia chini ya uongozi wa mwenyekiti wa sasa ‘DJ’ Freeman Mbowe, demokrasia imetoswa na kinachoshuhudiwa ni harakati za kisiasa zilizojaa ubabe.
Ni kwa mantiki hiyo ndiyo maana nikasema Mheshimiwa Rais ‘umewachokoza’ Chadema, kwa sababu sasa ndipo wanataka kudhihirisha wazi harakati zao za kisiasa kwa kisingizio cha ‘kupambana na udikteta’ bila kuainisha ni udikteta wa aina gani.
Na ‘umewachokoza’ kwa sababu Chadema walikuwa wakitafuta ‘kiki’ ya kuingilia mitaani kuanzisha harakati zao bila mafanikio. Kila walipotaka kuchokonoa waligonga mwamba!
Mheshimiwa Rais, unajua hata siku ile unakabidhiwa cheti cha ushindi, jamaa waligoma, na wakaendelea kugoma hata wakati unaapishwa pale Uwanja wa Taifa.
Kuonyesha kwamba hawa jamaa wana visa kama vya ndugu wa mume, wakagomea hata hotuba yako ulipokwenda kuzindua Bunge la 11 kule Dodoma, ingawa ‘walikunja mpunga’ na kutia kibindoni. Wacongo wanasema ‘Mbongo mbongio’ – fedha fedheha bwana!
Hawa jamaa wamejitahidi kutafuta ‘single’ ya kutokea katika awamu ya tano bila mafanikio na yote hii ni kutokana na utendaji wako makini, hasa baada ya kuanza la suala la kubana matumizi kwa kupunguza safari za nje ya nchi, kufuta sherehe zinazotafuna mabilioni ya fedha za maskini, kupambana na mafisadi na majizi pamoja na kasi yako ya kukusanya kodi huku ukiwatumbua majipu wale wote ambao walikuwa kwenye fungate!
Usishangae Mheshimiwa Rais, kwa sababu hawa jamaa licha ya kupigia kelele kwamba katika serikali ya wamu ya nne ufisadi ulitamalaki na wakataka aje rais mwenye uchungu na taifa hili, kumbe maneno yao hayakuwa na porojo za vijiwe vya kahawa, kwa sababu wao ndio walikuwa wa kwanza kukupinga eti kwa nini unawatumbua majipu baadhi ya watu.
Kwa sababu haiwezekani kama umekwenda kufichua uozo mkubwa katika Bandari yetu na Mamlaka ya Mapato na kukusanya fedha nyingi zitufae sote, halafu wanatokea wale wale waliokuwa wanalia kwamba serikali ‘inawalea mafisadi’ ati wanakasirika na kuchukia.
Mimi nadhani kuna siri nyuma yake kutokana na kupinga huko ama huenda waliotumbuliwa ni maswahiba wao au nao walikuwa wainufaika kwa namna moja ama nyingine – yote mawili yanawezekana.
Walipoona mbinu zao zinagonga mwamba huku wananchi wakiendelea kufurahia uchapaji kazi wako, wakarudi kwenye staili yao ya zamani ‘kususia vikao vya Bunge’.
Waligomea vikao vya Bunge mwishoni mwa mwaka 2015, wakagomea vikao vya Bunge mwezi Februari, wakagomea vikao vya Kamati za Bunge kuelekea kwenye Bunge la Bajeti, na katika Bunge lenyewe la Bajeti ndiyo wakasusa kabisa. Bado ‘single yao haikuhiti’ kwa sababu kila kona wananchi waliwalaumu kwa kutowatendea haki waliowaajiri – yaani kule katika majimbo wanakotoka.
Sasa baada ya Bunge la Bajeti kufikia tamati, wenzako wakaamua kubadili gea angani. Kwamba wakataka waandamane kupinga ‘ubabe’ wa Naibu Spika. Hiyo yote ilikuwa ni danganya toto tu, walikuwa wanakulenga wewe, wanakujaribu wakati mwenyewe umekwishasema hujaribiwi.
Mheshimiwa Rais, wenzako wamekwishaweka mikakati na wanajipanga vilivyo kuhakikisha kwamba Alhamisi Septemba Mosi wanaingia mitaani kupinga hicho wanachokiita udikteta.
Badala ya kutumia nafasi hii kukijenga chama kwa kunadi sera kwa wananchi kila mahali wanakotokea pamoja na kuweka mikakati mingine, wao wameamua kuingia barabarani, yote ikiwa ni kutaka kuyumbisha utendaji wako, usiwatumikie wananchi kwa kutekeleza ahadi zako nyingi ulizozitoa na kuanza kushughulika nao, ili baadaye ukishindwa kutimiza ahadi waanze kutumia kama kigezo kwamba umeshindwa.
Si unakumbuka wakati wa awamu iliyopita jinsi jamaa walivyokuwa wakishinda mitaani kila leo? Si unakumbuka waliwahi kumpa Mheshimiwa Kikwete (Rais mstaafu wa Awamu ya Nne) siku tisa kuhakikisha anaondoa kodi zote kwenye vyakula?
Si hawa hawa jamaa ambao ukaidi wao wa amri za dola ulisababisha kifo cha mwandishi Daudi Mwangosi kule Nyororo, Iringa kwa kisingizio cha kwenda kufungua matawi ya chama – ambayo yalikwishazinduliwa na kiongozi wa Kanda kitambo – licha ya kuelezwa kwamba kulikuwa na tukio la kitaifa la Sensa ya Watu na Makazi?
Naam. Ilikuwa Septemba 2, 2012, na sasa wameichagua tena Septemba Mosi – sijui kuna nini hapa?
Leo hii tunamlilia Mwangosi pamoja na watu wengine waliopoteza maisha ama kujeruhiwa kama kule Arusha na Morogoro kwa sababu ya ukaidi wa hawa hawa jamaa, achilia mbali yule kijana aliyemwagiwa tindikali kule Igunga!
Si hivi karibu vijana wa chama hicho walisikika wakijitapa kwamba Polisi hawana ubavu wa kuwazuia na wasingewazuia wakati walipotaka kwenda kuzuia Mkutano Mkuu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Dodoma. Kwamba kusudio la jeshi hilo kuwazuia kwenda Dodoma, lisingefanikiwa kwa madai kuwa Bavicha ina nguvu kuliko polisi.
Mheshimiwa Rais, usiulize maandamano yao kama yana tija kwa taifa. Chadema wana maslahi na maandamano haya kwa sababu kwanza wakifanikiwa watakuwa wameweza kukuyumbisha wewe na serikali yako, lakini pia watakuwa wamewafurahisha wale walio nyuma yao. Usiniulize ni akina nani – kwa sababu hata mimi mwenyewe siwajui ila tu hisia zinajia kwamba ukiona nyumbu anageuka nyuma ujue ana mwenzake!
Chadema hawaogopi chochote, ni wakaidi, na wanatumia mtaji wa vijana wanaharakati wa kisiasa kufanikisha azma yao bila kujali madhara yanayoweza kutokea kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Walipinga sana Bunge kutoonyeshwa ‘live’ kwenye luninga kwa sababu wengi walikuwa wanapenda ‘kuuza nyago’ tu na siyo kujadili hoja za maendeleo ya msingi.
Si unakumbuka Mheshimiwa Rais wakati hata wewe unaingia Bungeni mwaka 1995 Bunge lilikuwa halirushwi ‘live’? Hivi kipindi kile mijadala ilikuwa inakwama kweli? Mbona ni katika kipindi hicho ambacho tulishuhudia wabunge wanaotokana na CCM wakiwa wakali na kusababisha mawaziri watano kuondoka katika wamu ya tatu – Profesa Simon Mbilinyi, msaidizi wake Mchungaji Kilontsi Mpologomyi, Dk. Hassy Kitine, Monica Mbega na Iddi Simba!
Unajua Mheshimiwa, picha inayonijia hapa ni kwamba, hata Watanzania tungewapa hawa jamaa dhamana ya kukaa pale Magogoni kamwe wasingepambana na ufisadi kama walivyokuwa wakijinasibu, nachelea kusema huenda ufisadi ungeongezeka mara 10 zaidi ya ilivyokuwa mwanzo.
Tena basi hata wasingekuwa na mawazo ya kuhamishia serikali Dodoma kama wewe ulivyofanikiwa kutegua kitendawili cha miaka 43 iliyopita.
Binafsi ninashangazwa sana na uamuzi wa hawa viongozi wa Chadema, na ninawashangaa zaidi wafuasi wao ambao wanakurupuka kuunga mkono hoja za viongozi wao bila hata kupima kama zina mashiko au la.
Wao wenyewe kwanza hawana demokrasia, wamejawa na ubabe na udikteta wa kutisha, sasa sidhani kama ni sahihi kwenda kusafisha nyumba ya jirani yako wakati ya kwako chafu. Wangeanza kwanza kutoa boliti kwenye majicho yao kabla ya kutazama kibanzi cha jirani yao.
Halafu, Mheshimiwa, hivi kukusanya kodi ni udikteta? Kuhimiza uwajibikaji nako ni udikteta? Sikuulizi wewe, lakini napenda yeyote mwenye majibu sahihi anijibu, kwa sababu siku zote Watanzania walikuwa wanalalamika kushuka kwa nidhamu ya kazi na kupotea kwa fedha za umma kwa wachache kula rushwa na kutokusanya kodi.
Umaskini wa Watanzania ulitamalaki na ndiyo maana kila mmoja alihitaji mabadiliko, ambayo Mheshimiwa Rais umeyaonyesha na unaendelea kuyaonyesha kwa vitendo.
Lakini kwa mwenye busara, ningeshauri apime na kutafakari kabla ya kuiendea Septemba Mosi. Watanzania tuna changamoto nyingi kuliko kushuhudia maandamano, ambayo licha ya kutokuwa na tija, lakini pia serikali imeshayapiga marufuku!
Chapa kazi Mheshimiwa Rais, miaka mitano siyo mingi, ni michache sana na huu siyo wakati wa siasa, watu wanataka maendeleo!
Alamsiki.

Mwandishi ni msomaji wa blogu ya www.maendeleovijijini.blogspot.com. Anapatikana kwa simu namba 0625640753

Comments