Featured Post

CHADEMA WAANZE NA ‘OPERESHENI UKUCHA’ KABLA YA KULETA ‘UKUTA’!



 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akizindua rasmi Operesheni Ukuta jijini Dar es Salaam.

Na Daniel Mbega
FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amekunjua makucha yake na kuuonyesha udikteta wake hadharani.
Amekwishatoa tamko kwamba, viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho ambao watashindwa kuandaa maandamano ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), Septemba Mosi, mwaka huu, watakuwa wamepoteza sifa za kuwa viongozi, kwani watakuwa wamewasaliti wananchi ambao waliwachagua.
Chadema imeitisha maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima kuanzia Septemba Mosi, lakini Rais John Magufuli alionya akiwa ziarani Kanda ya Kati hivi karibuni kuwa kutekeleza azma hiyo ni kumjaribu, na "kawaambie... sijaribiwi na sitakaa nijaribiwe."

Rais Magufuli ametamka bayana kwamba, kipindi cha siasa kimekwisha wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, na sasa Watanzania wanataka kuona maendeleo kwa sababu ndiyo wanayoyalilia kwa muda mrefu.
Akawaambia wapinzani kwamba, kama mtu anataka kufanya mikutano, basi aende katika eneo lake alilochaguliwa akafanye mikutano na wananchi wake kuhusu ni kwa namna gani atatekeleza ahadi alizozitoa wakati wa kampeni.
“Haiwezekani wewe ni Mbunge wa Mbeya halafu uende ukazungumze na wananchi wa Mwanza, nenda kazungumze na wananchi waliokuchagua uwaeleze jinsi utakavyotekeleza ahadi zako,” alionya.
Pamoja na jitihada zilizofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuionya Chadema isifanye maandamano hayo, lakini bado Mbowe ameendelea kuwahimiza wanachama wake kukaa mguu sawa kwa maandamano na mikutano ya nchi nzima.
Katika serikali ya awamu ya nne, Chadema walieleweka na operesheni zao nyingi, ikiwemo ile maarufu ya ‘Operesheni Sangara’ walioyoianzisha kupinga mafisadi nchi nzima.
Wakailaumu serikali iliyopita kwamba ‘ilikuwa imelala’ na kusema Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, ati alikuwa ‘anacheka’ tu bila kuwashughulikia mafisadi.
Wakatamani sana kwamba rais ajaye baada ya Kikwete, awe ‘dikteta’ ili awanyooshe mafisadi wanaokwiba mali ya umma, lakini leo hii Dk. Magufuli hajafikia hata kwenye chembe ya kuitwa dikteta, tayari wanalalama.
Anachokifanya Dk. Magufuli ni kusimamia misingi ya uongozi iliyopo bila kumuonea haya mtu yeyote anayekiuka misingi hiyo, anajitahidi kuhimiza maendeleo kwa wananchi na kuwawajibisha wazembe, wala rushwa na mafisadi, ati anaonekana dikteta.
Kimsingi kinachohimizwa na Mbowe kifanywe na Chadema hapo Septemba Mosi mimi nilidhani kingekuwa bora kama hiyo ingekuwa siku ya kwenda kila kona ya mtaa, kata na majimbo waliyoshinda kushiriki pamoja na wananchi wao shughuli za maendeleo ikiwemo kuendeleza na kukusanya nguvu ya pamoja katika kuboresha na kujenga miundombinu mipya ya kuchochea maendeleo.
Siku hiyo ingekuwa ni ya pamoja kupiga vita umaskini, kuhakikisha wanafunzi wanapata vyumba vya madarasa, vyoo safi, vifaa vya mashuleni ili wawe na mazingira bora ya kujifunzia na kuelewa vizuri katika kuleta maendeleo na demokrasia zaidi ndani ya chama ambayo haipo ndani ya Chadema ili kukifanya chama kiwe na wanamapinduzi na viongozi wazuri wa baadaye.
Badala yake Mbowe anataka kuendeleza mapambano la serikali ya Rais Magufuli jambo amabalo litakipotezea muda mwingi chama hicho na hatimaye kitaendelea kuitwa chama cha vurugu na maandamano yasiyo na tija kwa wananchi.
Hili litakuwa kosa jingine la kimkakati la Chadema baada ya kulifanya kosa la kukumbatia ufisadi waliokuwa wakiupinga kwa kuwakaribisha watu ambao awali waliwahubiri kuwa ni mafisadi wanaotafuna nchi, akiwemo Edward Lowassa, ambaye walimkabidhi nafasi ya kuwania urais.
Kosa jingine la kimkakati walilolifanya ni kukimbia Bungeni, ambalo halikuleta manufaa yoyote kwa wananchi waliowatuma kwa sababu kelele zao hazikuweza hata kubadili ratiba ya vikao vya Bunge hilo.
Haya ni maigizo ambayo Mbowe anayaendeleza na kamwe mabadiliko hayawezi kuletwa kwa kuendelea kutunishiana misuli na serikali pamoja na vyombo vyake vya dola, na kwa hakika pengo la Dk. Wilbrod Slaa linaonekana hadharani.
Siasa za uanaharakati kamwe haziwezi kuleta mabadiliko ya kweli ya kimaendeleo na kijamii nchini, zaidi zitajenga chuki kwa wananchi na kuzaa makundi ambayo mwishowe yatazua uhasama na kuhatarisha Amani ya taifa hili.
Mwalimu Julius Nyerere alisema; “Pingana, usipayuke!” (Argue, don’t shout!). Kama ni chama cha kidemokrasia, Chadema kingetoa hoja badala ya kuanzisha uanaharakati na maandamano.
Madiwani na wabunge wa Chadema wangefanya kwa vitendo kutekeleza shughuli za maendeleo kwenye kata na majimbo yao lingekuwa jambo la busara sana kwa sababu Watanzania wangepima maendeleo ya maeneo yao na yale ambayo yanaongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kuangalia ufanisi uko wapi.
Watanzania wamechoshwa na siasa, WWatanzania wamechoshwa na siasa, wanataka kuona changamoto zinazowakabili kama maji safi na salama, elimu, afya, miundmbinu na uchumi kwa ujumla zinapatiwa ufumbuzi badala ya kushuhudia maandamano.
Lakini haya yote yanatokea si kwa sababu ya kudai demokrasia kama inavyoelezwa, bali yanatokana na udikteta ulioota mizizi ndani ya Chadema kiasi kwamba kauli ikitolewa na Mbowe, basi wote hawana budi kutii.
Kitendo cha kuwatishia viongozi wote kwamba endapo hawataandaa maandamano Septemba Mosi watakuwa wamejiondoa kwenye uongozi ni cha kidikteta na hakina mantiki yoyote.
Kwanza itakumbukwa kwamba, wakati wa kuelekea kwenye Mkutano Mkuu wa CCM Julai 23, Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) lilikuwa limetangaza kwenda Dodoma kuzuia mkutano huo ambao ulishuhudia Rais Magufuli akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho.
Hiyo ilikuwa ni baada ya mikutano mfululizo iliyofanywa na Bavicha kuhakikisha kuwa wanakwamisha Mkutano wa CCM.
Lakini Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, akawaomba Bavicha wasiende Dodoma na badala yake wanapanga Plan B ya kuikwamisha Serikali ya CCM isitekeleze mipango yake.
Hata hivyo, Mbowe hakubainisha mipango hiyo ijapokuwa alisema kuwa taarifa rasmi ya nini chama kimepanga kufanya itatolewa baada ya kikao cha Kamati Kuu ambacho kilimalizika Julai 26, na hapo ndipo wakaibuka na ‘Operesheni Ukuta’, ambapo hakueleza zaidi kama operesheni hiyo ni mbadala wa Ukawa.
Pamoja na ombi hilo la Mbowe, si Bawacha, Bavicha au Baraza la Wazee liliojitokeza kutangaza kuunga mkono tamko la Mbowe, na ni hapo alipoibukia Arusha na kutangaza kwamba yeyote ambaye hataandaa maandamano hayo atakuwa ameoteza sifa za kuwa kiongozi kwa sababu ni msaliti.
Udikteta ndani ya Chadema imekuwa sehemu ya uongozi. Itakumbukwa namna Chacha Wangwe alivyoupigia kelele mwaka 2008 kabla ya mauti kumkuta, baadaye akajitokeza Zitto Kabwe kutaka kuwania uenyekiti, lakini udikteta ukatumika kumnyamazisha kwa kashfa zisizo na idadi.
Kabla hilo halijakaa sawa, David Kafulila na wenzake wakatimuliwa Chadema.
Kilichowapata Zitto Kabwe na Kitila Mkumbo mwaka 2013 wengi wanakikumbuka, pamoja na akina Juliana Shonza, Mtera Mwampamba na wenzao.
Leo hii yeyote anayetokea kupinga kauli ya Mwenyekiti Mbowe ni adui namba moja wa Chadema kuliko hata CCM. Atashughulikiwa kuanzia kwenye vikao vya chama mpaka kwenye mitandao ya kijamii.
Mbowe hatakiwi kunyooshewa kidole kwamba amekosea, na anataka atakachotamka ndicho kitekelezwe hata kama hakina maslahi na kinakiuka taratibu.
Huu ni udikteta uliokomaa ambao unaminya demokrasia na ingefaa zaidi kuanza na ‘Operesheni Ukucha’ (Umoja wa Kuondoa Udikteta Chadema) kabla ya kukimbilia kwenye Ukuta.
Wananchi wanapaswa kuyaona haya badala ya kukimbilia na kufuata mkumbo, kwa sababu ukiona taasisi yoyote inakuja na operesheni jua kuna maahali wameshaharibu.
Operesheni ya Ukuta inaonyesha kwamba kuna mahali Chadema wameharibu na wanataka kujisahihisha na kuondokana na madhaifu yao ya nyuma.
Tatizo linakuja kuwa bado wameshindwa kujua adui yao ni nani. Chadema inategemea kauli ya mtu mmoja, siyo ya wengi. Kama ni uamuzi wa wengi, basi Mbowe asingewasaliti wenzake akina Dk. Slaa na Profesa Ibrahim Lipumba kuhusu kumbebea mbeleko Lowassa na kupa nafasi ya kugombea urais kinyume na makubaliano waliyokuwa wameyafanya awali.
Kwa hiyo basi, kama Chadema wanataka kuona demokrasia ya kweli Tanzania – ambayo wanasema haipo – ni vizuri kwanza waitafute ndai ya chama chao wenyewe.
Ikiwa hawataki kuona Tanzania ikiongozwa na mtu mmoja, ambaye ndiye Rais (ambaye hata hivyo kikatiba ndiye mwenye dhamana ya kuongoza taifa), kwanza waanze kukataa kupelekeshwa na kiongozi mmoja ndani ya chama.
Kama kweli wanataka Watanzania wasimuogope Rais, basi waanze kwanza kumpinga mwenyekiti wao wa Chadema; kama wanataka kupata uhuru wa kuandamana kumpinga rais anayehimiza maendeleo ya Watanzania wote, wanachama hao wapate kwanza uhuru wa kuandamana kumpinga mwenyekiti wao ambaye hata kwenye chaguzi zote hataki kuwa na mpinzani.
Wanachadema wapate kwanza uhuru wa kutoa mawazo mbadala ndani ya chama chao ndipo wanapoweza kudai uhuru wa mawazo Tanzania. Kumbukeni, ukitaka kumulika alipo nyoka, lazima uanzie miguuni kwako! 
CREDIT: TAZAMA

Comments