Featured Post

BURIANI ABOUD JUMBE MWINYI, SHUJAA ALIYEPONZWA NA KUHOJI MUUNGANO!



Hayati Aboud Jumbe Mwinyi

Na Daniel Mbega
ABOUD Jumbe Mwinyi (96) hatunaye tena. Naam, rais huyo wa pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar amefariki dunia nyumbani kwake Mji Mwema, Kigamboni jijini Dar es Salaam na amefariki akiwa mwingi wa siku.
Taarifa zaidi bado hazitatolewa, hivyo haijulikani kama kiongozi huyo aliyepata pia kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wakati wa awamu ya kwanza atazikwa kiserikali au la.

Hiyo inatokana na wasia aliopata kuutoa mwenyewe mwaka 2000 baada ya kifo cha Rais mwingine mstaafu wa nne wa Zanzibar, Idris Abdul-Wakil Nombe, aliyefariki Machi 15, 2000.
Katika wasia huo, inaelezwa kwamba Alhaj Jumbe alieleza kwamba pindi mauti yatakapomfika asingependa kuona bendi wala mizinga ikipigwa, na kwamba jeneza lake lisifunikwe kwa bendera ya Taifa wala ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
"Sitaki bendi, sitaki mizinga, sitaki maombolezo wala lolote lingine lenye hata chembe ya kufuru," sehemu ya wasia huo iliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari huku akisisitiza kwamba angependa kuzikwa Kiislamu: "Mimi Aboud Jumbe Mwinyi, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunibariki kuzaliwa ndani ya Uislamu na namuomba aniruzuku kufa na kufufuliwa ndani ya Uislamu".
"Ni matumaini yangu kwamba kama Mwenye Enzi Mungu alivyonirehemu kuwa Muislamu, atanijaalia nikifa kukoshwa, kuvishwa sanda, kutiwa katika jeneza, kusaliwa na kuzikwa kwa mujibu wa sunna ya Mtume Muhammad (s.a.w.).
"Nikiwa hai, dhamana ya vitendo vyangu inaniangukia mimi mwenyewe, nikifa dhamana ikiwa vitendo vyema au vibaya nitakavyofanyiwa itawaangukia waandalizi, watendaji na wenye kushiriki katika vitendo hivyo", anadaiwa kusisitiza katika wasia huo uliosainiwa na Msaidizi wake Bwana Abubakar.
Wasia huo anadaiwa aliutoa mbele ya Mufti wa Zanzibar, Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Naibu Kadhi Mkuu, Mwanasheria Mkuu, Sharrif Juneid, Masheikh wengine na wanawe.

Jumbe ni nani?
Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi alizaliwa Juni 14, 1920 mjini Juba, Sudan Kusini. Alishika nafasi mbalimbali za uongozi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ndani ya Afro-Shiraz Party (ASP) na yeye na Mwalimu Julius Nyerere ndio walioviunganisha vyama vya ASP na Tanu na kuzaliwa CCM Februari 5, 1977.
Baada ya kifo cha Sheikh Abeid Amaan Karume Aprili 7, 1972 yeye ndiye aliyeteuliwa kuwa Rais wa SMZ na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, wakati huo huo akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata baada ya kuzaliwa kwa CCM, yeye akawa Makamu Mwenyekiti wa CCM.
Yeye ndiye aliyesimamia kupatikana kwa Katiba ya kwanza ya Zanzibar mwaka 1979 baada ya Mapinduzi ya 1964.
Jumbe alikuwa Rais wa SMZ kuanzia Aprili 11, 1972 hadi Januari 30, 1984 alipovuliwa vyeo vyote mjini Dodoma.
Lakini unapozungumzia kuhusu Muungano wa Tanzania, lazima pia umzungumzie Alhaj Aboud Jumbe ambaye alikuwa sehemu kubwa ya utawala wa Visiwa vya Zanibar kwa takribani miaka 12.
Jumbe ana historia ndefu ya siasa za Visiwa hivyo, na mtazamo wake unawafanya mpaka leo wengi wajiulize kama ni shujaa, mpinga Muungano ama mtu aliyekuwa amekata tamaa.
Tukio la kujiuzulu kwake kwa shinikizo miaka 32 iliyopita linaweza kuwa ni historia nyingine ngumu kuelezeka kwa siasa za Tanzania. Nakumbuka hata mimi, ambaye wakati huo nilikuwa shuleni, sikuweza kuelewa kiini hasa cha kujiuzulu kwa kiongozi huyo mkubwa kabisa nchini.
Kwa kipindi ambacho nchi nyingi zilikuwa ndiyo kwanza zimetoka katika makucha ya ukoloni huku zikipigania kujenga chumi zao changa, tukio la kujiuzulu kiongozi lilionekana geni sana, ingawa huko nyuma tulikuwa tumeshuhudia viongozi kadhaa wakijiuzulu, akiwemo Alhaj Ally Hassan Mwinyi ambaye alijiuzulu mwaka 1978 kufuatia wimbi la mauaji ya watu, hasa vikongwe, kule Shinyanga.
Hata hivyo, suala la kujiuzulu kwa Jumbe halikuweza kujadiliwa mitaani kwa kipindi kile, tofauti pengine na kipindi hiki ambapo watu wangeweza hata kutoa hoja zao nyingi kuhusiana na kiini cha kujiuzulu kwake.
Kwa kipindi ambacho ilikuwa vigumu kunyoosha kidole hata kwa mtendaji wa kijiji, hakika ingekuwa vigumu kama kuuhamisha Mlima Kilimanjaro kwenda Dodoma kuhoji uamuzi wa kiongozi wa juu kama rais.
Jambo la msingi kuhusiana na kujiuzulu kwake ni kutambua kwamba Jumbe alitaka, na hata kesho angetaka, kuona Nyaraka za Muungano zinapitiwa upya ili kuleta usawa wa pande zote mbili zilizounda Muungano huo, Bara na Visiwani.
Ingawa yeye pia alishiriki katika maandalizi ya Nyaraka hizo, lakini hakuwa na mamlaka ya juu kipindi hicho kwa vile alikuwa chini ya mtu, na miaka takribani 20 baadaye aliona kuna haja ya kufanya mapitio mapya kuona Zanzibar inapewa heshima yake katika baadhi ya masuala yaliyoonekana kuingiliwa na Serikali ya Muungano.
Ndiyo maana hata katika kitabu chake cha Tanganyika and Zanzibar: The Partner-ship alichokitoa mwaka 1994, miaka 10 baada ya kujizulu kwake, alielezea kwa kirefu ni kwanini alitaka yafanyike mapitio ya Nyaraka za Muungano.
Anasema alimweleza Mwalimu Nyerere wakati wa kuadhimisha miaka 20 ya Mapinduzi Januari 12, 1984 kwamba kulikuwa na kero ambazo Wazanzibari waliona zilistahili kuzungumzwa ili kuimarisha Muungano huo.
Alikuwa amejiandaa kuelezea kwa kirefu kero hizo kwenye vikao husika, lakini kabla ya hapo akaandaa waraka uliopaswa kwenda kwa Mwenyekiti wa CCM, Mwalimu Nyerere. Kwa kuwa waraka ule ulikuwa umeandikwa kwa mkono, tena kwa lugha ya Kiingereza, alimpa mtu kuuchapa. Ukapotea katika mazingira ya kutatanisha.
Lakini ajabu ni kwamba, siku chache baadaye aliitwa Ikulu kwa Mwalimu Nyerere na alipokwenda akashangaa kuukuta waraka ule ule aliouandika mwenyewe kwa mkono wake ukiwa mkononi mwa Nyerere! Namna ulivyofika mimi, wewe na hata yeye mwenyewe hatujui, lakini Mwalimu angekuwa hai leo angeweza kutueleza aliupataje, kama tungekuwa na haja ya kujua hilo.
Na kwa vile tayari Jumbe alikuwa ameonyesha nia yake ya kujiuzulu wadhifa wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mwalimu alimwambia kwamba kama isingekuwa kwa waraka aliokuwa nao mkononi, katu asingekubali kujiuzulu kwake, lakini kwa yale aliyokuwa ameyaainisha kuhusu Muungano, naye alikuwa radhi kuona anajiuzulu.
Ndipo Januari 30, 1984, katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM kule Dodoma, akaamua kujiuzulu nyadhifa hizo. Ali Hassan Mwinyi, mtu aliyekuwa akiiunga mkono Tanzania Bara, akachukua madaraka na watu kadhaa walioonekana kuwa wapinzani wakakamatwa.
Mwinyi akaanzisha mfumo wa usawa Visiwani na Bara kabla hajawa rais wa Muungano mwaka 1985 baada ya Mwalimu Julius Nyerere kung’atuka huku Zanzibar ikiongozwa na Idris Abdul Wakil Nombe. Mwaka 1990 Dk. Salmin Amour Juma akachaguliwa Rais wa Zanzibar; akarejea tena madarakani katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 ambao unadaiwa haukuwa huru na wa haki.
Aboud Jumbe alipochukua urais baada ya mauaji ya hayati Sheikh Abeid Amani Karume mwaka 1972, jamii yote ilitegemea kwamba mambo ya kale yalikuwa yamefikia kikomo.
Na kwa kiasi fulani ndivyo ilivyokuwa, kwani utawala wake ulilegeza baadhi ya mambo kuliko ule uliotangulia, lakini kwa kuwa alikuwa chini ya Baraza la Mapinduzi, alipaswa kutekeleza baadhi ya sera ngumu zilizokuwepo, pale ilipobidi, kwa utashi wa washirika wake katika uongozi.
Wazanzibari wanakumbuka kwamba mlongo mmoja wa utawala wake ulitawaliwa na hali ya Zanzibar kuegemea zaidi Bara na mwaka 1977 akaongoza muungano wa vyama vya Afro-Shiraz na kile cha Tanganyika African National Union (TANU) cha Bara kuzaa Chama Cha Mapinduzi (CCM), chama ambacho bado kinaendelea kushika hatamu za uongozi hata leo.
Lakini kwa kiasi kikubwa, chini ya Jumbe watu walikuwa na uhuru na waliweza kusafiri ulimwenguni bila matatizo makubwa tofauti na serikali ya ‘mkono wa chuma’ ya hayati Karume. Hali hii ikamfanya kuwa kipenzi cha Wazanzibari wengi.
Jumbe huyu pia akafungua taasisi mbalimbali za elimu Tanzania Bara kwa ajili ya Wazanzibari waliopenda kuchukua elimu ya juu. Hali hii iliwawezesha Wazanzibari kufika mbali zaidi kielimu badala ya kusomea ualimu, taaluma pekee ambayo walikuwa na uwezo wa kuipata.
Siku za nyuma, nafasi za uongozi serikalini zilikuwa zikitolewa kwa watu waliokuwa kwenye mfumo wa chama tu, na zaidi ya kazi ya ualimu hakukuwa na uwezekano wowote wa watu kupata elimu ya juu zaidi.
Mnamo mwaka 1979, Jumbe aliweka historia kwa kufungua taasisi ya kwanza ya kidemokrasia, Baraza la Wawakilishi, lakini wajumbe wa baraza hilo walikuwa wakiteuliwa badala ya kuchaguliwa na wananchi wenyewe. Pia alifungua utawala wake kwa watu, ambao wangeweza kuwa pembeni kama kanuni ngumu za mapinduzi zingezingatiwa kama ilivyokuwa awali.
Hatua hii, ambayo baadaye alijikuta akiijutia, ndiyo iliyokuwa chanzo cha kuanguka kwake. Alikuwa haelewani na wale waliojulikana kama ‘Kamati ya Watu 14’ ambayo iliwahusisha watu wengi walioshiriki kwenye Mapinduzi. Ushawishi wao ulianza kupungua na madaraka yao yakaanza kuhojiwa.
Katika jaribio lake la kutaka kuokoa jahazi kutokana na matatizo hayo akawatema wajumbe wengi katika serikali yake na kufanya jaribio la kujitenga kutoka katika serikali moja kuu kwa Tanzania nzima. Lakini mwaka 1984 akalazimishwa na Kamati Kuu ya CCM kujiuzulu.
Hatua ya kujiuzulu kwake, kwa mwanamapinduzi inaweza kuchukuliwa kuwa ya kishujaa kutokana na hoja zile alizokuwa akizitetea. Hakujutia uamuzi wake, ingawa alisikitishwa kutokana na yale aliyokuwa ameyaainisha kushindwa kuwafikia wananchi wengi, ambao ni dhahiri hata leo hii hawajui ni kipi hasa alichokuwa akikipigia kelele.
‘Kwa shujaa huenda kilio, kwa mwoga huenda kicheko’, ndivyo Waswahili wasemavyo. Wale ambao hatukumwelewa Jumbe wakati huo tulimuona kama mtu aliyechanganyikiwa kueleza kasoro hizo ambazo hazikuwa na mantiki yoyote kwa kipindi hicho huku tukiendelea kuimba na kuzinadi sifa mbalimbali za viongozi wa chama na serikali.
Lakini leo hii yale ambayo alikuwa akiyasema Jumbe na kuyapigania tumeyaona Zanzibar. Kero za Muungano zimekuwa nyingi mno kiasi cha kuifanya hali ya amani Visiwani kuwa tete tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 ambapo baadhi ya wachunguzi wa masuala ya siasa wanadai kura ziliibwa ili Chama cha Wananchi (CUF) kisitawale.
Kero hizo ndizo zinazozidi kujenga ufa mkubwa hata ndani ya CCM Visiwani humo, na ingawa viongozi wake wanajitahidi kuficha, ukweli bado unaendelea kubaki pale pale kwamba kuna tatizo, tena kubwa.
Ujio wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba ukaibua mapya, kwa sababu ulikuja na mapendekezo ambayo Jumbe alikuwa ameyaeleza – hata kwenye kitabu chake. Na hoja ya kuwa na serikali tatu ikachukua nafasi.
Pengine lingekuwa jambo la busara sasa kumpa heshima ya ushujaa Alhaj Jumbe kwa yale yote aliyoyatenda enzi za utawala wake, pia hata kwa mawazo yake aliyokuwa ameyaandika kwenye waraka ambao ulimfikia mhusika hata kabla ya kuusaini mwenyewe.
Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ile ya Muungano hawapaswi kupuuza kero hizo kwa misingi ya kulinda chama, kwa sababu kama hazikutatuliwa siyo tu zitauvunja Muungano wenyewe, bali hata mustakabali wa chama utakuwa mashakani.
Buriani Jumbe. Mungu akupe pumziko la Amani!

Comments