Featured Post

BEI YA NYANYA YAPOROMOKA MKOANI MTWARA

By Haika Kimaro, MwananchiMtwara. Wafanyabiashara mkoani hapa wamelalamikia kupata hasara baada ya nyanya kuoza kwa kukosa wateja.
Wafanyabiashara hao wameiomba Serikali kuwajengea kiwanda cha kusindika mazao ya mbogamboga  ili kuondokana na hasara wanayoipata baada ya bidhaa zao hizo kuharibika.
Awali, Mtwara ilikuwa ikitegemea nyanya kutoka nje ya mkoa huo hali iliyosababisha bidhaa hiyo kuuzwa bei ya juu, lakini kwa sasa imeshuka kutoka Sh52, 000 kwa tenga hadi kufikia Sh12,000.
Mfanyabiashara Shahi Cheleuka alisema:  “Biashara ya nyanya sasa imekuwa hasara kutokana na wakulima kuwa wengi kuliko mahitaji kwa sababu asilimia kubwa ya nyanya zinazolimwa ni kwa ajili ya Mtwara pekee.”
Mwenyekiti wa Soko la Sabasaba, Selemani Mmoja aliiomba Manispaa ya Mtwara Mikindani kuwatafutia soko wafanyabiashara hao ili waweze kulipa ushuru baada ya  kuuza nyanya.
“Ni kweli biashara ya nyanya na mbogamboga imekuwa ngumu, naiomba manispaa iwatafutie  masoko nje ya Mtwara wafanyabiashara ili na manispaa nayo ipate ushuru kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake,” alisema Mmoja.
MWANANCHI


Comments