Featured Post

UKITAKA MAZIWA MENGI, BASI FUGA MBUZI AINA YA ALPINE




 Majike ya Alpine yenye pembe
 Dume la Alpine


Jike la Alpine lisilo na pembe.

Na Daniel Mbega
Mbuzi jamii ya Alpine, mara nyingi wakifahamika kama French Alpine, wana shingo ndefu na ngozi nzito ambayo huwa na rangi mbalimbali, na kila moja ina jina lake. Kwa kawaida, rangi ya mbele ni tofauti na rangi ya nyuma japokuwa baadhi wana rangi ya aina moja.
Mbuzi jike mkubwa huwa na uzito wa kilogramu 61.2 na beberu huwa na uzito wa kilogramu 77. Mbuzi jamii ya Alpine ndio hutoa maziwa mengi zaidi kuliko jamii nyingine za mbuzi wa maziwa, ambapo mbuzi moja hutoa takriban lita 907.18 za maziwa kwa mwaka yenye kiwango cha siagi cha asilimia 3.5.

Mbuzi hawa wa Alpine wana maumbile yenye ukubwa wa kati na makubwa zaidi, ni warefu wa kimo, na ndiyo jamii pekee ya mbuzi wenye masikio yaliyoinuka ambayo huwa na rangi tofauti na kuwatofautisha na wengine.
Mbuzi jamii ya Alpine ni wastahimilivu, wanaoweza kuishi katika mazingira yoyote na kuwa katika afya bora pamoja na kutoa maziwa ya kutosha. Manyoya yao ni mafupi. Nyuso zao ndefu, rangi kama za jamii ya Toggenburg inapatikana pia.

Walikotokea mbuzi wa Alpine
Inaaminika kwamba, mbuzi ndio wanyama wa kwanza kufugwa na binadamu. Mifupa ya mbuzi iliwahi kupatikana kwenye mapango pamoja na dalili za uwepo wa binadamu kuishi kwenye mapango hayo. Mojawapo kati ya mifupa ya mbuzi ilikuwa na uthibitisho kwamba mguu mmoja ulikuwa umepona baada ya kuvunjika na kupona kwake kunaweza kuwa ni kwa msaada wa binadamu. Wanasayansi wanasema mbuzi huyo angeweza kufa porini bila msaada wa binadamu. Mabaki hayo ya mbuzi yamechunguzwa kwa kutumia carbon na inaonekana mbuzi huyo aliishi kati ya miaka 12,000 – 15,000 iliyopita. Mbuzi hao walikuwa wa Kiajemi (Mashariki ya Kati) maarufu kama “Pashang.” Baadhi ya mbuzi wa Pashang walihamia kwenye Milima ya Alps. Inawezekana kabisa baadhi ya mbuzi hao walihamia Milima ya Alps wakiwa na binadamu waliokuwa wakiwafuga na wanyama wengine wa mwitu wakawepo pia milimani.
Mbuzi wa Alpine wa sasa asili yao ni mbuzi wa Pashang, pia wanajulikana kama Bezoar. Kwa hiyo mbuzi hawa wa Alpine wanapatikana kwa wingi katika maeneo ya Milima ya Alps barani Ulaya.
Kwa maelfu ya miaka, jamii ya mbuzi wa Alpine imeendelezwa katika hali ya ustahimilivu kwenye miteremko mikali ya milima ambako wamekuwa wastahimilivu na wanaweza pia kuishi hata kwenye jangwa bila shida. Ni katika kipindi hicho ambapo wafugaji barani Ulaya walianza kuwafuga kwa ajili ya maziwa.
Uwezo wa mbuzi hao wa Alpine kuzowea mazingira haraka, ustahimilivu, na rangi zao murua ambazo zinavutia umewafanya waenee sehemu nyingi duniani ambako walisambazwa katika safari za awali za mahajazi na meli. Safari za awali za majahazi na meli zilikuwa zinaonekana nzuri zaidi kama watu walichukua pia na mbuzi kwa ajili ya maziwa na nyama. Manahodha wa zamani waliacha jozi moja ya mbuzi katika visiwa ambako safari zao zilipitia na waliporejea walikuta mbuzi hao wamezaliana hivyo waliweza kuwakamua maziwa ama kuwachinja kwa kitoweo. Hivi leo mbuzi wa jamii ya Alpine wanapatikana katika mazingira yote duniani.
Usishangae leo ukisikia kuna aina nne au tano za Alpine: French Alpine, Rock Alpine, Swiss Alpine (ambao sasa wanaitwa Oberhasli), German Alpine na hata American Alpine.
Mbuzi hawa wanapatikana hata katika Afrika Mashariki, hivyo unaweza kumuuliza ofisa mifugo akakuelekeza namna ya kuwapata. Ni wazuri kama umeamua kufanya ufugaji wa kibiashara wa mbuzi wa maziwa kwa sababu wanatoa maziwa mengi kuliko jamii nyingine za mbuzi.

Ikiwa una maoni au ushauri, usisite kunipigia au kunitumia ujumbe wa simu au whatsapp kupitia namba 0656 331974 au nitumie barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.


Comments