Featured Post

NUBIA NDIO MBUZI WA MAZIWA NA NYAMA WANAOWEZA KUSTAHIMILIA HALI YA JOTO SANA


Dume na jike la Nubia

 Jike la Nubia

Na Daniel Mbega


Hapa tutazungumzia aina mbili za mbuzi wa maziwa jamii ya Nubia. Kwanza kuna mbuzi wa Nubia wa asili ambao kwao hasa ni Sudan na ukanda wa kusini wa Misri. Mbuzi hawa wa Nubia ndio maarufu zaidi kwa watengenezaji wa cheese na ice cream kutokana na maziwa yao kuwa na mafuta mengi kuliko mbuzi wengine.

Mbuzi hawa wako katika rangi mbalimbali na ndio mbuzi wakorofi zaidi kati ya jamii za mbuzi wa maziwa.

Unaweza kuwatofautisha mbuzi wa Nubia na jamii nyingine kutokana na uso wao wa duara (maarufu kama pua ya Kirumi) na masikio marefu yaliyotepeta. Mbuzi jike mkubwa ana uzito wa zaidi ya kilogramu 61 wakati beberu ana uzito wa zaidi ya kilogramu 77. Jike la Nubia linatoa wastani wa lita 680 za maziwa kwa mwaka yenye kiwango cha asilimia 4 ya siagi.

 Dume la Nubia


Halafu kuna mbuzi aina ya Anglo-Nubia, ambayo huko Marekani wanaiitia Nubia tu. Jamii hii ni chotara ambao walipatikana nchini Uingereza kutokana mbuzi jike wa asili wa maziwa wa Uingereza na madume kutoka Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati.

Mbuzi hawa hawana tofauti sana na Nubia wa asili kwa sababu sifa zao kubwa ni miili mikubwa, masikio makubwa na marefu yaliyotepeta na pua ya Kirumi.

Kutokana na asili yao ya Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati ambako kuna jangwa na joto jingi, Anglo-Nubia wanaweza kuishi katika mazingira ya joto kali na wana msimu mrefu wa kuzaa kuliko jamii nyingine ya mbuzi wa maziwa.

Anglo-Nubia wanafahamika zaidi kama mbuzi wa maziwa na nyama pia, lakini ni maarufu kwa maziwa yao ambayo yana mafuta mengi, ingawa kwa wastani, wanazalisha kidogo kuliko jamii nyingine za mbuzi hao wa maziwa.

Anglo-Nubia ni wakubwa, ambako jike linafikisha uzito wa kilogramu 64 wakati dume linaweza kufikisha hadi kilogramu 90.

Wastani wa kimo kwa mbuzi hawa wa maziwa wakipimwa ni sentimeta 81 kwa jike na sentimeta 94 kwa beberu.

Kama ilivyo kwa jamii zote za mbuzi wa maziwa, mbuzi hawa wanapaswa kuondolewa pembe kwa kuzikata mara kwa mara tangu wanapokuwa na wiki mbili bada ya kuzaliwa. Hiyo inaleta usalama kwa ajili ya utunzaji na ukamuaji, hasa ikizingatiwa pia kwamba jamii hii ni wakorofi.

 

Asili yao


 
Kama nilivyoeleza hapo awali, Anglo-Nubia ni mbuzi chotara wa uzao uliopatikana nchini Uingereza baada ya kupandisha jike la mbuzi wa maziwa wa asili Old English Milch Goat na beberu la Zariby kutoka India na Russia pamoja na beberu la Nubia kutoka Sudan. Mbuzi hao wamsambazwa sehemu mbalimbali duniani kwa sasa na huko Marekani wanafahamika kama Nubia tu.

Kwa hiyo, mbuzi wa Anglo-Nubia halisi ni lazima awe yule ambaye ni mkubwa na mwenye asili mchanganyiko ya Asia, Afrika na Ulaya ambaye anafahamika kwa utoaji wa maziwa yenye siagi nyingi.

Kama unataka kuwafuga, wasiliana na ofisa mifugo aliye jirani ili akuelekeze wapi pa kuwapata pamoja na mambo ya msingi kuyazingatia katika ufugaji.



Ikiwa una maoni au ushauri, usisite kunipigia au kunitumia ujumbe wa simu au whatsapp kupitia namba 0656 331974 au nitumie barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.



Comments