Featured Post

MBUZI WA MAZIWA: UPANDISHAJI, UZALISHAJI NA UTUNZAJI WA WATOTO


 Na Daniel Mbega
 Mbuzi wa maziwa wanatoa maziwa, lakini baada ya kuzaa. Hii maana yake ni kwamba lazima uwapandishe (breeding), hivyo unahitaji kuwa na beberu au kwa Kiingereza buck.
Kama unazingatia ufugaji bora wa mbuzi, hakika kipengele hiki ni muhimu sana kwako, vinginevyo itakuletea changamoto kubwa. Kuwalisha, kuwanyweshwa na kuwatibu tu hakusaidii ikiwa utashindwa kuwaangalia katika masuala haya muhimu ya kuanzia kuwapandisha, kuwazalisha na kuwatunza watoto wanapozaliwa.
Wafugaji wachache wanaoanza ujasiriamali hushauriwa kutafuta beberu kwa sababu ya kuboresha uzao, kupunguza gharama, na kuweka harufu ya beberu zizini.
Lakini ni rahisi kujua wapi anapatikana beberu na kumsafirisha mbuzi wako jike wakati anapokuwa katika joto tayari kwa kupandwa (heat period).

Mbuzi jike anaweza kupandishwa wakati anapofikisha uzito wa kilogramu 39 hadi 40, hususan anapokuwa amefikisha umri wa miezi tisa ambao ndio umri bora kumpandisha.
Mbuzi majike ni wepesi kushika mimba wanapokuwa katika kilele cha joto ndani ya siku 2-3 kila baada ya siku 18-23, hususan wakati wa masika au kipupwe. Wakati mwingine ni kati ya Septemba na Januari kutegemeana na mazingira na hali ya hewa.
Dalili ambazo ni muhimu kuziangalia ni pamoja na kuchezesha sana mkia, anakuwa hajatulia, anaweza kuwakimbiza wenzake au wenzake wakamkimbiza, sehemu za uzazi kuvimba kidogo na wakati mwingine kutoa majimaji, na kukojoa mara kwa mara. 
Ukiona hivyo nenda katafute lilipo beberu mpeleke huyo jike. Kama beberu atampanda halafu yeye akiwa ametulia, tambua kwamba yuko katika joto. 
Weka rekodi ya tarehe, na subiri dalili hizo za joto wiki tatu baadaye ambao ndio mzunguko wake (siku 21). Kama usipoziona dalili hizo, tambua kwamba tayari mbuzi wako ana mimba. Halafu weka alama kwenye rekodi zako za tarehe ukitegemea kwamba anaweza kuzaa baada ya siku 145 au 150 tangu ulipompandisha.
Chagua beberu bora, na kama unajua mbuzi wako jike ana matatizo, kama vile ya miguu, basi chagua beberu ambaye ni imara.
Mbuzi mwenye mimba anahitaji uangalizi maalum na makini. Kama ulikuwa unamkamua, jaribu kuwacha miezi miwili kabla ya kujifungua. Kimsingi inashauriwa baada ya kupandwa usimkamue tena, lakini inakuwa vigumu kwa mbuzi ambaye unamtegemea na anatoa maziwa mengi. Njia mbadala ni kupunguza kumpa chakula cha nafaka. Katika mazingira mengi, mbuzi anapokuwa na mimba hupunguza utoaji wa maziwa na inafikia mahali unaona hakuna haja ya kumkamua kwa sababu maziwa ni kidogo.
Hapo sasa unapaswa kumpa chakula cha nyuzi nyuzi ambacho kina kiasi kidogo cha protini hasa katika miezi mitatu ya kwanza ili kuruhusu watoto wakue tumboni, vinginevyo atanenepeana na vitoto vitakosa afya na kukua taratibu. Theluthi mbili ya ukuaji wa watoto tumboni huwa ni katika wiki nane za mwisho. Katika kipindi hicho chakula chake kiongoezwe na kiboreshwe, lakini bila kuweka protini nyingi, ili ajenge mwili pamoja na kusaidia watoto wajijenge. Vitamin na madini, hususan iodine, kalsiumu na vitamin A na D ni muhimu sana.

Kuzaa

Siku chache kabla ya kuzaa, muweke mbuzi huyo kwenye banda safi la peke yake ukimuwekea matandazo safi ya kulalia, maji, na nyasi nzuri. Usije ukashangaa wakati utakapoamka asubuhi na kukuta mbuzi ana watoto wawili au watatu, hata kama hakuonyesha dalili za utungu.
Ni jambo muhimu sana kupanga kuwa karibu na mbuzi wako anapozaa – lakini kwanza lazima uanze kuwa karibu naye kuanzia siku ya 140 baada ya kupandwa. Kuna dalili nyingi za kuangalia. Unaweza kuwagusa watoto kwa mkono wakati mbuzi anapokuwa ametulia na wanaweza kuwa katika kila upande wat umbo. Kama utafanya hivyo mara mbili kwa siku utagundua kwamba ni wakati gani huwagusi. Basi hapo tambua kwamba mbuzi huyo anaweza kuzaa ndani ya saa 12 zijazo. Wakati mtoto wa kwanza anapokaribia kuzaliwa, mbuzi atalazimika kulala ubavu. Kadiri muda unavyokaribia, mbuzi ataanza kulalamika. Anaweza kutoa ute wa manjano.
Wakati anapokuwa na utungu anaweza kukwangua sakafu na kulala na kusimama tena mara nyingi huku akihangaika. Kama atakuwa na utungu kwa zaidi ya saa mbili au anaonekana kuwa na matatizo, mwite mtu mwenye uzoefu na mifugo hata jirani, na kama wewe mwenyewe ni mzoefu, basi ni jambo jema. Njia nzuri ya kujifunza kukabiliana na nyakati hizo ngumu ni kujifunza kwa kumwangalia mtu mzoefu anavyofanya.
Uzazi wa kawaida unaweza kudumu kwa saa nne au zaidi, lakini ukiona kwamba kuna matatizo ya uzazi kwa mbuzi – kama kutokeza mguu mmoja ukiwa umejikunja, au kitovu kikiwa kimejiviringa – na unataka kumsaidia mbuzi, hakikisha unanawa mikono yako kwa sabuni yenye dawa (germicidal soap) na kupaka mikono mafuta yenye madini, kabla ya kuingiza mikono yako kumsaidia.
Kwa bahati nzuri, mambo kama haya yanaweza yasitokee mara ya kwanza unapokuwa umejianza ufugaji wako, lakini ikiwa yatatokea wala usishangae. Ingiza mikono yako, jaribu kuangalia mikono ya mbele na kichwa halafu saidi kuvivuta taratibu ukisubiri mbuzi asukume kwanza.
Ninazungumza haya kutokana na uzoefu wangu katika ufugaji, kwa sababu nimekwishawahi kusaidia hata ng’ombe kuzaa. Kama una uzoefu na ujasiri ni jambo linalowezekana.
Mara ya kwanza haikuwa rahisi kwangu. Nakumbuka ilitokea mwaka 1978 wakati nikiwa mdogo. Nilikuwa nachunga kundi la mbuzi, kondoo na ndama. Mbuzi mmoja mwenye mimba akapata uchungu. Sikujua nifanye nini kwa sababu tayari mbuzi wengine – kama walivyo wasumbufu – walikuwa wakiendelea kusonga mbele porini wakichunga.
Kumwacha huyu anayetaka kuzaa sikuona jambo la busara, ikabidi nimsubiri. Kwa kuwa sikuwa na uzoefu, huku nikifikiria kwamba mbuzi wengine wamekwishasonga mbele, nikaanza kulia peke yangu.
Baadaye nikaona ujinga kwa sababu kilio changu kisingeleta maana yoyote. Pamoja na kutokuwa na uzoefu, nikamsogelea mbuzi yule aliyelala akihangaika. Silaha zangu za jadi nikaziweka chini. Kitoto cha mbuzi kilikuwa kinagoma kutoka kwa sababu mguu mmoja ulitangulia na mwingine ulikuwa umejikunja. Nikaingiza mkono na kumshika taratibu na kufanikiwa kuuvuta mguu, hatimaye kitoto kikatoka salama. Nikasubiria kitoto cha pili, nacho kikatoka salama baada ya kumsaidia mbuzi yule kwa mara nyingine.
Baada ya kuvisafisha na kuviacha vinyonye kidogo, nikavibeba na kuondoka huku yule mama yao akipiga kelele. Kumwongoza haikuwa rahisi kwa sababu anawataka watoto wake, hivyo nikaamua kutangulia mimi na yeye akanifuata kueleka waliko mbuzi wengine ambapo nilimpatia watoto wake akawanyonyesha. Kwa vile watoto wale hawakuwa na nguvu na uwezo wa kutembea, kazi yangu ya kuchunga ikawa ngumu kwa sababu muda wote nililazimika kuwabeba. Na niliwabeba vivyo hivyo hadi kwenye boma muda wa kurudi ulipofika.
Nakumbuka baba yangu alinizawadia. Akaenda kuninunulia kaptura ya khaki mnadani! Zawadi kubwa sana enzi hizo katika mazingira yetu ya kushinda ukiwa umevaa lubega tu! Baada ya hapo sikuwa na hofu tena, na niliwasaidia hata ng’ombe walipokuwa katika matatizo ya kuzaa.
Hatua muhimu baada ya kuzaa ni kuondoa utando kwa watoto ili kuwafanya wapate hewa (mama yao anaweza kufanya hivyo kwa kuwalamba kama wewe haupo), wawekee iodine kwenye vitovu ili kuzuia maambukizi hasa ya bakteria na uwakaushe watoto.
Taratibu jaribu kukamua maziwa kutoka kila titi ili kujiridhisha kwamba linafanya kazi na siyo limeziba.
Safisha matandazo ya kulalia na weka mengine safi. Hakikisha kwamba watoto wanapata maziwa ya kwanza (colostrum), ikibidi yakamue na uwanyweshe watoto kwa kutumia chupa maalum yenye nyonyo kama zile za watoto. Maziwa hayo mazito ya njano yanayotoka katika siku za kwanza ni muhimu kwa ukuaji wa watoto.
Mbuzi anayenyonyesha huhitaji chakula kingi zaidi ili kukidhi mahitaji ya mwili na kuzalisha maziwa kwa ajili ya watoto. Pamoja na nyasi, mikunde na majani ya miti, malisho kilo 1.8 – 2.5 kwa siku ni muhimu apewe chakula cha nyongeza kilo 0.3 – 0.8 kwa kila lita ya maziwa inayoongezeka baada ya lita 2 na maji safi, salama na ya kutosha wakati wote.

Utunzaji wa watoto
Kwa kawaida, utunzaji wa watoto wa mbuzi huanza mara tu baada ya kuzaliwa. Kuna nadharia nyingi za kuwalea watoto wa mbuzi, lakini njia ya asili ni kuwaacha na mama yao. Hiyo haiwezi kuwa namna bora kama unafuga mbuzi kwa ajili ya maziwa.
Lakini kama nilivyosema hapo awali, mfugaji ahakikishe kitoto cha mbuzi kinapata maziwa ya mwanzo (manghanda) ndani ya saa 24 tangu kuzaliwa na kwa muda wa siku 3. Kama kinanyweshwa maziwa, kipewe lita 0.7- 0.9 kwa siku. Maziwa haya, ni muhimu kwani yana viinilishe na kinga dhidi ya magonjwa.
Ikitokea mama hatoi maziwa au amekufa, inashauriwa kutengeneza maziwa mbadala ya aina hiyo au kama kuna mbuzi mwingine aliyezaa anaweza kusaidia kukinyonyesha kitoto hicho.
Hata hivyo, wafugaji wengi wa mbuzi wa maziwa huwaondoa watoto kwa mama yao mapema baada ya kuzaliwa na kuwapatia maziwa kwa kuwakamulia.
Watoto hao lazima walazwe kwenye sehemu safi, kavu na salama, na ikiwezekana wawe mbali na mama yao. Kuwanywesha maziwa badala ya kunyonya kunahitaji ustahimilivu na muda kwa sababu lazima uwafundishe watoto namna ya kunywa maziwa hayo.
Wafugaji wengi wanawanywesha watoto maziwa ya vugu vugu kulingana na joto la mama, mara tatu au nne kwa siku.
Wiki 2 baada ya kuzaliwa, pamoja na maziwa, kianze kupewa vyakula vingine kama nyasi laini na chakula cha ziada ili kusaidia kukua kwa tumbo. Uwaachishe watoto kwa kuangalia uzito, siyo umri, na ni lazima wanapokuwa wamefikia uzito wa kilogramu 9, bila kusahau kuvipatia kinga na tiba ya magonjwa kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.
Lakini hakikisha kwamba kitoto kinapewa maji wakati wote na vyombo vinavyotumika kulishia vinakuwa safi muda wote.

Kwa maoni na ushauri, usisite kunipigia ama kuwasiliana name kwa whatsapp kupitia namba 0656-331974. Au barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.


Comments