Featured Post

MBUZI WA MAZIWA JAMII YA KINDER




MBUZI wa jamii ya Kinder ni uzao chotara baina ya jike la Nubia na dume la Pygmy. Watoto ni wadogo kwa umbo, wana nguvu na wana uwezo wa kula na kukua kwa haraka, na kuifanya jamiihiyo kuwa muafaka kwa ufugaji wa maziwa na nyama.
Mbuzi hawa wana masikio marefu ambayo yananing’inia na ngozi yake inaweza kuwa ya rangi yoyote tu. Umbo lake ni la wastani, yaani katikati ya maumbo ya Nubia na Pygmy na jike ana uzito wa kilogramu kati ya 52 na 57 wakati dume ana uzito kati ya kilogramu 61 na 68. Kimo cha jike ni sentimeta 66 wakati dume ni sentimeta 71.

Mbuzi jike jamii ya Kinder anaweza kuzalisha lita 680 za maziwa kwa mwaka zenye wastani wa asilimia 3.5 ya mafuta.
Jamii hii ya mbuzi ilipatikana mwaka 1985 kwenye Shamba la Zederkamm huko Snohomish, WA nchini Marekani baada ya kupandisha mbuzi jike wa Nubia na dume la Pygmy. Chotara huyo alipatikana kwa bahati tu, wala haikuwa kwa utafiti mkubwa. Hatua hiyo ilitokana na beberu aliyekuwemo kwenye kundi la mbuzi jamii ya Nubia kufa na kuyaacha majike mawili ya Kinubia yakiwa hayana dume.
Kwa vile akina Zederkamm walikuwa wanafuga na mbuzi jamii ya Pygmy na walikuwa na beberu lake wakaamua kulipandisha beberu hilo kwa mbuzi wa Nubia ingawa ilikuwa kazi kubwa kwa sababu beberu wa Pygmy ni mfupi kuliko jike la Nubia. Mnamo Juni 30 na Julai 4, 1986 Kinder wa kwanza watatu walizaliwa ambao walipewa majina ya Zederkamm Briar Rose, Zederkamm Liberty, na Zederkamm Tia na walikuwa majike. Ilichukua mwaka mmoja zaidi kabla ya bebeeru wa kwanza jamii ya Kinder hajazaliwa ambaye alipewa jina la Zederkamm Napoleon.
Uzuri wa mbuzi jamii ya Kinder ni kwamba, wanaweza kuzaa wakati wowote wa mwaka, sifa ambazo zimerithiwa kutoka kwa mbuzi jamii ya Pygmy. Pia wanazaa mapacha wengi kuanzia tatau hadi watano kwa mara moja, na kuna wakati waliwahi kuripotiwa kwamba walizaa mapacha sita kwa mpigo.
Maziwa ya Kinder yana kiwango kikubwa cha siagi ambacho ni wastani wa asilimia 7 na maziwa yake ni mazito kiasi kwamba yanafaa kutengeneza jibini.
Pamoja na umbo dogo, lakini mbuzi jamii ya Kinder wana minofu mingi kuliko mbuzi wa kawaida wa maziwa, ambapo wanaweza kutoa nyama kiasi cha asilimia 60 ya uzito wao wakiwa hai.

Baada ya kuzijua jamii bora za mbuzi wa maziwa, sasa tutaichambua jamii moja baada ya nyingine ili kama imetokea unataka kuwafuga, ama unawafuga tayari, uweze kuwaelewa tabia na uwezo wao pamoja na ustahimilivu wa magonjwa.
Ikiwa una maoni au ushauri, usisite kunipigia au kunitumia ujumbe wa simu au whatsapp kupitia namba 0656 331974 au nitumie barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.

Comments