Featured Post

MAONESHO YA 40 YA BIASHARA YA KIMATAIFA (SABA SABA) YAPANUA WIGO WA USHIRIKI

Ulinzi na usalama ni kipaumbele cha kwanza kwenye maonesho hayo.

Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), imekua ikiandaa maonesho haya ya biashara ya kimataifa kila mwaka. Maonesho ya 40 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam yameanza tarehe 28 Juni hadi tarehe 8 Julai, mwaka huu katika uwanja wa maonesho wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam yameendelea kuwa maonesho makubwa na yenye mafanikio katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Maonesho haya yanalenga kutekeleza kwa vitendo Sera ya Biashara ya mwaka 2003, ikiwa ni katika jitihada za kukuza biashara. Wigo wa maonesho ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam hutoa fursa mbalimbali.
Fursa hizo hutolewa kwa wazalishaji, wafanyabiashara na watoa huduma kuonesha bidhaa zao kwa ajili ya kutafuta masoko ya bidhaa hizo, kuweka mazingira ya wafanyabiashara wa nchi mbalimbali kukutana na kufahamiana kwa ajili ya kutengeneza mitandao ya kibiashara.
Kusaidia waoneshaji wa ndani kupata teknolojia za kisasa za uzalishaji, kujifunza mbinu bora za biashara, ufungashaji, kujilinganisha na wazalishaji wengine wa huduma au bidhaa zinazofanana. Vilevile, husaidia washiriki wa maonesho haya kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa wateja wao kuhusu hisia kwa bidhaa zinazooneshwa. Hali hii humsaidia mzalishaji kujumuisha mapendekezo ya wateja kwenye bidhaa husika katika uzalishaji wa toleo linalofuata, pamoja na kutoa fursa kwa wafanyabiashara kuuza bidhaa zao.
Kila mwaka kumekuwepo na kauli mbiu, kauli mbiu ya mwaka huu inafanana na ya mwaka jana ambayo inasema “Tunaunganisha uzalishaji na masoko”, yenye maana ya kuonesha umuhimu wa mnyororo wa uzalishaji ambao ndio chimbuko la upatikanaji wa bidhaa bora zenye ushindani mkubwa katika soko. Pia kubainisha uhusiano uliopo kati ya uzalishaji na masoko.
Maonesho haya ya 40 ya biashara ya kimataifa yamekuwa yenye ushiriki mkubwa kutoka mataifa mengi duniani kuliko maonesho yaliyopita. Kaimu Mkurugenzi wa TanTrade Bw. Edwin Rutageruka anasema kupitia Taasisi inayosimamia maonesho ya Biashara ya Kimataifa Duniani (UFI) ambayo TanTrade ni mwanachama wake imekua ikiyatangaza maonesho haya kwenye tovuti na kuonesha kwamba ni moja ya maonesho yanayotambukila kimataifa. Njia hii husaidia kuyatambulisha, kuyakuza pamoja na kuchangia kuvutia nchi mbalimbali duniani kuomba kushiriki.
Hali hiyo imechangia nchi nyingi zaidi kuomba kushiriki maonesho  ya 40, Bw. Rutegeruka anasema “Nchi 30 kutoka sehemu mbalimbali duniani zinashiriki katika maonesho haya, ikiwa ni ongezeko la nchi tano zaidi ya nchi zilizoshiriki maonesho haya mwaka jana”.
Kwa kuwa maonesho haya ya kila mwaka yanalenga kutoa fursa ya wafanyabiashara wa ndani kujifunza mambo ya biashara na uzalishaji bora wa bidhaa kulingana na soko la kimataifa, kutengeneza mitandao ya mawasiliano na kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani kuuza bidhaa zao, kampuni za ndani zaidi ya 600 zinashiriki maonesho haya, pamoja na wajasiriamali 2000 kutoka sehemu mbalimbali za nchi.
Mkurugenzi Mtendaji Msaidizi wa Taasisi ya kuwawezesha wanawake katika masuala ya biashara (TWCC), Bi. Mwanajuma Hamza anasema mwamko wa wanawake wajasiriamali kushiriki katika Maonesho ya Biashara ya 40 umekua mkubwa kwa vile kumekuwepo na uhamasishaji mkubwa zaidi, lakini pia kupitia maonesho haya ya kila mwaka  wanawake wengi wamefanikiwa  kupata masoko ya nje ya nchi na hivyo uchumi wao umekua.
Bi. Mwanajuma anasema Taasisi yake inayoshiriki maonesho haya kila mwaka, imekua ikiwasaidia wanawake kuwapatia taarifa za biashara za nje na mfumo kuhusu biashara za kimataifa ikiwa ni pamoja na kuanzisha majukwaa ya wanawake wafanyabiashara za kuvuka mipaka.
Aidha, anaendelea kusema kuwa kuanzia mwaka 2012 hadi sasa taasisi hiyo imesaidia wanawake wafanyabiashara zaidi ya 7000, ikiwemo vijana wa kike. Na katika maonesho haya ya 40 wameweza kuwaandalia banda maalumu la wafanyabiashara wanawake pamoja na wale wanawake wanaofanyabiashara za kuvuka mipaka ili kuonesha bidhaa zao pamoja na kupata masoko.
Doreen Chriss na Suzana Mwalongo ni wasichana wenye umri kati ya miaka 17 na 25 wanaomiliki duka la “ African flawles fashion” kutoka jijini Arusha, ambao wanauza bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa kwa kutumia vitenge na khanga kama vile mikoba, nguo na viatu ni washiriki wa maonesho ya 40 ya biashara ya kimataifa, wenye malengo ya kutanua wigo wa biashara zao na kuuza nje ya nchi.
Bi. Doreen anasema, “Kiwango hiki cha kushiriki ni cha kawaida ambacho wengi tunaweza kukimudu, pia malengo yetu ya kushiriki maonesho haya ni kuuza bidhaa zetu ndani na nje ya nchi, kwani tunaamini kuwa kupitia maonesho haya yenye kujumuisha watu wengi utoka sehemu mbalimbali duniani yatatusaidia kufikia malengo yetu.”
Anaendelea kusema kuwa anafurahi kuona watu wengi wameendelea kutembelea kwenye banda lao kwa ajili ya kuangalia na kununua bidhaa zao ambazo  zinadumu kwa muda mrefu na wanaamini watapata mafanikio kupitia maonesho haya.
Kwa upande  wa Taasisi za Serikali, umekuwepo ushiriki mzuri wa taasisi hizo pamoja na Wizara katika kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati. Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeongeza uwezo wake wa kushiriki katika   maonesho ya mwaka huu kwa kuzishirikisha kwa kiasi kikubwa taasisi zilizo chini yake kama SIDO, TFDA, CBE, TBS na BRELA.
Wizara imefikia azma hiyo kwa kuona kuwa wananchi hasa wenye nia ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo wamekuwa wakihitaji taarifa zaidi kuhusu masula ya biashara na viwanda.
Afisa Biashara wa Wizara hiyo Bw. Baruti Mwaigaga, anasema maonesho ya mwaka huu yamekuwa ya tofauti na yenye hamasa kubwa kwa vile wananchi wengi wenye viwanda na wenye nia ya kuanzisha viwanda nchini wamekua wakitembelea banda la Wizara kwa ajili ya kupata maelezo jinsi gani ya kupata mikopo ya kuanzisha viwanda pamoja na kuunganishwa na masoko ya bidhaa za kilimo.
Aidha, Bw. Mwaigaga anasema Wizara imendaa programu za kuendeleza viwanda vidogo vidogo nchini kwa kuanzia mikoa ya Iringa, Pwani, Tanga, Ruvuma na Manyara, na kusisitiza upatikanaji wa masoko ya ndani kwa zao la ufuta, huku akiwataka wananchi kwa ujumla kutembelea kwa wingi banda hilo ili kupata taarifa zinazoweza kuwasaidia katika masuala ya uzalishaji na masoko.
Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa yamefunguliwa rasmi na Rais wa Serikali ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame tarehe 1 Julai 2016 ambapo ametoa wito kwa washiriki wa maonesho  hayo kushirikiana ili kubuni mawazo mapya ya biashara ikiwa ni pamoja na  kutambua fursa zilizopo katika soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, katika kukuza biashara zao na kusaidia ukuaji wa uchumi wa pamoja katika nchi wanachama wa  Jumuiya hiyo.
Baada ya kufungua maonesho hayo, Rais Kagame alikabidhi tuzo kwa Wizara, taasisi za Serikali, makampuni, nchi washiriki pamoja na mashirika yaliyoshinda katika maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa, kwa kushinda kwa kuonesha bidhaa bora na kueleza huduma nzuri wanazotoa.
Ni imani yangu kuwa maandalizi ya maonesho ya 41 yataanza mara tu baada ya kumalizika kwa maonesho haya, lengo likiwa kushirikisha makampuni mengi, wajasiriamali wengi na nchi nyingi zaidi.
Tafsiri yake ni kwamba hali hiyo itasababisha wafanyabiashara wa ndani kutambulika nje ya mipaka ya nchi kwa kiasi kikubwa, kupata ujuzi wa kutengeneza bidhaa mbalimbali na vile vile kupata soko kubwa kwa ajili ya kuuza bidhaa zao.
Wito wangu kwa waandaaji wa maonesho haya, ni vyema wakatafuta namna  ya kuandaa maonesho kama  haya katika ngazi za shule za sekondari na vyuo vikuu nchini, ili kuchochea ubunifu pamoja na kutengeneza mazingira ya kujiajiri kwa vijana wanaomaliza shule na vyuo kila mwaka.
Jambo hili litasaidia watoto na vijana kupunguza kujiingiza katika makundi na tabia zisizofaa, litakuza vipaji na ubunifu kwa watoto na vijana, kuongeza idadi ya viwanda vidogo nchini ikiwa ni pamoja na kuzalisha ajira na kukuza uchumi wa Taifa letu.

Comments