Featured Post

AKINAMAMA KIJIJI CHA KITANGA KUZALISHA BIDHAA 300 ZA MUHOGO



Baadhi ya bidhaa zinazozalishwa kutokana na unga wa muhogo. Hii ni kazi nzuri ya kikundi cha akinamama wa Kitanga Green Voices katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe.
Mchanganyiko wa mihogo, maharagwe, mboga za majani na nyama. Ni chakula kizuri sana hiki chenye aina nyingi za vitamin, wanga na protini.

PENGINE unafahamu faida tatu au nne tu za muhogo ambazo ni kuutafuna mbichi, kuuchemsha au kuuchoma; unga wake kwa ajili ya lishe, majani yake kama mboga ya kisamvu na dawa pamoja na miti yake inapokauka kutumika kama kuni.
Inawezekana hujui kama maganda ya mihogo baada ya kumenywa ni chakula bora cha mifugo yakikaushwa au mabichi.
Siyo ajabu pia hufahamu kwamba muhogo ukitwangwa mbichi na kuchujwa, maji yake yake yanatoa wanga (starch) ambao hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi za awali za ukuta na sukari (sugar syrup) na pia ni lishe nzuri.

Lakini zao la muhogo ni zaidi ya linavyofikiriwa kwa sababu licha ya faida hizo chache, lakini pia linazalisha bidhaa zaidi ya 300 kama ambavyo akinamama wa Kijiji cha Kitanga, Kata ya Msimbu wilayani Kisarawe wameamua kufanya.
Akinamama hao kupitia kikundi chao cha Kisanga Green Voices mbali ya kuzalisha unga pamoja na chips, sasa wanatengeneza bidhaa lukuki zenye ubora kama chapati, maandazi, skonzi, biskuti, tambi, cassava chop, na nyinginezo nyingi.
Hatua hiyo imekuja baada ya kupatiwa mafunzo kupitia mradi wa Green Voices unaofadhiliwa na taasisi ya maendeleo ya wanawake wa Afrika inayojulikana kama Women for Africa Foundation, ambayo iko chini ya Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega.

Baadhi ya akinamama wa Kitanga Green Voices wakiwa wameushikilia muhogo pamoja na viongozi wa kijiji na Kata ya Msimbu wilayani Kisarawe.
Kijana akiwa amebeba muhogo baada ya kuchimba shambani.

Kuanzishwa kwa mradi huo wa kusindika muhogo pamoja na bidhaa zake kumeliokoa zao hilo ambalo licha ya kuwa na manufaa makubwa kwa jamii, lakini limekuwa likidorora hata katika soko la vyakula.
“Tangu tumeanzisha kikundi hiki miezi mitatu iliyopita hivi sasa muhogo hauwezi kuozea shambani na wananchi wanaona umuhimu wa zao hilo,” anasema Mama Abia Magembe, ambaye ni mratibu wa mradi huo.
Mama Magembe, ambaye yeyé pamoja na akinamama wengine tisa walipatiwa mafunzo nchini Hispania kwa nia ya kuanzisha shughuli za ujasiriamali unaoendana na utunzaji wa mazingira pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabianchi, anasema kwamba zao la muhogo sasa limepata thamani kubwa kijijini hapo na wana uhakika wakulima wa wilaya ya Kisarawe wanaweza kugeukia miradi kama hiyo ili kuongeza mnyororo wa thamani.
Akinamama 10 wanaofanya miradi mbalimbali ya ujasirimali kupitia mradi wa Green Voices wanatoka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro, Pwani na Mwanza.
Silvera Mujuni, Ofisa Chakula na Lishe wa Wilaya ya Kisarawe, anasema kwamba wilaya hiyo ina fursa kubwa ya kusindika na kuchakata mazao mengi yatokanayo na muhogo kwa kuwa zao hilo ndilo kuu kwa chakula na biashara.
Anasema kwamba, ardhi katika vijijini vingi vya wilaya hiyo inastawisha muhogo kwa wingi, hivyo ikiwa wananchi watajizatiti na kujifunza namna ya kuchakata bidhaa za muhogo wanaweza kupata faida kubwa kiuchumi.
“Muhogo ndilo zao kuu katika maeneo mengi ya wilaya hii ambayo haiwezi kustawisha mazao mengine kama mahindi, hivyo ni vyema wananchi wakajifunza utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao hilo,” anasema Bi. Silvera aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Wilaya hiyo na ambaye ndiye alikuwa akiwafundisha akinamama hao namna ya kutengeneza bidhaa mbalimbali.

Diwani wa Kata ya Msimbu, Amina Lilomo, akizungumza na akinamama wa kikundi cha Kitanga Green Voices wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika Kijiji cha Kitanga hivi karibuni.
Mshiriki kiongozi wa Kitanga Green Voices Women Group, Mama Abia Magembe, akiwahamasisha wanawake wenzake katika uzinduzi huo.

Awali Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Wazir Yakoub Wazir, aliwataka akinamama hao wajipange wasajiliwe rasmi ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na serikali na taasisi nyingine za binafsi.
“Ofisi yangu iko wazi wakati wote, mkitaka kwenda kusajiliwa wilayani hata leo niko tayari kuwasaidia, nawaombeni mje niwasaidie hata namna ya kuandaa katiba ya kikundi pamoja na taratibu nyingine,” alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Msimbu, Anna Lilomo, amesema atajitahidi – kwa kushirikiana na diwani mwenzake wa viti maalum Mossy Sultan Kufurumbaya – kuwapigania akinamama hao kwenye vikao vya Baraza la Madiwani ili waweze kupatiwa misaada na mikopo hata kupitia katika asilimia 10 ya bajeti ya halmashauri ambayo hulenga kuwasaidia wanawake na vijana.
“Bahati nzuri sisi hapa ni madiwani wanawake, kwa hiyo tutalipeleka suala la akinamama hawa kwenye Baraza la Madiwani na kuelezea umuhimu wa kuongeza thamani kwenye zao letu la muhogo ili limkomboe mkulima,” alisema Diwani Lilomo.
Mratibu wa Mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, anasema kwamba anafarijika anapoona wanawake wakihamasika kushiriki shughuli za maendeleo, hasa ujasiriamali unaolenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
“Suala la kuhakikisha uhakika wa chakula, kutokomeza umaskini, kuwawezesha wanawake kiuchumi na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni mambo yaliyopewa kipaumbele katika Malengo Endelevu ya Dunia, hivyo wanawake wanaotekeleza miradi ya Green Voices wanayatekeleza malengo hayo kwa wakati mmoja,” anasema Secelela.

Diwani wa Kata ya Msimbu wilayani Kisarawe, Amina Lilomo (kushoto) na Diwani wa Viti Maalum, Mossy Sultan Kufurumbaya, wakiwa makini kusikiliza maelezo kuhusu namna ya kusindika bidhaa mbalimbali kutokana na zao la muhogo.
Akinamama wa Kitanga Green Voices wakiwa katika picha ya pamoja na mwandishi Tukuswiga Mwaisumbe (kilemba cha njano).

Muhogo ni zao linalochukuliwa na wengi kama la ziada hasa kwenye ukame, lakini wengi hulifanya kama mlo wa hamu bila kutambua kwamba zao hilo lina manufaa makubwa kwa lishe na kibiashara.
Wengi wanauchukulia muhogo kama chakula cha maskini, hawa wale wanaojitiahidi kulima zao hilo, huyapa kipaumbele mazao mengine kuliko muhogo.
Lakini muhogo ni zao mojawapo ambalo linaweza kuiepusha jamii na baa la njaa huku katika baadhi ya mataifa likitumika kama chanzo cha nishati ili kukabiliana na bei ya mafuta na nishati nyinginezo.
Baa la njaa ni tatizo kubwa linalozikumba nchi nyingi barani Afrika, Tanzania ikiwa miongoni mwazo, lakini licha ya watu kuhimizwa kulima muhogo, bado wanalipuuza zao hilo na kuliona kama zao fulani la mizizi tu.
Katika mikoa kama Lindi na Mtwara ambayo kwa miaka mingi inalima kwa wingi muhogo, chakula chao kikuu kilikuwa ugali wa muhogo.
Licha ya kudharauliwa kwa zao hilo, lakini siyo ajabu ukakuta mlo wa siku hiyo umetokana na muhogo kasoro chumvi na nazi, kwani inawezekana kuni zilizopikia ni matawi ya muhogo, ugali wa muhogo na kisamvu cha muhogo!
Na wakulima wengi katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara wanakula ugali wa muhogo pale wanapokosa unga wa mahindi, ambapo wanaokula ugali huo wa muhogo (Wazaramo wanasema ‘bada’ na Wamakua wanauita ‘matamba’) huonekana maskini wa kutupa.
Leo hii wanapohamasishwa kulima muhogo kwa sababu ya kustahimili ukame, bado wengi wanasuasua, lakini watakapoambiwa kwamba unga wa muhogo unatoa bidhaa nyingi zenye faida kubwa, huenda wengi wakaligeukia zao hilo na kulima kibiashara.
Inafurahisha sana siku hizi kuona watu wengi wakikimbilia ugali wa muhogo hata hotelini, lakini hiyo bado haijatosha kulirasimisha zao hilo ili liwe na tija kubwa.
Akinamama wa Kijiji cha Kitanga wanaweza kuwa mabalozi wazuri wa zao hilo, kwa sababu tayari wameanza kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo hata wananchi wa kijiji hicho wameshangazwa nazo baada ya kuzionja na kuona ubora wake.
Kilimo cha muhogo siyo tu kitasaidia kukuza pato la mkulima, lakini kinaweza pia kuokoa mazingira pamoja na kuisaidia Tanzania kuokoa karibu Dola za Marekani 20 milioni sawa na Shs. 42 bilioni zinazotumika kuagiza chakula nje, jukumu ambalo kikundi cha Kitanga Green Voices kimeamua kulibeba.

Mashine hizi ndizo zinazotumika kuuponda muhogo na kuucharanga kama chips. Kila kijiji kikiwa nazo kinaweza kutengeneza unga bora wa muhogo ambao utazalisha bidhaa mbalimbali.
Mihogo ikiwa imeandaliwa tayari kwa kuchakatwa kwenye mashine. 



Faida za muhogo ni nyingi kama zilivyoelezwa hapo juu, lakini kwa msisitizo ni kwamba, unga wake hutumika kutengeneza vyakula mbalimbali, baadhi ni uji na ugali, vitafunwa kama keki, mikate, skonzi, biskuiti, mandazi, mafuta ya lishe, sabuni ya unga, kuni, mboga, huksi pamoja na bidhaa nyingine nyingi
Mazao yanayopatikana katika mzizi wenyewe, miti na majani huweza kuzalisha bidhaa anuwai za viwandani kama vifaa vya nguo, karatasi, mafuta, kilevi, dawa za binadamu na plastiki wakati ambapo wanga hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi za awali za ukuta na sukari (sugar syrup).
Takwimu za kilimo cha muhogo duniani zinaonyesha kuwa, Afrika ni bara la tatu duniani kwa kuzalisha zaidi muhogo ambapo huzalishaji takriban tani milioni 102.6 kila mwaka.
Tanzania ni nchi ya nne kati ya wazalishaji wakubwa wa muhogo barani Afrika baada ya Nigeria, Ghana na Kongo DRC ambapo inaelezwa kwamba karibu ekari 670,000 za ardhi ya kilimo zinatumika kuzalisha muhogo, zao linalochangia karibu asilimia 15 za chakula kwa nchi nzima ambapo karibu kaya 1,213,958 huzalisha muhogo nchini.
Mikoa inayozalisha muhogo kwa wingi ni Mwanza, Mtwara, Lindi, Shinyanga, Tanga, Ruvuma, Mara, Kigoma, Pwani na maeneo yote ya Zanzibar. Ukanda wa Ziwa ni wazalishaji wakubwa zaidi ikifuatiwa na ukanda wa kusini. Mkoa wa Ruvuma huzalisha kati ya 5-10% ya uzalishaji wote Tanzania. 
Muhogo ndilo zao la pili kwa kuchangia pato la taifa kwa asilimia 19 baada ya  mahindi.
Taarifa ya Shirika la Utafiti wa Viwanda na Maendeleo ya Mazao ya Chakula Tanzania (TIRDO) inaonyesha kuwa zao la muhogo linastawi kirahisi.
Hii ni pamoja na kuvumilia ukame na halishambuliwi na magonjwa au wadudu wanaoathiri mazao mengine na pia muhogo unaweza kutoa mazao mengi katika ardhi duni ambayo mazao kama mahindi hayawezi kustawi.
Kwa mujibu wa TIRDO, muhogo ni zao la pili kuwa na wanga mwingi baada ya viazi vitamu ambavyo vina asilimia 20 hadi 30 ya wanga na kwamba asilimia 84 ya zao hilo hutumika kama chakula cha binadamu.

Comments