Featured Post

TAZAMA PICHA MBALIMBALI ALIZOPIGA CHARLES KITWANGA NA MADIWANI WA MISUNGWI BAADA YA KUTOKA BUNGENI!



Waziri Charles Kitwanga (nyuma kabisa) mara baada ya kutoka Bungeni alipiga picha hizi pamoja na wabunge na madiwani kabla ya kwenda Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na kwingineko.


                                      
 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
                                                            23/05/2016.
Napenda kuwasalimu wote na kushukuru kwa kujaliwa na uzima.
Ndugu wanahabari tumewaiteni hapa kuja kuwaelezeni ukweli uliojificha kuhusu kitendo klichopelekea Mh. Rais Dk. John Pombe Magufuli kutengua uteuzi wa  Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga.
Kama mnakumbuka kuwa Rais alichukuwa uamuzi huo Ijumaa ya Mei 20 mwaka huu kwa kwa kosa la kwamba Kitwanga aliingia bungeni akiwa amelewa.
Sisi wananchi wa Jimbo la Misungwi tumesikitishwa na taarifa hiyo ambayo imemkuta kiongozi wetu na Mbunge wetu kwa kuvuliwa hiyo nafasi kwa sababu nyepesi zenye uongo mwingi wenye lengo la kumchonganisha na Rais Magufuli ili kufanikisha lengo la waovu ambao  wamebanwa na Serikali hii ya Awamu ya tano kupitia wizara hiyo nyeti kwa usalama wa nchi.
 Miongoni mwetu tulikuwa mjini Dodoma kwa kuungana na madiwani wa Jimbo la Misungwi ambao walikwenda kumtembelea bungeni, tulizungumza mengi kwa ajli ya jimbo letu na katika kikao chetu hapakuwa na chembe ya kilevi chochote na hata kesho yake alipoinga bungeni alikuwa mzima wa afya ya kimwili na akili timamu na tunawahakikishieni kuwa Kitwanga hakuwa amelewa.
 Ndugu waandishi wa habari asubuhi ya tarehe 20 tulielekea bungeni kwa mwaliko wa Charles Kitwanga, tukiwa sehemu ya mualiko uliowajumuisha Madiwani wa jimbo lake tukiwa tumeambatana naye tukaingia ndani ya ukumbi wa bunge,tukashuhudia anajibu swali,baada ya kujibu swali la mbunge Sakaya,tulitoka nje na kupiga picha na madiwani wote wa Misungwi waliokuja kumtembelea Dodoma.
Baada ya zoezi la kupiga picha kukamilika pale nje ya ukumbi wa Bunge, tulitoka na kuelekea Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa lengo la  kututembeza maeneo yote ya Dodoma , lakini ilipofika jioni wakati tukirejea nyumbani tukiwa naye, ghafla tukaona habari zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Waziri Kitwanga amevuliwa uongozi kwa kuwa alionekana na Waziri Mkuu akiwa amelewa.
Tukiwa na madiwani wa CCM wa Misungwi, tunasema hizo ni habari za kupikwa na ambazo zililenga kumchafua mbunge huyo ambaye alikuwa anaongoza huku akiwa na maadui wengi ndani ya serikali,CCM na nje ya CCM wakiwemo mtandao wa dawa za kulevya,walioachishwa kazi NIDA,pamoja na Uhamiaji walikuja dodoma kuhakikisha hilo la kuondolewa Kitwanga linafanikiwa.
Ndugu wanahabari , tulishangazwa wote kwani  tulikuwa tumekaa naye pale nyumbani kwake Sengia Dodoma (site 2) tukipata chakula cha usiku ,alionekana kutoaamini na hata madiwani pia na wengine ambao tulikuwepo hapa nyumbani kwake tukipata chakula hawakuamini.
Tunachosema ni kwamba waziri Kitwanga hakulewa kama ambavyo imetafsiri sababu ya kumvua uongozi,bali alikuwa anatafutwa ili kufanikisha lengo ambalo limefanikiwa.Mtandao wa dawa za kulevya,pamoja na wale waliokuwa wanamshutumu kwamba amehusika kuondolewa kwao kazini wakiwemo Watu wa NIDA, Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Mfanyabiashara Said Lugumi pamoja  na kundi  mafisadi waliokwapua mabilioni ya fedha  NSSF. Pia na baadhi ya wabunge wa CCM na Upinzani ambao walikuwa hawafurahishwi na kasi ya utendaji kazi wa Kitwanga katika Wizara ya Mambo ya ndani.
Kwa niaba ya wananchi wenzetu tunamtahadharisha Mhe. Rais awe makini na makundi la wafanyabiashara wa madawa ya kulevya, pamoja na lile kundi la wanamtandao masalia ndani ya  CCM na serikalini na kwenye vyombo nyeti vya ulinzi na usalama, ambayo kwa ujumla yalikuwa na mkakati kabambe wa kuhakikisha wanamtenganisha na Rais.
Ndugu waandishi wa habari, kilichotushangaza zaidi baada tu ya Kitwanga kuvuliwa madaraka yake ya uwaziri, kuna watu walianza kufanya sherehe wakishangilia hususani wale waliovuliwa madaraka NIDA pamoja na NSSF,Uhamiaji na wale wanaotuhumiwa kuhusika na madawa ya kulevya.
Ndugu waandishi wa habari, tunajua namna kundi la Said Lugumi,Ridhiwani Kikwete na kampuni yao walivyokuwa wanadhamini  kwa mbinu za kifedha  katika vita hii ya kitwanga ili aondolewe, lakini baada ya kuondolewa, wakajifanya kutoa taarifa ya kushangazwa kuondolewa kwake,
Kitwanga amekuwa mtumishi wa serikali akiwa mtumishi mwaandamizi benki kuu Tanzania (BOT),amekuwa mbunge na Naibu waziri kwa miaka 10,lakini hata siku moja hakuwahi kuonekana amelewa.
                                
MAAZIMIO YETU
=Tunaliomba Bunge kumuomba radhi Mhe. Charles Kitwanga kwa kumdharirisha mbele ya wapiga kura wake wa Jimbo la Misungwi familia yake pamoja na watanzania wote waliokuwa wanaamini utendaji wake kupitia video iliyochezewa na wataalamu wa IT katika studio za Bunge ili kufanikisha lengo la kumuonyesha Kitwanga kuwa alikuwa amelewa bungeni.
=Tunamuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye ndiye Kiongozi Mkuu wa Serikali bungeni atoe uthibitisho wa kikemia unaotanabaisha wazi kama   Kitwanga alikuwa katumia kilevi wakati akiwa bungeni.

=Tunaliomba Bunge lifanye uchunguzi na kubaini wale wote walisambaza ile video inayoonyesha Kitwanga akiwa anaongea na kuonekana amelewa wakati kiuhalisia hakulewa na alijibu maswali yote vizuri
=Tunaliomba Bunge kuchunguza idara ya habari ya Bunge pamoja na studio ile ya Bunge ambao wamehusika na kuhariri ile picha ya video iliyokuwa inasambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
=Tunahoji uhalali wa kumvua mtu madaraka kwa sababu ya ulevi bila uthibitisho wa daktari ambaye kisheria ndiye mwenye mamlaka hayo kugundua kilevi cha mtu.
= Tunaomba Watanzania wote waliosikitishwa na taarifa hizi wajue tu kwamba ile video ambayo imemtia hatiani Kitwanga ilihaririwa kwa ustadi mkubwa kupitia wafanyakazi wa Bunge ambao wanapitia zile asadi za bunge pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa serikali kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ambao hawakupenda kitwanga aendelee kuwa pale ,kwa nia ya kumhujumu na sasa wanasema kwenye vyombo vya habari ili kuhalalisha uhujumu huo.
=Tunaomba mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) kuangalia picha zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya Mhe Mbunge wa Misungwi ambazo zinaonekana kumchafua wachukue hatua dhidi ya watu hao kwani kisiasa zinaendelea kumchafua na kumharibia kwa wapigakura wake,familia yake,mama yake mzazi ,ndugu zake .
=Tunajiandaa kuchukua hatua kwa Bunge za kisheria kama watashindwa kuthibitisha tuhuma hizo dhidi ya Charles Kitwanga ambazo tunaamini zimetengenezwa kwa maslahi ya makundi yanayompinga ndani ya Serikali wakiwemo mtandao wa dawa za kulevya.
Pia tunamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa makini kundi la wanamtandao walio ndani ya serikali ambalo linaongozwa wahafidhina wasio taka mabadiliko ndani ya serikali.

Imeandaliwa na Madiwani wa Jimbo la Misungwi pamoja na wakereketwa wa jimbo hilo
Baraka Kingamkono, Gaudency Tungaraza na IDDY Majumuisho.

                          Asanteni na Mungu awabariki.


   

Comments