Featured Post

JUHUDI ZIKIONGEZWA KATIKA MAPAMBANO, MALARIA YAWEZA KUTOKOMEA TANZANIA

Dk. Robert Malima akitoa maelezo ya namna watafiti wanavyofanya utafiti na kuwakusanya mbu katika chumba maalum cha kufanyia utafiti kwa waandishi wa habari kutoka Kituo cha Waandishi wa Habari wa Kimataifa (ICFJ) na Taasisi ya “Malaria No More” kutoka nchini Marekani walipotembelea Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) cha Amani mkoani Tanga kujionea namna Tanzania inavyopambana na ugonjwa huo.
Watafiti wakiweka vitambaa vyenye viatilifu kwenye nyumba. Kitambaa hiki hudumu Kwa miaka 3 hadi 4 vikifanya kazi ya kuuwa mbu.
(PICHA NA ELEUTERI MANGI-MAELEZO)
 
 
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO

“SAFARI moja huanzisha nyingine” na “Safari ni hatua”, hii ni misemo inayoonesha ili kufika hatua fulani katika maisha ni lazima kuanza na hatua ya moja inayopelekea hatua nyingine kufuata na kundelea hadi utakapofikia malengo uliyojiwekea.
Juhudi za kufikia malengo haijalishi zinanzia wapi, kwani kila mtu anakipaji ambacho ni tofauti na cha mwengine, lengo ni kupambana na changamoto zinazoikabili jamii na kuzipatia majawabu.
Kulingana na historia, neno adui si geni kwa Tanzania kwani Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema miongoni mwa maadui wanaolikabili taifa aliloliongoza ni magonjwa.
Tanzania ikiwa miongoni mwa mataifa ya dunia hii na taifa lililo kusini mwa Jangwa la Sahara, halikwepi magonjwa abayo husababishwa na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo malaria.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za Shirika la Afya Duniani (WHO) malaria ni ugonjwa hatari unayosababisha vifo vya watu wengi duniani na unawaathiri akinamama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Ndiyo maana Wataamu wa masuala ya afya wanasisitiza kuwa kila mtu anatakiwa kuchua tahadhari ili kupunguza idadi ya vifo vinavyoweza kuzuilika kwa kufuata kanuni za afya na maelekezo ya kitabibu kama yalivyotolewa na watoa huduma ya afya.
Ili kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa la mfano duniani katika kupambana na adui malaria wataalamu wa afya nchini wanaendelea kunoa vichwa vyao kuhaikikisha wanapunguza au kumaliza tatizo la malaria linaloathiri watu wa rika zote ambao ni nguvu kazi ya taifa la sasa na lijalo.
Hadi sasa Tanzania imefanikiwa kuanza kufanya majaribio na kuwa nchi ya kwanza duniani kupambana na mbu waenezao magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria kwa kutumia kitambaa kilichowekewa viatilifu ili kudhibiti mbu waenezao ugonjwa malaria ambao ni tishio kwa afya ya wananchi wengi wanaoishi vijijini.
Hatua hiyo ya utafiti imefikiwa na watafiti wa magonjwa ya Binadamu katika kituo cha Taifa cha Magojwa ya Binadamu (NIMR) cha Amani mkoani Tanga hatua ambayo imeanza kuonesha matunda kwa kuweza kuwadhibiti mbu waenezao ugonjwa huo.
Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) cha Amani mkoani Tanga Dkt. William Kisinza aliwadhihirishia  Waandishi wa Habari wa Kimataifa (ICFJ) na Taasisi ya “Malaria No More” kutoka nchini Marekani walipotembelea kituo hicho hivi karibuni na kuwadhihirishia kuwa hatua hiyo iliyofikiwa na watafiti hao inaridhisha na inaendelea vizuri katika kupambana na ugonjwa huo.
Katika kufanikisha majaribio hayo, Dkt. Kisinza aliwaambia waandishi hao wa habari kuwa kituo hicho kinaendelea vizuri na majaribio ambapo wanatarajia kufanya mchanganuo wa utafiti huo mwishoni mwa mwaka 2016 na taarifa kamili itatolewa rasmi mwaka 2017 ili viatilifu hivyo viweze kutumika nchi nzima hatua itakayosaidia kuwapunguzia adha Watanzania ili waweze kutumia muda mwingi kuzalisha mali badala ya kutumia muda mwingi kuhudumia wagonjwa wa malaria.
Tanzania likiwa taifa linalojali masuala ya ushirikiano na mataifa au taasisi nyingine duniani na kuthamini nafasi ya washirika hao, inapelekea kuamini kuwa taifa haliwezi kusonga mbele peke yake, juhudi za mataifa na taasisi nyingine zinahitajika katika kufikia mafanikio hayo.
Ndio maana waswahili husema “Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu”, hiyo haikuwa shida kwa NIMR, Dkt. Kisinza anasema kuwa mafanikio ya taasisi yake yanayohusisha majaribio hayo ya kudhibiti mbu waenezao nmalaria yanatokana na ushirikiano mzuri uliopo na taasisi nyingine za kitaaluma ndani na nje ya nchi.
Miongoni mwa taasisi hizo ni Chuo Kikuu cha Afya cha Kilimanjaro (KCMC), Kituo cha Kudhibiti Kuzuia na Magonjwa cha Marekani (CDC), Taasisi ya Tiba, Dawa na usafi wa mazingira ya London nchini Uingereza (LSHTM) na Chuo Kikuu cha Brandeis cha nchini Marekani.
Juhudi za Serikali kupitia tasisi ya Amani na washrika zimekuwa ni nyota njema inayosaidia kupelekea mafanikio ya kupunguza maambukizi ya malaria nchini.
Takwimu zinaonesha kuwa malaria bado ni tatizo kubwa nchini katika maeneo ya vijijini ikilinganishwa na maeneo ya mjini ambapo maambukizi maeneo ya vijijini ni asilimia 10.7 na mjini ni asilimia 3.4
Tofauti hiyo inaonesha kuwa maambukizi ya malaria yamepungua kwa asilimia 50 kutoka asilimia 18 mwaka 2007/2008 hadi asilimia 10 mwaka 2011/2012.
Katika kuonesha Serikali ipo mstari wa mbele katika kupambana na adui malaria, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alipokuwa akitoa tamko wakati wa kilele cha Siku ya Malaria Duniani mjini Dodoma Aprili 25 mwaka huu alisema kuwa Tanzania inafanya kila juhudi kuhakikisha maambukizi ya malaria yanapungua hadi asilimia 5 mwaka 2016 na asilimia 1 ifikapo mwaka 2020.
Kituo cha Utafiti cha Amani mkoani Tanga kimeanza kwa vitendo kuonesha matumaini hayo na kuunga mkono juhudi za Serikali ambapo Mtafiti Mkuu anayesimamia zoezi la majaribio ya kuweka vitambaa vyenye viatilifu vijulikanavyo kama “insecticide treated wall liners”, Dkt. Joseph Mugasa amesisitiza kuwa zoezi hilo linahusisha vijiji 44 ambapo kaya zaidi ya 25,000 zipo kwenye mradi na idadi ya watu wanaonufaika na majaribio hayo ni zaidi ya 100,000 katika maeneo mbalimbali ndani ya wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Mbali na kuangalia uwezo wa vitambaa hivyo, mradi huo unaangalia pia uwezo wa vitambaa hivyo katika kukabiliana na upugufu wa damu kwa watoto chini ya miaka 11, uwezo wa vitambaa kupambana na mbu sugu kwenye viatilifu vingine na pia kufanya tathmini ya gharama anazoingia mwananchi katika kugharamikia tiba za malaria.
Ili kupambana na mbu waenezao malaria katika makazi ya watu, Kitambaa hicho huwekwa kwenye kuta za nyumba kwa ndani kitatumika sambamba na chandarua ili kuweza kutoa kinga madhubuti mara mbili kumkinga binadamu dhidi ya mbu waenezao magonjwa.
Mradi huo wa majaribio ya kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini umeanza kufanyiwa utafiti nchini miaka mtatu iliyopita kuanzia 2013 na unafadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) chini ya Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Malaria (PMI) ambao hadi kukamilika kwake utarajiwa kugharibu zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 3.
Meneja wa Mawasiliano Taasisi ya “Malaria No More” ya nchini Marekani Dena Gudaitis ambaye pia alikuwa Mkuu wa msafara wa waandishi hao waliokuja Tanzania waliofanya ziara kujionea namna Tanzania inavyopambana na malaria kuanzia Mei 9 hadi 13 mwaka huu amesema kuwa Tanzania imeonesha nia ya dhati katika kusimamia afya za wananchi wake hasa wale wa kipato cha chini ambao wengi wao wanaishi vijijini.
Aidha, Rais Mstaafu Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete ambaye ni mshindi wa tuzo ya “White House Summit Award” aliyoipata mwezi Aprili mwaka huu inaudhihirishia Ulimwengu akiwa madarakani alitumia hekima na busara katika mapambano dhidi ya malaria kupitia kampeni mbalimbali ikiwemo “Zinduka Maleria haikubaliki” aliyoizindua February 13, 2010 zilionesha ujasiri wake wa kupambana na ugonjwa wa malaria nchini.  
Ni dhahiri tuzo hiyo aliyopewa Dkt. Kikwete imetokana na kutambua jitihada na kuthamini mchango wake ambao yeye ni miongoni mwa waasisi walioasimamia uanzishwaji wa Muungano wa Viongozi wa Afrika katika mapambano dhidi ya malaria (ALMA), muungano ambao hadi sasa una viongozi 49.
Hatua ya iliyofikiwa na Tanzania kupitia kituo cha Amani kufanya majaribio ya utafiti katika ugonjwa wa malaria unaakisi taswira ya hatua mbalimbali zinazoendelea duniani ambapo uhalisia unaonesha kuwa idadi ya watu waliokufa kwa ugonjwa wa Malaria kimeshuka chini ya nusu milioni mnamo mwaka uliopita.
Hatua hiyo inaonesha mafanikio makubwa yanayofikiwa na nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara dhidi ya ugonjwa huo unaoenezwa na mbu.
Ripoti mpya ya Shirika la Afya Ulimwenguni inaonyesha kuwa vifo vilivyotokana na ugonjwa wa Malaria vimeshuka hadi 438,000 mnamo mwaka 2015, ikiwa ni idadi ndogo ikilinganishwa na mwaka 2000, ambapo watu 839,000 waliuawa na Malaria.
Aidha, WHO inaeleza katika ripoti yake kuwa katika muda wa miaka 14 iliyopita, mikakati ya kupambana na ugonjwa huo katika nchi nyingi za Afrika, ikiwemo matumizi ya vyandarua wakati wa kulala na kupuliza dawa ya kuuwa wadudu nje na ndani ya nyumba imeokoa mamilioni ya maisha ya watu na fedha nyingi ambazo zinaweza kutumiwa kuwatibu wagonjwa wengine.
Ni dhahiri zaidi ya asilimia 35 ya vifo vyote vinavyotokana na Malaria ulimwenguni vinatokea katika nchi mbili za Kiafrika ambazo ni Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hatua hiyo imepelekea Shirika la Afya Ulimwenguni kujiridhisha kuwa katika mwaka wa 2013, zaidi ya watu milioni 198, waliambukizwa ugonjwa wa malaria na ambapo imekadiriwa watu 584,000 walikufa kutokana na ugonjwa huo.
Taswira hiyo inaonesha karibu watu 4 kati ya 5 waliokufa ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Ugonjwa huo unatishia mamia ya nchi na maeneo mbalimbali ulimwenguni, na watu bilioni 3.2 wanakabili hatari ya kuambukizwa.
Tanzania ikiwa mojawapo ya nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, imejiwekea mikakati ya kuudhibiti ugonjwa huo inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Mikakati hiyo ni kutumia viandarua vyenye viatilifu vya muda mrefu, kusafisha mazingira na kuua viluwiluwi vya mbu kwa kutumia viuadudu vya kibailojia katika maeneo ya mijini, unyunyiziaji wa viatilifu ukoko katika kuta za ndani ya nyumbaambao unatekelezwa katika baadhi ya wilaya za mikoa ya Kanda ya Ziwa zenye maambukizi makubwa ya malaria.
Zoezo hilo la dawa ya ukoko limefanyika katika halmashauri nane za mikoa ya Musoma, Butiama, Ngara, Misenyi, Kwimba, Bukoba Vijijini Chato na Sengerema ambapo jumla ya kaya 459,212 zimepuliziwa viatilifu hivyo na kukinga takribani jumla ya wakazi 2,296,260.
Mikakati mingine ni kuendelea na uchunguzi na kutoa matibabu ya ugonjwa wa malaria mara unapogunduliwa kwa wagonjwa, kuongeza kasi ya upimaji kwa kutumia kipimo kinachotoa majibu haraka (MRDT) ndani ya dakika 15 au kwa kutumia hadubini na kutumia dawa sahihi kulingana na maelekezo ya daktari na mtoa huduma.
Hatua hiyo ya kuboresha vipimo kwa kutumia MRDT Mtaalamu wa Maabara kutoka Zahanati ya Ithna-Asheri iliyopo jijini Arusha Apolinary Mushi anasema kuwa ni kizuri na kinaweza kutumiwa katika mazingira yeyote nchini mijini na vijijini.
Kwa mujibu wa tamko la Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alilolitoa mjini Dodoma wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya malaria duniani, Serikali inaendelea kuwapatia utaalamu wataalamu ili waweze kujengewa uwezo na weledi katika kutekeleza majukumu kulingana na taaluma yao.
Hatua hiyo ya Serikali itaendelea kusaidia kuboresha ongezeko la upimaji wa malaria nchini kufikia asilimia 83 ambapo kiwango hicho cha upimaji kinazidi lengo ambalo Serikali imejiwekea la angalau asilimia 80. 
Akiwasilisha taarifa ya namna Tanzania inavyopambana na kudhibiti magonjwa mbalimbali wakati wa mkutano wa 69 wa afya duniani unaofanyika Geneva nchini Uswisi hivi karibuni, Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania imeweza kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria kutoka asilimia 18 hadi 9.5 kwa Tanzania bara na kwa upande wa Zanzibar imefanikiwa kupunguza idadi ya wagonjwa hadi kufikia asilimia 0.6 .
Juhudi zinazofanywa na Serikali katika kujali na kusimamia afya za watu wake zinapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania kwa nafasi yake ili kutokomeza ugonjwa wa malaria ambao ni hatari kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Shime Watanzania, tukumbuke Zama zimebadilika, “Sio kila homa ni malaria nenda ukapime” na “lala kwenye chandarua kila siku” kujikinga na malaria, kumbuka Tanzania bila malaria inawezekana.

Comments