Featured Post

BILIONI 8 KUTUMIKA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA VYUO VYA AFYA

  
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Hamisi Kigwangallah

Na Aron Msigwa - MAELEZO.
25/5/2016. 
Dodoma.

Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 8 kuboresha miundombinu ya vyuo vya Afya kote nchini katika mwaka wa fedha 2016/2017 ili kuwawezesha wanafunzi wa fani ya Afya kusoma katika mazingira mazuri.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Hamis Kigwangala ameyasema hayo Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Muhambwe Mhe. Atashasta Justus Ntitiye, alieyata kujua mkakati wa Serikali wa kuboresha vyuo vya Afya nchini hususan chuo cha Uuguzi Kibondo kilicho katika jimboni lake la Muhambwe wilayani Kibondo.
Dk. Kigwangala amesema kuwa Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017 imejipanga kuboresha mazingira ya vyuo vya Afya katika maeneo mbalimbali nchini kikiwemo Chuo cha Uuguzi Kibondo ambacho kimetengewa shilingi milioni 680.
Ameeleza kuwa vyuo vya Afya vimekuwa vikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo madeni ya wazabuni wa vyakula waliokuwa wakiidai  Serikali  kiasi cha shilingi Bilioni 6.8 kuanzia mwaka 2009 hadi 2015.
Amesisitiza kuwa tayari Serikali imekwishahakiki madeni yote ya wazabuni   ili yaweze kulipwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 na kuongeza kuwa suala la usambazaji wa vyakula limeachwa chini Sekta binafsi ili zifanye kazi hiyo.
Katika hatua nyingine Dk. Kigwangala amesema kuwa kuwa Serikali inaendelea kuangalia uwezekano wa kuyatumia majengo yaliyoachwa kwenye kambi za wakimbizi zilizofungwa mkoani Kigoma hususan wilaya ya Kibondo ili yaweze kutumika kama vyuo vya kutolea elimu ya Afya.
"Niko tayari nikishirikiana na waheshimiwa wabunge kwenda mkoani Kigoma kuzungumza na viongozi wa mkoa huo ili tuweke utaratibu wa namna ya kuyatumia majengo hayo" Amesisitiza Dkt.Kigwangala.

Comments