Featured Post

HAYA NDIYO MAGARI MAALUMU YANAYOPAA


 
Na Kalunde Jamal
Fikiria magari kama haya iwapo yatakuja nchini Tanzania ni kwa jinsi gani yanaweza kusaidia kero ya foleni zisizokuwa na kikomo katika Jiji la Dar es Salaam?
Haya siyo mengine ni magari ya kupaa ambayo yametengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu yanayoyawezesha kupaa inapostahili pia hutembea ardhini.

Kuna magari mengi yanayopaa lakini iliyozinduliwa hivi karibuni na kampuni ya Uingereza iitwayo Terrafugia ni aina nyingine ya gari inayopaa.

Gari hilo lenye uwezo wa kupaa kwa saa 20 angani, linaweza kuwa ndege binafsi yenye viti viwili matairi manne na mabawa yanayofunga na kufungua ili kuweza kuendeshwa kama gari la kawaida barabarani.

Aina hii ya gari ina uwezo wa kusafiri kilometa 180 kwa saa, huhitaji eneo kubwa kama la kutua na kupaa ndege ili liweze kupaa na kushuka iwapo dereva atahitaji.

Teknolojia hii sasa imekukua pia kampuni nyingine kutoka nchini Slovakia iitwayo AeroMobil inatarajia kuingiza sokoni magari yanayopaa itakapofika mwaka 2017 na kutumika kama magari mengine ya kawaida, huku yakihitaji nafasi ndogo kupaa na kutua tofauti na yale ya Terrafugia ambayo yanahitaji nafasi kubwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni hiyo, mpaka sasa wameweza kuunda gari kwa kutumia teknolojia mpya ambalo hubadilika na kuwa ndege iwapo mtuamiaji atahitaji kupaa.

“Hapo awali tulikuwa tukitumia teknolojia ya zamani kuunda magari ijulikanayo kama Aeromobil 1.0 na Aeromobil 2.5 lakini sasa gari hili litakuwa likitumia gesi na litakuwa na mabawa yanayoweza kufunguka na kulisaidia kupaa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Gari hilo halitahitaji kukimbia kwa umbali mrefu kwenye lami ili kupaa, badala yake litanyanyuka moja kwa moja kutoka mahali liliposimama.

Hata hivyo, gari hilo litabeba abiria wawili ambao ni rubani na abiria wake lakini pia litakuwa na uwezo wa kuruka umbali wa kilometa tatu pekee kutoka ardhini na kabla ya kujazwa mafuta litasafiri kilometa 700.

Kabla ya gari hizo, gari nyingine zilizokuwa zikipaa zilikuwa zikijulikana kama “SKYWORTHY na zikiwa zinatembea kawaida na huwezi kuona mbawa zake wala kudhani kuwa zinaweza kupaa jambo ambalo lilifanya ziivutie zaidi.

Gharama ya gari hizo ni Dola za Marekani 300,000.
CREDIT: MWANANCHI

Comments