Featured Post

YANGA FUNGA, SIMBA RUDISHA - KAMA 1996 VILE!

Picha kwa hisani ya jestina-george.com

SIMBA na Yanga zimetoka sare. Ni sare ambayo haikutegemewa na mashabiki wa Yanga waliokuwa wanaamini timu yao ingeweza kupata ushindi wa mabao mengi baada ya kuongoza kwa mabao 3-0 hadi timu zinakwenda mapumziko.
Lakini kitendo cha Simba kurudisha mabao yote matatu katika kipindi cha pili, siyo tu kimedhihirisha kwamba ngome za timu zote ni mbovu na kwamba timu zetu hazina utamaduni wa kulinda mabao yao, bali kimewakumbusha wengi sare ya ajabu ya ‘funga-nirudishe’ kama ile ya mwaka 1996 mjini Arusha.
Yawezekana wengine wamesahahu mechi hiyo, ambayo ilikuwa ya pili kwa timu hizo kukutana mjini Arusha. Ngoja niwamegee uhondo.
Wapenzi wa soka wa mikoa ya Singida, Dodoma, Mara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Dar es Salaam na nchi jirani ya Kenya walianza kuwasili mjini Arusha kuanzia Novemba 7 kushuhudia pambano la soka la marudiano la Ligi Kuu ya Muungano kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga, ambalo lilipangwa kufanyika Jumamosi, Novemba 9, 1996 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Timu hizo zilipambana baada ya miaka sita tangu zilipopambana kwa mara ya kwanza mjini humo mwaka 1989 katika kuwania Kombe la Bonanza lililoandaliwa na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) na Yanga kunyakua ubingwa huo kwa ushindi wa goli 1-0 lililofungwa na Joseph Machella.
Mashabiki hao waliwasili sambamba na timu hizo zilizoondoka Jijini Dar es Salaam siku hiyo ya Alhamisi, Novemba 7 kwa mabasi kufuatia msaada wa tiketi 30 ambazo kila moja ilipewa na Chama cha Soka Tanzania (FAT) baada ya chama hicho kukosa shilingi milioni moja za kuipa kila timu kwa ajili ya maandalizi. Simba iliwasili kwa basi la Super Star wakati Yanga ilikwenda kwa basi la Tawfiq na kupelekwa na mfadhili wao wa mjini humo ‘kula maraha’ katika hoteli ya kitalii ya Sakina.
Pambano hilo, lilichezeshwa na mwamuzi Bakari Mtangi wa Tanga aliyesaidiana na washika vibendera Aggrey Mnzavas wa Kilimanjaro na Sudi Abdi wa Arusha. Kiingilio katika pambano hilo, ambalo mgeni rasmi alikuwa Jaji wa Mahakama ya Kimataifa iliyokuwa inashughulikia mauaji ya Rwanda Leonnart Aspegren, kilikuwa Shs. 5,200 kwa Jukwaa A, Shs. 2,200 mzunguko na Shs. 500 kwa yosso.
Hata hivyo, bao lililofungwa na Dua Said dakika za majeruhi siku hiyo liliiokoa Simba kuepuka janga la kuendelea kuwa mteja wa Yanga mwaka huo na kuzifanya timu hizo zitoke sare ya magoli 4-4 katika pambano lililopooza.
Hii ilikuwa mechi pekee ya sare ya magoli mengi kuliko zote baina ya timu hizo. Mechi iliyokuwa na magoli mengi kuliko zote ilikuwa ya mwaka 1992 Simba iliposhinda kwa penati 6-5 na mwaka 1966 Yanga ilipoifunga Simba 5-4.
Simba ilikuwa inaongoza kwa  magoli matatu  hadi dakika ya 60. Iliwachukua vijana wa Mtaa wa Msimbazi dakika saba tu kuhesabu goli la kwanza kupitia kwa Thomas Kipese kwa shuti kali la mpira wa adhabu lililokwenda moja kwa moja wavuni. Adhabu hiyo ilitolewa na mwamuzi Bakari Mtangi wa Tanga baada ya mlinzi Abdallah Msheli kumfanyia madhambi Ahmed Mwinyimkuu wa Simba katika eneo la hatari.
Kuingia kwa bao hilo kuliwafanya Yanga wazinduke na kuliandama lango la Simba mfululizo katika dakika za 10,19 na 22, lakini walikosa mabao ya wazi kabisa. Jitihada za timu hiyo kusawazisha zilizaa matunda katika dakika ya 28 wakati Edibily Lunyamila alipoifungia bao kwa njia ya penati. Lunyamila aliwasili mjini humo muda mfupi kabla ya pambano akitokea Afrika Kusini kupitia Nairobi. Penati hiyo ilitolewa na mwamuzi Mtangi baada ya Rajab Msoma wa Simba kuunawa mpira katika eneo la hatari katika jitihada za kuokoa.
Dakika tatu baadaye kipa Baldwin Sisinawa wa Yanga ilimbidi afanye kazi ya ziada kuokoa bao la wazi alipopangua kiki kali ya Bitta John na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda. Mwinyimkuu aliwarejeshea furaha mashabiki wa Simba alipofunga bao la pili katika dakika ya 43 baada ya kuunganisha hewani krosi ya Kipese aliyoituliza gotini kabla ya kufumua shuti kali lililojaa wavuni. Hadi mapumziko Simba ilikuwa inaongoza kwa 2-1.
Kipindi cha pili Simba iliwatoa Hoza, Bitta na Mwinyimkuu na kuwaingiza Marsha, Tigana na Dua, wakati Yanga iliwatoa Sylvatus Ibrahim na Bushako na nafasi zao kuchukuliwa na Mgaza na Anwar. Mabadiliko hayo yalianza kwa Simba kupata bao la tatu lililofungwa na Dua Said kwa kichwa katika dakika ya 60 kufuatia krosi ya Mwanamtwa Kihwelu iliyomkuta Bitta (kabla hajatoka) aliyemsogezea mfungaji ambaye aliukwamisha mpira wavuni.
Pamoja na magoli hayo, Yanga haikukata tamaa na juhudi zao ziliwezesha kupata bao la ‘dezo’ katika dakika ya 64 wakati Hoza (kabla hajatoka) alipojifunga mwenyewe wakati alipokuwa anamrejeshea kipa wake Issa Manofu, ambaye alikuwa ametoka golini.
Bao la tatu la Yanga lilifungwa na Kizota katika dakika ya 70 kwa kichwa baada ya kuunganisha wavuni mpira uliorushwa na Bakari Malima. Katika dakika ya 75 Sanifu Lazaro aliifungia Yanga goli la nne kwa kichwa lililoamsha mayowe mengi kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo. Sanifu alifunga bao hilo kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Lunyamila aliyemlamba chenga Deo Mkuki na kumimina krosi iliyomkuta mfungaji.
Wachezaji wa timu ya soka ya Yanga walilalamika kuwa, walipunjwa mgao wao uliotokana na mapato ya mechi hiyo. Wachezaji hao walisema, mbali ya kupunjwa mgao wao, walidanganywa pia na viongozi wao kuwa, klabu hiyo ilipata shilingi milioni 4.0 kutokana na shilingi milioni 30.5 zilizopatikana katika mechi hiyo. Kila mchezaji alipata Shs. 73,000, kiasi ambacho ni asilimia 40 ya shilingi milioni nne, kinyume na makubaliano kati yao na viongozi kwamba, timu hiyo inapotoka sare wachezaji hustahili asilimia 50 ya mapato hayo.
Katika mchezo huo viongozi waliosimamia mapato  huko Arusha walikuwa Mwenyekiti Jabir Katundu na Mjumbe wa Kamati Kuu, Edward Ngabona, ambaye ndiye aliyegawa fedha hizo kwa wachezaji. Wakati kila mchezaji alipata Shs. 73,000, makocha wa timu hiyo, Sunday Kayuni na Jella Mtagwa na daktari wa timu, Godfrey Kalimba, walipata Shs. 109,000 kila mmoja.
Wachezaji hao walimshutumu Ngabona kwa kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa, kila mchezaji alipata Shs. 100,000 kutokana na mapato ya mchezo huo wakati haikuwa kweli. Waliilaumu pia FAT kwa kuwapa mgao wa timu hiyo viongozi wa klabu badala ya wachezaji kama walivyoomba kabla ya mchezo huo kutokana na kutokuwa na imani nao baada ya kuwadhulumu zawadi ya ushindi wa pili ya Shs. Milioni 2.5 ya Kombe la Hedex Afrika Mashariki na mechi nyinginezo.
Walisema, kulaghaiwa kwao kulichangiwa sana na kuugua ghafla kwa mjumbe wa Kamati ya Kudhibiti Mapato ya klabu hiyo, Majjid Suleiman, mara baada ya mchezo huo, ambaye walisema alikuwa mstari wa mbele kutetea haki na maslahi ya wachezaji wa timu hiyo. Majjid ndiye aliyesimamia mapato ya timu hiyo ilipopambana na Simba kwenye mchezo wa awali wa Ligi Kuu ya Muungano na pia zawadi ya Shs. Milioni 7.5 ilizopata kwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Safari Lager, ambapo kila mchezaji alipata Shs. 195,000.
SIMBA: Issa Manofu, Deo Mkuki, Alphonce Modest, Mustafa Hoza/Hussein Marsha, Mathias Mulumba, Shaaban Ramadhan, Mtwa Kihwelu, Bitta John/Ally Yussuf, Abdallah Mwinyimkuu/Dua Said, Rajab Msoma na Thomas Kipese.
YANGA: Baldwin Sisinawa, Sylvatus Ibrahim/Reuben Mgaza, Kenneth Mkapa, Bakari Malima, Abdallah Msheli, Said Mwamba, Idelfonce Amlima, Thabit Bushako/Anwar Awadh, Mohammed Hussein, Sanifu Lazaro na Edibily Lunyamila.

NB: Makala haya ni kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘MIAKA 50 YA UBINGWA WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za mwisho kuchapishwa. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu +255 715 070109 au brotherdanny5@gmail.com.

Comments