Featured Post

WANAWAKE WA TANZANIA KIBOKO, WAIKONG'OTA MSUMBIJI 10-0




TIMU ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20, The Tanzanite, jana ilianza vema kampeni ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa mwakani nchini Canada, baada ya kuifumua Msumbiji mabao 10-0.
The Tanzanite chini ya kocha wake Rogasian Kaijage, ilipata ushindi huo wa kimbunga katika mechi ya kwanza ya kampeni hizo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, vijana wa The Tanzanite walianza kuonyesha cheche zao dakika ya saba tu baada ya Neema Paul kufunga bao la kwanza akiunganisha krosi ya Therese Yona kabla Shelder Boniface kufunga la pili dakika ya 25, baada ya kuwatoka mabeki na kumlamba chenga kipa, Paulina Jambo.
Dakika ya 36, The Tanzanite walizidi kutakata baada ya kupata bao la tatu likifungwa na Deonisia Daniel kabla ya kufunga la nne, likiwekwa nyavuni na Shelder baada ya kumlamba chenga kipa, hivyo wenyeji kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao manne.
Kipindi cha pili kiliendelea kuwa kizuri kwa The Tanzanite kwani dakika ya 47, walipata bao la tano likifungwa na Neema, likiwa la pili kwake katika mechi hiyo.
Dakika ya 64, kipa wa Msumbiji, Paulina, aliumia akiwa katika harakati za kuokoa baada ya kugongana na Therese aliyekuwa akienda kufunga, hivyo akatolewa na kuingia Catarina Franque.
The Tanzanite walizidi kutakata kwani dakika ya 69, Shelder alirejea katika nyavu za Msumbiji na kufunga bao lake la tatu likiwa la sita kwa timu yake, akitumia udhaifu wa kipa Franque kuutema mpira vibaya.
Bao la saba lilifungwa na Amina Ali kwa shuti la mbali kabla ya Deonesia kufunga kwa penalti baada ya Shelder kuangushwa ndani ya boksi wakati akienda kumtungua kipa.
Dakika ya 81, The Tanzanite walipata bao la tisa likifungwa na Amina kwa shuti la mbali kabla ya kupata bao la 10, likifungwa na Stumai Abdallah dakika 87 baada ya kupanda mbele na ‘kuuchopu’ mpira.
Kocha Kaijage alisema anashukuru timu yake kupata ushindi huo ambao ni mwanzo mzuri kuelekea mechi ya marudiano itakayochezwa wiki mbili zijazo mjini Maputo.
Alisema ushindi huo ni faraja kubwa kwa wachezaji na Watanzania, na mwanzo wa kujenga kikosi imara cha timu ya taifa ambayo itawapa furaha wapenzi na mashabiki wa soka kwa siku zijazo.
Kaijage alisema pamoja na timu yake kupata ushindi mnono, bado kuna makosa yalifanywa na nyota wake kwani kama wangezitumia nafasi zote walizopata, wangeweza kuibuka na ushindi wa mabao 20.
Kocha wa Msumbiji, Muhadji Raxide, aliwapongeza The Tanzanite kwa kucheza vizuri akisema walistahili kushinda na kuongeza kuwa  timu yake imepata kichapo hicho kutokana na uchanga wake.
The Tanzanite:  Celina Julius, Stumai Abdallah, Maimuna Said, Fatuma Issa, Anastazia Anthony, Deonisia Daniel, Vumilia Maarifa, Amina Ali, Neema Paul, Shelder Boniface, Therese Yona.
Msumbiji: Paulina Jambo, Esperancia Malaita, Felismisa Moiane, Emma Paulino, Gilda Macamo, Deolinda Gove, Jessica Zunguene, Cidalia Cuta, Nelia Magate, Lonica Tsanwane, Onesma David.

Comments