Featured Post

MBIO ZA ROCK CITY MARATHON 2013 ZAFANA


Na Mwandishi WetuWANARIADHA Alphonce Felix kutoka Arusha na Vicoty Chepkemoi kutoka Kenya jana walitawazwa mabingwa wapya mbio za kilomita 21 katika mashindano ya Rock City Marathon 2013 yaliyofanyika jijini Mwanza na kujipatia zawadi ya shilingi mil. 1.5 kila mmoja.
Alphonce alishinda mbio hizo kwa upande wa wanaume baada ya kutumia saa 1:02:17 hivyo kuvunja rekodi iliyowekwa mwaka jana na Kopiro Chacha aliyetumia 1:05:00, wakati kwa upande wa wanawake, Chepkemoi akitumia saa 1:12:44.
Joel Kimtiae wa Kenya alishika nafasi ya pili kwa wanaume, huku Sarah Ramdhani wa Arusha, Tanzania, akikamata nafasi hiyo upande wa wanawake, wakifuatiwa na Sambo Andrea kwa wanaume na Zakia Mrisho kwa wanawake wote wakitokea Tanzania.
Zaidi ya wanariadha 1,090 kutoka mikoa mbalimbali nchini walishiriki, pamoja na wakimbiaji kutoka nchi za Kenya, Uganda, India, Canada, Australia, Afrika Kusini, Rwanda,  chini ya uratibu wa kampuni ya Capital Plus International (CPI) ya jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo kwa mwaka huu yalidhaminiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Africa Barrick Gold, Precision Air, Airtel kupitia Airtel Money, TANAPA, Bank M, PPF, Nyanza Bottling Ltd, New Mwanza Hotel, Sahara Communications, Continental Decoders na Umoja Switch.
Wakati Wambura Lameck kutoka Holili aling’ara katika mbio za km tano, Dotto Ikangaa wa Arusha akishika nafasi ya pili, Muhindiro Yusto kutoka Mwanza alishinda km tatu kwa wazee na Benard Samike pia wa Mwanza kwa upande wa watu wenye ulemavu.
Kwa upande wa watoto ambao walikimbia kilometa mbili, Benedicto Mashauri wa Mwanza alishika nafasi ya kwanza huku Suzana Madary wa Mwanza pia aking’ara kwa upande wa wasichana na kuibuka kidedea.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) Suleiman Nyambui alisema Rock City Marathon imeonyesha kukua kila mwaka, kwa kuwa ina uwezo wa kukimbiza mbio za ngazi zote; nusu marathon, kilometa tano, kilometa tatu kwa walemavu, kilometa tatu kwa wazee na kilometa mbili kwa watoto.
Alisema shirikisho lake limezingatia usimamizi mzuri wa Rock City Marathon na liko tayari kutoa kibali kitakachoiwezesha Capital Plus International kuandaa mbio ndefu za kilometa 42 (full Marathon), watu wakiweza kuhamasika na kushiriki kwa wingi zaidi.
Ofisa Michezo Manispaa ya Ilemela, Kizito Bahati, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Everist Ndikilo, aliwataka wakazi wa Kanda ya Ziwa kuchangamkia fursa inayoletwa na mbio hizo, huku akiwataka viongozi wa vyama vya riadha kuwa na program endelevu kwa kushirikiana na maofisa michezo wa mikoa na wilaya.
Mbali na medali walizopata, washindi hao walipata zawadi za fedha taslimu ambapo washindi wa pili katika mbio za kilometa 21, upande wa wanaume na wanawake walipata sh 900,000 na ving’amuzi vya Continental kila mmoja huku washindi wa tatu wakipewa king’amuzi na sh 700,000.
CHANZO: HABARILEO

Comments