Featured Post

MALINZI: NINAWEZA, NIPENI KURA


MGOMBEA wa nafasi ya rais katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, anayechuana na Athumani Nyamlani katika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho hilo, amezidi kusisitiza kuwa anaweza na anaomba aaminiwe zaidi na Watanzania kuongoza chombo hicho.
Akizungumza Jumatano wiki hii siku anazindua rasmi kampeni zake mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Malinzi alitaja vipaumbele vyake kadhaa atakavyovifanyia kazi kama akipewa ridhaa ya kuongoza shirikisho hilo.
Malinzi anasema ili soka ya Tanzania iweze kusonga mbele inahitaji vitu vinne muhimu, ambavyo ni vipaji, makocha, vifaa na viwanja.
“Kuhusu vipaji, sayansi ya uibuaji vipaji ni muhimu na si kila mtu anaijua. Watafutwe wanaoijua, watufanyie kazi ya kutuibulia vipaji vipya na katika hili ni sharti mpira wa ushindani uchezwe nchini kote ili vipaji vionekane,” anasema.
Kuhusu makocha anasema kuna haja ya kuwaendeleza zaidi ili kuhakikisha taifa linakuwa nao wengi ambao watasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua vipaji vya wachezaji makinda, hasa wanafunzi.
Malinzi anasema, kama akiingia madarakani atahakikisha anasaidiana na wadau mbalimbali kuvipatia vifaa shule, kwani huko ndiko mpira unakochezwa, ikiwa pamoja na kuomba mamlaka husika kuondoa kodi kwenye vifaa vya michezo, huku akisisitiza umuhimu wa viwanja bora.
Kuhusu Idara ya Ufundi, anasema atahakikisha anaiboresha zaidi kwani ndiyo iliyobeba jukumu la kuendeleza soka hapa nchini huku fedha nyingi za TFF akisema zitaelekezwa ndani ya idara hiyo, ikiwa ni pamoja na rasilimali mbalimbali.
“Iwapo nitachaguliwa nitapendekeza jukumu la kwanza la Kamati ya Utendaji liwe ni kurekebisha na kuboresha mfumo wa uendeshaji wa idara ya ufundi.
“Nitapendekeza Idara ya Ufundi iendelee kuongozwa na Mkurugenzi wa Ufundi na chini yake awe na wakurugenzi wasaidizi wa vitengo watatu,” huku akiwataja mmoja atashughulika na ufundi, mwingine ni elimu na mafunzo na watatu ni maendeleo ya mpira.
Mgombea huyo alisema pia atashirikiana na klabu, vyama na wadau mbalimbali katika kuendeleza soka, hasa kuhakikisha taifa linafanikiwa kusonga mbele.
Unajua Rais Jakaya Kikwete wakati anazindua ziara ya Kombe la Dunia katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam pamoja na mambo mengine anasema:
‘‘Kwa Watanzania wenzangu tuichukulie ziara ya Kombe la Dunia nchini mwetu kama ni changamoto kubwa kwetu inayotutaka tufanye vizuri zaidi katika soka ili tulingane na heshima hii tuliyopewa. Hasa ni changamoto kwa viongozi wa soka wa ngazi zote pamoja na wachezaji na wapenzi wa mpira wa miguu nchini. Kuja kwa kombe hili ni deni kwetu na kulilipa kwetu sisi ni kuzinduka, tuendeleze kiwango chetu cha soka nchini.
“Hili jambo linawezekana. Wapo wenzetu Afrika wameweza, kwa nini sisi tusiweze? Wao ni watu kama sisi, maadam wameweza na sisi tutaweza.
“Lakini ili tuweze hatuna budi kuiga mfano hususan waliyofanya wenzetu na wanayoendelea kufanya kuendeleza mpira wa miguu. Twende tukajifunze kutoka kwao. Lakini hata kabla ya kwenda huko, yapo mambo hatuna budi kuyafanya. Naomba nitaje baadhi yake:
“Tuimarishe uongozi, utendaji na uendeshaji wa klabu za mpira. Mchezaji hufundishwa kucheza mpira katika klabu yake. Hapo ndipo hufundishwa maarifa ya kucheza mpira na vipaji kuendelezwa. Hebu tujiulize hali ya klabu zetu za soka ikoje. Je, zinaongozwa vizuri? Zinaendeshwa vizuri?
“Jibu tunalijua sote kuwa ni hapana. Lazima suala hili tulitafakari kwa makini na kulipatia jawabu. Tukishindwa kupata jawabu muafaka na mambo yakaachwa kuendelea yalivyo, mpaka mwisho wa dunia hatutakuwa tunasogea popote.
“Tupate walimu wenye uzoefu kufundisha timu zetu. Hii ndiyo njia ya uhakika ya kukuza na kuendeleza vipaji, hivyo kupata wachezaji bora.
“Tuwekeze katika kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji kutoka umri mdogo. Klabu ziwe na timu za watoto na vijana. TFF isaidie kuanzishwa kwa shuleza mchezo wa mpira wa miguu kwa watoto na vijana. Mashuleni wapatikane walimu wa michezo walio wazuri kufundisha.
“TFF ionekane zaidi ya ilivyo sasa katika mipango ya kuendeleza soka mashuleni, vijijini, mitaani na klabuni. TFF ikiwa na mipango na kuisimamia na kuwabana wadau kuitekeleza itasaidia. Vinginevyo TFF itabakia kusimamia Ligi Kuu, kutoa adhabu kwa wachezaji na kusimamia timu ya taifa. Hiyo haitoshi.’’
Malinzi anasema, kutokana na angalizo hilo la rais ana uhakika mkubwa wa kufanya makubwa zaidi kama atafanikiwa kuchaguliwa kuiongoza taasisi hiyo.
“Kama nitachaguliwa kuwa Rais wa TFF, kwa kushirikiana na viongozi wote wa TFF kuanzia ngazi ya klabu, wilaya, mikoa na Kamati ya Utendaji Taifa na kwa kuhusisha kwa karibu vyama vya kimataifa vya FIFA na CAF, serikali, halmashauri, taasisi zisizo za kiserikali, vyombo vya habari, sekta binafsi, mashirika ya umma na wadau wa mpira wa miguu Tanzania ninaahidi kuenzi mafanikio ya awamu inayomaliza muda wake, kustawisha utulivu katika uendeshaji wa mpira na kufanya jitihada za kubuni, kuboresha na kustawisha maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania. Jitihada kubwa zitawekwa kwenye maeneo makuu yafuatayo:
“Ufundi: Muundo wa Idara ya Ufundi, Katiba ya TFF imeainisha wazi kuwa TFF ndiye msimamizi mkuu wa soka, hivyo jukumu la kuleta maendeleo ya mchezo huu kwa kiasi kikubwa linaiangukia TFF. Ni kwa msingi huu basi asilimia kubwa ya rasilimali za TFF lazima iwekezwe katika kuleta maendeleo ya mpira.
“Kwa mfumo wetu wa uendeshaji, kichocheo kikuu cha maendeleo ya mpira ni idara ya ufundi ya TFF. Hivyo idara hii ya ufundi inapaswa kuwa ndiyo idara mama ya TFF ambayo inapaswa kuongoza kwa matumizi ya fedha, idadi ya waajiriwa na matumizi ya rasilimali nyingine za TFF. Kwa sasa pale TFF hali sivyo ilivyo.
“Iwapo nitachaguliwa nitapendekeza jukumu la kwanza la Kamati ya Utendaji liwe ni kurekebisha na kuboresha mfumo wa uendeshaji wa idara ya ufundi. Nitapendekeza idara ya ufundi iendelee kuongozwa na Mkurugenzi wa Ufundi na chini yake awe na wakurugenzi wasaidizi wa vitengo watatu; Mkurugenzi Msaidizi (Ufundi), Mkurugenzi Msaidizi (Elimu na Mafunzo), ambaye kwa sasa anaitwa Education Officer na Mkurugenzi Msaidizi (Maendeleo ya Mpira).
“Kitengo cha Ufundi kitahusika na kubuni na kusimamia shughuli zote zinazohusu maendeleo ya timu za taifa kuanzia za wakubwa hadi za vijana. Hii itakuwa ni pamoja na kuandaa mitaala ya taifa (national football curriculum) ya ufundishaji wa mpira Tanzania kuanzia umri wa miaka mitano hadi watu wazima.
“Walimu wa timu za taifa wataripoti kwake. Kitengo cha Elimu na Mafunzo kitahusika na kubuni na kuratibu kozi zote na mafunzo yote yanayohusiana na mpira kama vile kozi za marefa, makocha, madaktari, makamisaa, watawala, waandishi wa habari za michezo, n.k.
“Kitengo cha Maendeleo ya mpira kitahusika na kubuni, kuratibu na kusimamia mpango wa maendeleo ya vijana (grass root) na kutafuta vipaji (scouting).
Kitengo hiki kitafanya kazi kwa kushirikiana kwa ukaribu na idara za serikali.
“Wakuu wa vitengo hivi wataajiriwa kwa kufuata vigezo makini na bila upendeleo wala kujuana.”
Kwa muda mrefu Malinzi amekuwa mstari wa mbele katika michezo ambapo kati ya mwaka 1995 na 2001, Kampuni yake ya DJB Promotions Ltd iliweka historia ya ngumi za kulipwa nchini kwa kudhamini mabondia walionyakua mataji ya dunia akiwamo Rashid Matumla.
Kati ya mwaka 1999 na 2005, alishika nyadhifa mbalimbali Yanga zikiwamo seneta, mkurugenzi wa kuchaguliwa na Kaimu Katibu Mkuu.
Amekuwa mwenyekiti wa mashindano ya mpira wa miguu Mkoa wa Pwani (2009 - 2011) na mjumbe wa Baraza la Michezo la Mkoa wa Dar es Salaam (2009-2012).
Tangu mwaka 2011 hadi sasa ni mjumbe kwenye Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka Wilaya ya Misenyi, pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera (KRFA).
Kwa sasa ni Mwenyekiti wa KRFA, wadhifa alioupata mwaka 2012 na anaendela na utekelezaji wa programu ya vijana ya miaka mitatu 2013-16.

Comments