Featured Post

MABAO 162, MECHI 76 ZA SIMBA NA YANGA LIGI KUU

Furaha ya ubingwa kwa Simba 2012 huku wakisherehekea ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya mahasimu wao, Yanga.

Na Daniel Mbega
HUKU utasikia: “Simba! Simba! Simba!” halafu kule nako kutasikika: “CCM! CCM! CCM!” Naam, hivi ni vibwagizo vinavyosikika kila wakati Simba na Yanga zinapokutana, iwe kwenye mechi za Ligi, mashindano mbalimbali na hata zile za kirafiki.
Mashabiki wa Simba wanaweza kusikika pia wakisema: “Amesimama kidedea, eeee kidedea!” halafu upande mwingine utawasikia wakichombea: “Kitimtimu, mtakiona leo, nyumba ya shetani mwendawazimu kaingiaje!”
Hapo hakuna ugomvi, ni burudani ya jukwaani huku mashabiki wakiendelea kutazama buradani nyingine ndani ya uwanja wakati vijana walio katika jezi nyeupe na nyekundu wakipelekeshana puta na wenzao walio kwenye jezi za kijani na manjano.
Mandhari haya ndiyo yaliyokuwepo Jumapili Oktoba 20, 2013 kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa, wakati Simba na Yanga zilipoumana katika mchezo wa kwanza wa  Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013/2014.
Wakati Yanga, ambayo inatetea ubingwa wake huku ilikuwa katika nafasi mbaya kwenye msimamo, ilikuwa inatafuta ushindi ili kukwea kileleni lakini pia kulipa kisasi cha mabao 5-0 ilichokipata mwaka 2012 katika mchezo wa mwisho. Jambo hili lilionekana kuwa ni ndoto baada ya kushindwa kutalinda mabao yake matatu iliyoyapata katika kipindi cha kwanza, hivyo kuifanya Simba isawazishe na kuleta matokeo ya ajabu ya sare ya 3-3.
Simba wao walikuwa na mambo mawili: Kwanza, walitaka kulipa kisasi cha kufungwa katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Mei 17, 2013, lakini pili, walikuwa wanatafuta ushindi ili kujiweka sawa zaidi na kutwaa ubingwa baada ya mwaka huu kukosa nafasi hata ya pili.

Mechi zao
Hii ilikuwa mechi ya 76 kuzikutanisha Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu tangu mwaka 1965 ilipoanzishwa Ligi ya Taifa na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Milan Celebic.
Katika kipindi chote hicho, msisimko wa kuelekeza mechi hizi umekuwa mkubwa, bila kujali nani anawania kitu gani.
Hata hivyo, katika mechi hizo 76, Watanzania wameshuhudia Yanga ikitawala zaidi kwa kushinda mara 29, wakati Simba imeshinda mara 22. Timu hizo zimetoka sare mara 25 huku mabao 162 yakifungwa. Kati ya mabao hayo, Yanga imefunga 86 na Simba imefunga 75. Ikumbukwe kwamba, mechi hizi hazihusishi mechi za Ligi ya Muungano.

Idd Pazi, Kaseja kiboko
Makipa wa Simba, Idd Pazi ‘Father’ na Juma Kaseja wana rekodi ya pekee kwenye mechi za Simba na Yanga kutokana na ukweli kwamba ndio makipa pekee baina ya timu hizo kufunga bao. Pazi alifunga bao la kuongoza kwa penalti Jumamosi Machi 10, 1984 katika dakika ya 20 na akajitahidi kulinda lango la Simba hadi dakika ya 72 wakati Omar Hussein alipomzidi ujanja na kusawazisha. Matokeo yakawa 1-1.
Kaseja naye aliingia kwenye rekodi hiyo katika mechi ya Mei 6, 2012 ambayo Simba ilishinda 5-0 baada ya kufunga kwa penalty katika dakika ya 67, likiwa ni la nne kwa timu yake.
Mlinzi Suleiman Said Sanga ‘Totmund Wanzuka’, ndiye pekee aliyewahi kujifunga wakati timu hizo mbili zilipomenyana kwenye Ligi. Sanga alijifunga katika harakati za kuokoa katika mechi ya Julai 19, 1977 wakati Yanga ilipokubali kipigo cha mabao 6-0, huku Abdallah Athumani ‘King Kibadeni’ akifunga hat trick (mabao matatu) peke yake na mengine mawili yakifungwa na Jumanne Hassan Masimenti.

Wafungaji wa mabao
Katika mechi 72 zilizopita na kuzaa mabao hayo 147, Omar Hussein ‘Keegan’ wa Yanga ndiye anayeongoza kwa ufungaji, akiwa amezifumania nyavu mara sita akifuatiwa na Abeid Mziba ‘Tekero’, Idd Moshi na Jerry Tegete wa Yanga pia, pamoja na Edward Cyril Chumila na Musa Hassan 'Mgosi' ambao wamefunga mabao manne kila mmoja.
Waliofunga mabao matatu kila mmoja ni Kitwana Manara ‘Popat’, Maulid Dilunga, Said Mwamba ‘Kizota’ na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ wa Yanga, pamoja na Abdallah Athumani ‘Kibadeni’.
Orodha hiyo inaonyesha waliofunga mabao mawili kwa upande wa Yanga ni Salehe Zimbwe, Juma Mkambi, Rashid Hanzuruni, Said Sued 'Scud', Makumbi Juma 'Homa ya Jiji’, Issa Athumani, Idelfonce Amlima, Sekolojo Chambua, Ben Mwalala na Sunday Manara.
Kwa upande wa Simba ni Jumanne Hassan ‘Masimenti’, John Makelele 'Zig Zag’, Malota Soma ‘Ball Jugler’, Nicodemus Njohole, Dua Said, Steven Mapunda, Madaraka Selemani, Ulimboka Mwakingwe, Athumani Machupa, Emmanuel Okwi.
Wachezaji waliopachika bao moja kwenye mechi hizo kwa upande wa Yanga ni Mawazo Shomvi, Abdulrahman Lukongo, Andrews Tematema, Emmanuel, Leonard Chitete, Gibson Sembuli, Charles Boniface, Edgar Fongo, Justin Mtekere, Thomas Kipese, Sanifu Lazaro, Ken Mkapa, James Tungaraza, Akida Makunda, Constantine Kimanda, Salvatory Edward, Kally Ongala, Pitchou Mwango Kongo, Aaron Nyanda, Said Maulid, Athumani Idd, Stephano Mwasika, Davies Mwape, Said Bahanuzi, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza.
Nyota wa Simba waliofunga bao moja kila mmoja ni Mustafa Choteka, Haji Lesso, Willy Mwaijibe, Haidari Abeid 'Mchacho', Adam Sabu, Mohammed Bakari ‘Tall’, Abbas Dilunga, Abdallah Mwinyimkuu, Thuwein Ally, Kihwelu Musa, Zamoyoni Mogella, Mohammed Bob Chopa, Sunday Juma, Mavumbi Omar, George Masatu, Athumani China, Mchunga Bakari, Abdallah Msamba, Athumani Machepe, Abuu Juma, Juma Amir, Joseph Kaniki, Athumani Machupa, Nurdin Msigwa, Emmanuel Gabriel, Moses Odhiambo, Ramadhan Chombo, Haruna Moshi, Uhuru Suleiman, Hilary Echesa, Idi Pazi, Patrick Mafisango, Juma Kaseja, Felix Sunzu, Amri Kiemba.

Kukimbiana
Mechi za Simba na Yanga hazikosi kuwa na vituko, lakini vinavyojulikana zaidi ni kule ‘kukimbiana’ uwanjani ama kwa kutopeleka kabisa timu uwanjani, au kwa kugomea mchezo.
Zifuatazo ni rekodi za timu hizo kukimbiana kwenye Ligi Kuu:
05/11/1966: Mchezo ulivunjika katika dakika ya 75 baada ya Yanga kugoma kumtoa mchezaji wao Awadh Gessani aliyeamriwa atoke nje baada ya kumchezea vibaya yule wa Sunderland. Sunderland wakapewa ushindi na baadaye kuwa bingwa wa taifa kwa mara ya pili. Kabla ya mchezo kuvunjika Yanga ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-0. Nahodha wa Yanga, Mohammed Hussein Hassan ‘Msomali’, alifungiwa na FAT kutocheza mpira kwa miezi 12 na kwamba asipewe cheo cha unahodha, na Awadh Gessani akafungiwa kutocheza mechi tatu. Yanga ikatishia kujitoa kwenye ligi pamoja na African Sports, lakini baadaye timu hizo zikashauriwa kuendelea na ligi.
30/03/1968: Mchezo ulivunjika baada ya mchezaji wa Sunderland, Emmanuel Albert Mbele ‘Dubwi’, kumpiga mwamuzi Jumanne Salum katika dakika ya 20. Wakati huo Yanga ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Kitwana Manara. Mchezo huo ukapangwa kurudiwa Juni Mosi, 1968 ambapo Yanga ilishinda kwa mabao 5-0.
03/03/1969: Sunderland iligoma kabisa kutia mguu uwanjani, hivyo, FAT ikaipa Yanga ubingwa na kuitoza Sunderland faini ya shilingi 500, ambazo hata hivyo, hazikulipwa baada ya kulisuluhisha suala hilo.
18/06/1972: Sunderland iligoma kuingia uwanjani kwa kipindi cha pili kupambana na Yanga huku Yanga ikiwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Leonard Chitete. Huu ulikuwa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Taifa, ambapo Yanga ilipewa ushindi.
10/08/1985: Simba iligomea penati iliyotolewa na mwamuzi Bakari Bendera wa Tanga katika dakika ya 84 baada ya sentahafu wake Twalib Hilal kuunawa mpira katika eneo la hatari. FAT ikaipa Yanga ushindi na kuwa bingwa wa Tanzania Bara.
26/08/1992: Yanga ilikataa kutia timu uwanjani kucheza na Simba katika mchezo wa marudiano wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara kwa kuwa tayari ilikwishatwaa ubingwa. Simba ikapewa ushindi na kisha FAT ikaipiga Yanga faini ya shilingi 250,000 ambazo zililipwa na Murtazar Dewji aliyekuwa amejiunga na timu hiyo akitokea Pan African.
25/02/1996: Simba iligoma kupeleka timu uwanjani baada ya FAT kukataa ombi lao la kuahirisha mchezo huo kwa kuwa ilikuwa inajiandaa na mechi ya Kombe la Washindi dhidi ya Chapungu FC ya Zambia, ambayo hata hivyo, haikuja kabisa. Yanga ikapewa ushindi.

Msimamo kamili
Yanga 76 29 25 22 86 – 75
Simba 76 22 25 29 75 - 86

Comments