Featured Post

KWA HERI TENGA TFF, HAKUNA ASIYEJUA ‘KUKUNJA CHAPATI’

Na Daniel Mbega
LEO hii ulimwengu wa soka unasikilizia matokeo ya uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF)unaofanyika kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront jijini Dar es Salaam.
Kufanyika kwa uchaguzi huu ni mafanikio mengine ya kuondoa sintofahamu iliyokuwepo baada ya kuahirishwa mara kadhaa kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za wagombea kukata rufaa FIFA kupinga kuenguliwa.
Lakini sasa mambo yote yako sawa na jana TFF ilifanya Mkutano wake Mkuu kabla ya kuelekea uchaguzi huu wa leo.
Rais anayemaliza muda wake, Leodegar Chillah Tenga, ameendelea kuiweka rekodi yake safi katika soka la Tanzania tangu alipokuwa anacheza soka na hata kuiongoza Taifa Stars kwenye Kombe la Mataifa Afrika kule Lagos, Nigeria mwaka 1980.
Tumeona mafanikio mengi katika miaka nane aliyokuwepo madarakani, ingawa wapo watu ambao wanaendelea kubeza. Duniani hakuna anayeweza kuridhika kwa asilimia 100, hivyo ni mambo ya kawaida kabisa haya.
Soka lililokosa mwelekeo wakati wa iliyokuwa FAT lilibadilika ghafla tangu mwaka 2004 TFF ilipoundwa na uongozi mpya kushika madaraka.
Kitu pekee ambacho kimeonekana kuwa dhahiri ni kwamba, uongozi wa soka sasa unashikiliwa na wanaoujua mchezo wenyewe, tofauti na miaka ile ambapo yeyote mwenye ushawishi – wa fedha na maneno – aliweza kuongoza hata kama haweza kupiga danadana mpira.
Wagombe wa nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa leo ni Athuman Jumanne Nyamlani na Jamal Emily Malinzi (Rais), Imani Omari Madega, Ramadhan Omar Nassib na Wallace Karia (Makamu wa Rais).
Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Kalilo Samson (Kanda namba 1- Geita na Kagera), Jumbe Odessa Magati, Mugisha Galibona, Samwel Nyalla na Vedastus Lufano (Kanda namba 2- Mara na Mwanza), Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Kanda namba 3- Shinyanga na Simiyu).
Ali Mtumwa, Elley Simon Mbise na Omar Walii Ali (Kanda namba 4- Arusha na Manyara), Ahmed Idd Mgoyi na Yusuf Hamis Kitumbo (Kanda namba 5- Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo na Blassy Mghube Kiondo (Kanda namba 6- Katavi na Rukwa), Ayoub Shaibu Nyenzi, David Samson Lugenge, John Exavery Kiteve, Lusekelo Elias Mwanjala (Kanda namba 7- Iringa na Mbeya).
James Patrick Mhagama na Stanley William Lugenge (Kanda namba 8- Njombe na Ruvuma), Athuman Kingombe Kambi, Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder (Kanda namba 9- Lindi na Mtwara), Hussein Zuberi Mwamba, Stewart Ernest Masima, Charles Komba (Kanda namba 10- Dodoma na Singida), Farid Nahdi, Geofrey Irick Nyange, Juma Abbas Pinto, Riziki Juma Majala) na Twahil Twaha Njoki (Kanda namba 11- Morogoro na Pwani).
Davis Elisa Mosha, Khalid Abdallah Mohamed (Kanda namba 12- Kilimanjaro na Pwani), Alex Crispine Kamuzelya, Kidao Wilfred Mzigama, Muhsin Said Balhabou na Omary Isack Abdulkadir (Kanda namba 13- Dar es Salaam).
Ukiitazama orodha hiyo utaona na kukubali kwamba ‘hakuna siyejua kukunja chapati’, yaani wote wanaujua mpira. Tena hakuna ‘mwenye tongotongo’, wote wanauelewa uongozi.
Nitawakumbusha kidogo kisa cha Ukiwaona Ramadhani Mwinshehe Omari Ditopile wa Mzuzuri na Luta Nelson mwaka 1994. Luta alikuwa anawania uenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Dito alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Wakati wa kufungua mkutano wa uchaguzi, Dito akawataka wajumbe wasiwachague ‘watu wasiojua kukunja chapatti, na ambao tongotongo hazijawatoka’. Luta akasema amedhalilishwa na kutukanwa na ndiyo maana alishindwa ushaguzi ule, akaenda mahakamani. Baadaye yalikwisha lakini.
Naam. Uongozi wa soka kwa sasa siyo sehemu ya majaribio, wala hauhitaji kumtazama mtu usoni ili umchague, bali unazingatia sifa na uwezo (merit and ability).
Pamoja na hayo, TFF kama zilivyo taasisi nyingine za umma, inazingatia uzalendo na maadili kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi yetu. Ndiyo maana hata mchakato mzima ulikuwa mrefu na wagombea wengine walijikuta wakitupwa nje kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za uraia.
Wageni wengi wanajificha kwenye michezo ambako, kama ilivyo kwenye vyama vya siasa ambako hakuna mkaguzi, wanadhani wanaweza kufanikisha mambo yao bila matatizo.
Tukumbuke ile kashfa ya Alhaj Omar Juma ya mwaka 1994. Ilikuwa aibu kubwa siyo kwa familia ya soka tu, bali kwa taifa zima kwa ujumla. Yawezekana wengi wameisahau, nitawakumbusha:
Wakati ligi ya Tanzania Bara ikielekea ukingoni, FAT ilikumbwa na kashfa kubwa baada ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Alhaj Omar Juma kufukuzwa nchini kutokana na kuwa na uraia bandia wa Tanzania. Taarifa iliyotolewa Ijumaa Agosti 5, 1994 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Augustine Lyatonga Mrema, ilisema kuwa kiongozi huyo wa FAT alikuwa akiishi nchini kwa njia za udanganyifu akiwa raia wa Kenya. Taarifa hiyo ilisema kwamba Alhaj Omar Juma alifukuzwa mara moja nchini kwa kuwa ni mgeni mkazi asiye mwaminifu na alitakiwa kuirudisha mara moja pasipoti ya Tanzania yenye nambari A 0047788 iliyotolewa Agosti 17, 1992 kwa kuwa aliipata isivyo halali na kuishi kwake Tanzania hakukuwa halali pia.
Taarifa kamili ya Serikali iliyotiwa saini na Waziri Mrema ni kama ifuatavyo: "Taarifa hii inamhusu Alhaj Omar Juma raia wa Kenya ambaye kwa miaka mingi sasa ameishi hapa Tanzania kwa kutumia uraia bandia wa Tanzania ambao aliupata kwa njia za udanganyifu.
"Alhaj Omar Juma baada ya kuingia Tanzania kwa nyakati tofauti alitumia mbinu mbalimbali kuupata uraia wa Tanzania na katika kufanya hivyo mara zote ametoa taarifa zenye kudanganya ambazo baada ya uchunguzi wa kina na wa muda mrefu, ukweli halisi kumhusu umedhihirika. Pamoja na kuingia kwake Tanzania kama mgeni na hata baada ya kupata vibali vya kufanya kazi akiwa mgeni kutoka Kenya, amekuwa kwa wakati wote siyo raia mgeni mwaminifu. Utaratibu wa mgeni kupata uraia wa Tanzania kisheria upo wazi na taratibu zake zinaeleweka wazi. Hakuna wakati wowote ule ambapo Alhaj Omar Juma alifuata utaratibu huo wa kuomba uraia wa Tanzania. Maelezo yafuatayo yanadhihirisha ukweli wa mambo ulivyo:-
*Alhaj Omar Juma alizaliwa Nairobi, Kenya tarehe 15/3/1949 na alijulikana kwa jina la Peter Kinyanjui. Mama yake anaitwa Elizabeth Wanjiku au Mary Kinyanjui, ambaye ni Mkikuyu na mzaliwa wa Kenya. Anaishi Mathare North, Thika Road, Nairobi. Haijulikani baba yake hasa alizaliwa wapi, lakini kwa mujibu wa kiapo ambacho Alhaj Omar Juma alikiwakilisha Uhamiaji wakati akiomba pasipoti, kinaonyesha baba yake alizaliwa Mafia mwaka 1921. Kwa maana hii Alhaj Omar Juma alikuwa raia wa Kenya na Tanzania hadi alipotimiza miaka 18.
* Alhaj Omar Juma aliingia Tanzania kwa mara ya kwanza tarehe 15/4/1970 kwa matembezi akitokea nchini Kenya. Aliondoka na kurejea tena Tanzania tarehe 15/4/1971 kuja kufunga ndoa na Bi Eshe Abbas Max ambaye walifahamiana Nairobi wakati binti huyo alipokuwa akifanya kazi ya Air Hostess katika Shirika la Ndege la Afrika Mashariki. Baada ya ndoa hiyo alirudi Nairobi. Mwaka 1972 alikuja tena Tanzania akiwa Disco Joker (DJ) baada ya kukodiwa na Frank Marealle aliyekuwa anamiliki Hoteli ya Sea View jijini Dar es Salaam. Wakati huo alijulikana kwa jina la Mc-Twist. Baadaye aliondoka kurudi Nairobi.
* Mnamo Septemba 1975 aliingia nchini Tanzania baada ya kutoroka kutoka Kenya kutokana na matatizo anayoyafahamu mwenyewe.
* Agosti, 1980 aliwasilisha maombi ya pasipoti katika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji yaliyoambatana na Hati ya Viapo (Affidavits) zikionyesha kuwa jina lake ni Omar Juma badala ya Peter Kinyanjui na jina lingine la Mc-Twist. Hakuna ushahidi ulioonyesha kuwa alibadili dini au alikuwa amebadili jina kwa taratibu za kisheria (Deed Poll). Hati hizo zinaonyesha kuwa Alhaj Omar Juma alizaliwa Nairobi, Kenya 15/3/1949, na baba yake aitwaye Juma Omar alizaliwa Mafia, Tanzania mwaka 1921. Hati hizo alipatiwa na mtu aitwaye Hassan Ahmed. Alipohojiwa na maofisa Uhamiaji Alhaj Omar Juma alidai kuwa baba yake alizaliwa Mikindani, Mtwara mwaka 1910 na kuwa baba yake yu hai na anaishi Nairobi. Kutofautiana kwa tarifa hizi kunadhihirisha udanganyifu aliokuwa akiuendeleza. Kiutaratibu hapa aliyepaswa kumwapia ni baba yake mzazi na viapo hivyo vingetolewa kutoka kwa mahakama za Nairobi, Kenya siyo Tanzania.
"Kutokana na viapo hivyo alijipatia pasipoti za Tanzania Na. 111366 ya Agosti, 1980, Na. 161011 ya 11/6/1983, Na. 247766 ya 30/8/1989 na Na. A0047788 ya 17/8/1992 zote zikiwa zimetolewa kwa kuzingatia udanganyifu alioufanya Alhaj Omar Juma.
"Kwa kuzingatia sheria, Omar Juma alikuwa raia wa Kenya kwa kuzaliwa na ule wa Tanzania kwa kurithi (by descent) kama kweli baba yake alikuwa mzaliwa wa Tanzania. Aidha, kwa misingi ya sheria ya uraia wa Tanzania Alhaj Omar Juma alipaswa kuukana uraia mmojawapo kati ya ule wa Kenya (kuzaliwa) au ule wa Tanzania (kurithi) alipotimiza miaka 18 kwa kuwa sheria haziruhusu uraia wa nchi mbili (Dual Nationality). Jambo hili hakulifanya na hivyo aliupoteza uraia wa Tanzania kwa mujibu wa sheria. Alitimiza umri wa miaka 18 tarehe 14/3/1967.
"Kutokana na maelezo haya Alhaj Omar Juma au Peter Kinyanjui au Mc Twist siyo raia wa Tanzania na wala siyo mgeni mwaminifu. Serikali ya Tanzania imefikia uamuzi wa kuifuta pasipoti yake Na. A0047788 iliyotolewa tarehe 17/8/1992 kwa Alhaj Omar Juma isivyo halali. Aidha, Serikali imeamua kumfukuza Alhaj Omar Juma kutoka nchini mara moja kwa kuwa kuishi kwake Tanzania siyo halali."
Ilikuja kufahamika baadaye kwamba, Peter Kinyanjui ndiye aliyehusika na mauaji ya Mbunge maarufu wa Kenya, Joshua Mwangi Kariuki 'JM' mwaka 1975 na baada ya mauaji hayo na Polisi wa Kenya walipompokea mpakani wakasema kwamba watafanya uchunguzi, ikibainika kama ndiye aliyehusika na mauaji ya Mbunge huyo aliyekuwa kipenzi cha wengi, basi angefikishwa mikononi mwa sheria.

Comments