Featured Post

HEMEDI MANETI ULAYA 'CHIRIKU'

Hemedi Maneti Ulaya. Picha kwa hisani ya issamichuziblog.
Kikosi kamili cha Vijana Jazz enzi hizo. Picha kwa hisani ya blog ya John Kitime. 
 Na Daniel Mbega
"...Ni wewe Maria Maria wangu, ni wewe wa kufa na kuzikana eeh
Angalia pendo langu kwakooo, nakuomba ulitunze pendooo
Akili zimeniruka Manetiii..."
Hayo ni baadhi tu ya maneno yaliyomo katika kibao cha Mary Maria kikiwa moja ya vibao vingi mno vya al-marhum Hemedi Maneti Ulaya 'Chiriku' aliyeipandisha chati Vijana Orchestra tangu alipojiunga nayo hadi mauti yalipomfika hapo mwaka 1990.
Ilikuwa Mei 31,1990 saa 11 jioni wakati Tanzania ilipopata pigo kubwa la kuondokewa na mmoja wa wanamuziki wake mashuhuri, Hemedi Maneti, ambaye alifariki katika Hosipitali ya Mwananyamala, Jijini Dar es Salam baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Ingawa ni miaka mingi imepita akiwa ndani ya kinywa cha ardhi, lakini sauti yake kila isikikapo huonyesha ni jinsi gani mwanamuziki huyo alivyokuwa mtunzi na mwimbaji mkubwa mwenye kipaji cha aina yake.
Maneti ambaye alikuwa kiongozi na mwimbaji wa Vijana Orchestra kwa karibu miaka 16 aliacha pengo kubwa siyo kwa bendi yake tu, bali kwa taifa zima, ambalo bado lilikuwa likiuhitaji mchango wake kwa hali na mali.
Maneti, aliyezaliwa katika kijiji cha Mamboleo, wilayani Muheza, Tanga mwaka 1954, alizikwa kijijini kwake baada ya umati mkubwa wa mashabiki na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi na serikali yake kutoa heshima zao za mwisho.
Kama ndoto za mashabiki zilivyokuwa juu ya wasiwasi wao, pengo la mwanamuziki huyo lilionekana dhahiri katika maonyesho ya bendi, jambo lililochukua muda mrefu kabla wanamuziki hawajajiweka sawa na kumudu, japo kwa kiasi kidogo, kuliziba ingawa umuhimu wa marehemu Maneti katika bendi hadi sasa bado unaonekana.

ALIKUWA MWANASIASA...
Kipaji cha utunzi na uimbaji alichojaliwa na Al-Qudusi kilionekana wazi katika tunzi zake maridhawa. Kuna msururu mrefu wa sifa na mchango mkubwa alioutoa marehemu Maneti katika mambo mbalimbali kupitia sanaa ya muziki.
Unaweza kusema kwamba, kwa vile bendi ya Vijana Orchestra ilikuwa, na bado, inamilikiwa na Umoja wa Vijana wa CCM, ndiyo sababu Maneti alikuwa akiimba nyimbo za siasa. Lakini ukweli unabaki wazi kwamba, mwanamuziki huyo alikuwa mwanasiasa safi ambaye hakuhutubia kwenye mikutano ya siasa, bali aliuonyesha uanasiasa wake kupitia jukwaa la muziki.
Maneti alitunga nyimbo nyingi za siasa na moja kati ya kazi zake bora ni ule wimbo wa Ally Hassan Mwinyi apewe kura za Ndiyo alioutunga mwaka 1985 katika kumpigia debe aliyekuwa mgombea pekee wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano kwa wakati huo, Rais Mstaafu wa pili Alhaji Ally Hassan Mwinyi.
Wimbo huo ulipigwa kila siku na Redio Tanzania na kutokea kupendwa sana na watu wakiwemo viongozi wa kisiasa, na ubora wa wimbo ulionekana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1990 pale bendi yake ya Vijana ilipoukarabati na kuutumia tena kwenye kampeni za Rais Mwinyi na Rais wa Zanzibar, Dakta Salmin Amour Juma.
Aidha, Maneti hakuwa nyuma katika masuala ya ukombozi pamoja na kutetea amani na alidhihirisha wazi kwamba ni mtetezi wa amani alipotunga wimbo safi wa Magaidi wa Msumbiji mwaka 1987. Wimbo huu pia ulitokea kuwa kipenzi cha watu na ni moja kati ya kazi za kukumbukwa.
Nyimbo nyingine za siasa ni Muungano umekamilika, Rushwa adui wa haki, Vijana nguzo na jeuri ya Chama, Operesheni Maduka, Mwenge umulike nje ya mipaka ya Tanzania, Tamasha la Vijana Moshi na nyinginezo nyingi.

...KATIKA MAPENZI
Mwanamuziki huyo alionyesha kipaji chake pia katika tunzi za mapenzi kiasi kwamba vibao vyake vingi bado vinawakuna wengi hadi sasa. Miongoni mwa vibao alivyotunga, na vingine kutungiwa na kuviimba, ni kama Niliruka ukuta (sehemu ya I na II mwaka 1975), Mary Maria, Maggy wanipa mateso, Kosa la Wazazi, Chiku saizi yangu, Ilikuwa lifti tu, Aza, Pili wangu nihurumie (ulitungwa na Abdallah Mensah), Penzi halina umaarufu, Penzi haligawanyiki I na II, Heshima ya mtu kuoa na kuolewa, Chaurembo na nyinginezo.
Pia aliimba nyimbo nyingi  za kijamii kama vile Masimango, Mwanaume gani anasuka nywele, Nsabi, Kamata Ooh Sukuma, Matata Matata, Watoto wanalia sana, Mudinde acha fitina, Ooh Masido, Amba kawa baharia, Acha acha ngoma Jirekebisheni, Wifi zangu, Wajue wana Koka, Bujumbura na Safari yetu Zambia ambao haukurekodiwa.
Maneti hakuwa mwanamuziki wa kubahatisha wala kubabaika. Alikuwa ni mvumilivu na wala hakubweteka na umaarufu kwa muda wote aliokuwa na Vijana Orchestra. Hakujaribu hata siku moja kuihama bendi hiyo.
Wanamuziki wengi walikuwa wakiingia bendi hiyo na kutoka, lakini kamwe Maneti hakutingishika licha ya vishawishi vingi kutoka bendi kadhaa za hapa nchini ambazo zilikuwa zikimtafuta kila kukicha.
Alijiunga na bendi ya Vijana Orchestra mwaka 1974 akitokea katika bendi ya TK Lumpopo iliyokuwa ikiongozwa na mwanamuziki mkongwe nchini, Juma Kilaza, ambaye ni shemeji yake, na tangu alipoingia Vijana akapewa uongozi msaidizi wa bendi hadi mwaka 1982 alipoteuliwa kuwa kiongozi wa bendi.
Katika kuwepo kwake kwenye bendi ya Vijana, bendi hiyo iliweza kupitia kwenye mitindo mingi na mingi kati ya hiyo ikiwa ni ubunifu wake. Mitindo hiyo ni kama vile Takatuka (ambao aliukuta), Koka Koka, Heka Heka, Pamba moto I na II na Pamba Moto Shambulia 'Hot Dance', jambo lililopelekea kurundikiwa shehena ya majina yakiwemo ‘Simba Mwendapole’ na ‘Chiriku’, jina ambalo lilimkaa mpaka likaonekana kama moja ya majina yake halisi. Pia aliweza kupitia ngazi kadhaa za uongozi katika siasa kama mjumbe wa Baraza la Utekelezaji la Taifa la Umoja wa Vijana wa CCM.
Kutokana na uongozi wake imara bendi hiyo haikuyumba chini yake hata pale wanamuziki wake nyota walipokuwa wakihama. Baadhi ya wanamuziki ambao waliihama bendi hiyo katika vipindi tofauti na kusababisha mapengo makubwa katika bendi hiyo ni kama vile Cosmas Thobias Chidumule, George Mpupua, Hassan Dalali, Komandoo Hamza Kalala ambaye aliondoka na baadaye kurejea tena kabla ya kuihama tena na kwenda Washirika Tanzania Stars 'Watunjatanjata' pamoja na Eddy Sheggy na Adam Bakari 'Sauti ya Zege' waliokuwa nyota katika bendi hiyo.
Wengine ni Athumani Momba, Jerry Nashon 'Dudumizi', Mohammed Gotagota, Msafiri Haroub ambao nao, kama Kalala, waliihama bendi hiyo na kurejea tena, Kida Waziri na Mohammed Shaweji.
Maneti bado anakumbukwa ambapo baadhi ya wanamuziki waliokuwa naye akiwemo Rashid Pembe, waliwahi kukiri kuwa pengo aliloliacha Maneti.

...WANAMUENZI?
Kipindi cha miaka ya 1990 baadhi ya wanamuziki waliokuwa wanaunda Vijana Jazz walikuwa na utamaduni kutembelea kaburi la Maneti kila mwaka kijijini Mamboleo ikiwa ni pamoja na kuwajulia hali wazee na ndugu wa marehemu, lakini kwa sasa hali hiyo imetoweka, pengine kutokana na bendi hiyo kusuasua ambapo kwa sasa ipo kama haipo.
Vile vile wengi kati ya wanamuziki waliokuwa pamoja na Maneti wamekwishafariki dunia kama Edson Shekabughe 'Eddy Sheggy', Suleiman Mbwembwe, Adam Bakari, Jerry Nashon 'Dudumizi', Mohammed Gotagota, Msafiri Haroub, na wengineo.
Mwaka 1994 bendi hiyo, baada ya kupigiwa kelele sana na mwandishi mmoja mkongwe wa burudani, ilitoa albam ya Kumbukumbu ya Maneti iliyoitwa Homege de Maneti ambayo ilikuwa na baadhi ya nyimbo zilizotamba enzi za uhai wake.
Mwenyezi Mungu azidi kukung'arishia nuru huko uliko. AMINA.
 Tazama mashairi ya kibao cha Mary Maria:

Mary Maria Maneti: [Mary!!! Maria eee!! Angalia ninavyoteseka juu yako Maria, 
Wala usingizi sipati juu yako Maria, wasikilize awamu ya pili wanavyolia juu yako Maria] 

Kwa kweli sasa nimenaswa, Sina ujanja eeeh eeeh, 
Sina ujanja eehhh 
Kupenda sawa na ajali, Haina kinga eeh eeh 
Haina kinga eeh 

Nilivyomuhusudu mtoto Mary sijapata kupenda toka nizaliweeeee 
Na wala sitapenda mpaka nife, 
Mpaka nife, mama Mary eeeh 

Nasononeka oooh mama, nasononeka, 
Ninateseka ooh mama, ninateseka, 
Aaaah nimezama kwenye dimbwi 
Oooh la mapenzi x2 

Aiya yaya Maria wangu (Maria wangu) 
Aiya yaya Maria ooooh Maria (I love you) 

Ni wewe Maria, Maria wangu 
Ni wewe wa kufa na kuzikana eeeh 
Hakuna mwingine zaidi yako 

Angalia penzi langu kwakoooo 
Nitakuwa wa milele Manetiiii 
Nakuomba ulitunze penziiiii 

Ni wewe Maria, Maria wangu 
Ni wewe wa kufa na kuzikana eeeh 
Hakuna mwingine zaidi yako ayaya 

Aiya yaya Maria wangu (Maria wangu) 
Aiya yaya Maria ooooh Maria (I love you)

Awamu ya pili, pamba moto! 
(Rudi mwanzo)

Comments