Featured Post

FERGUSON AITABIRIA MAN UNITED UBINGWA



BOSI wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amesema timu hiyo inaweza kubadilika na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuanza vibaya msimu, pamoja na kuwa nyuma kwa pointi nane dhidi ya vinara Arsenal.
Ushindi wa mechi mbili kati ya tatu zilizopita unamaanisha kikosi hicho cha David Moyes kimerejea kwenye fomu baada ya kuanza vibaya yakiwa ni matokeo mabovu zaidi katika miaka 14 iliyopita.
Ferguson, 71, alisema: "Tumekuwa tukianza vibaya msimu mara nyingi. Sisi ndiyo klabu pekee kwenye ligi ambayo inaweza kuanza vibaya na kutwaa ubingwa kwa sababu ya historia yetu."
Ferguson, ambaye kwa sasa ni mkurugenzi wa klabu, alijiuzulu ukocha mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kutwaa mataji 38 katika miaka 27 aliyokaa Old Trafford.
Na Moyes amekuwa akihangaika kupata sapoti ya baadhi ya mashabiki baada ya kuanza vibaya kasi hiyo ndani ya Man U.
Lakini akizungumza katika kipindi cha maswali na majibu kwa mara ya kwanza baada ya kutoa kitabu cha pili cha wasifu wake, Ferguson alielezea changamoto zinazotokea kwenye kazi hiyo.
Pia alitetea sababu zake za kuchapisha kitabu ambamo aliwalashutumu wachezaji wa zamani kama Roy Keane na David Beckham, akiongeza kwamba "inashangaza" kwamba alikuwa na "masuala sita tu na wachezaji" wakati alipokuwa Old Trafford.
"Niliandika kitabu kwa ajili ya mashabiki, kuwasaidia kuelewa kwa nini nililazimika kufanya uamuzi fulani," alisema.
"Haikuwa kwa ajili ya vyombo vya habari, kilikuwa ni kitabu kilicholenga kuwasaidia watu kuelewa jinsi ilivyo vigumu kufanya kazi Manchester United. Ni kazi kubwa, ndiyo kubwa zaidi duniani"
CHANZO: BBC

Comments