Featured Post

AZAM MBABE WA SIMBA, YANGA

TIMU ya Azam imeendeleza ubabe kwa timu kongwe nchini, baada ya leo kuitungua Simba mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. 
Kabla ya mechi ya leo, Azam walitoa kipigo cha 3-2 kwa Yanga katika mechi nyingine ya Ligi Kuu iliyochezwa Septemba 22, wakidhirisha uwezo chini ya kocha wake Stewart John Hall, raia wa Uingereza.
Ushindi huo umeiwezesha Azam iliyomaliza nafasi ya pili msimu uliopita, hivyo kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho, kufikisha pointi 23, ikiongoza ligi hiyo inayoshindanisha timu 14.
Simba walianza mechi kwa kasi na kutangulia kupata bao katika dakika 20 likifungwa na Ramadhan Singano ‘Messi,’ aliyezima na kupiga baada ya kupokea krosi iliyopigwa na Zahoro Pazi, bao ambalo liliongeza kasi ya mchezo kwani wakati Simba wakitaka kuongeza, Azam walipambana kusawazisha.
Dakika mbili kabla ya filimbi ya mapumziko, juhudi za Azam zilizaa matunda baada ya Kipre Tchetche kuisawazishia bao Azam kutokana na juhudi kubwa ya Erasto Nyoni, hivyo timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Katika kipindi cha pili, Azam walikianza kwa kasi ya mashambulizi ambapo dakika ya 63 nusura wapate bao, lakini John Bocco alishindwa kuitendea haki krosi ya Kipre licha ya kubaki na nyavu baada ya kipa Abel Dhaira kupotezwa na krosi hiyo.
Dakika ya 73, Kipre alirejea katika nyavu za Simba na kuifungia Azam bao la pili kutokana na juhudi binafsi akimlamba chenga beki William Lucian kabla ya kumtungua Dhaira kupitia nyavu ndogo, ikiwa ni dakika moja tu tangu Sino Augustino wa Simba apoteze nafasi ya wazi ya kufunga.
Licha ya Simba kupambana kuepuka kichapo, hadi mwamuzi Oden Mbaga anamaliza mchezo, Simba walitoka vichwa chini kwa mabao 2-1.
Simba: Abel Dhaira, William Lucian, Issa Rashid, Joseph Owino, Hassan Khatib, Jonas Mkude/Edward Christopher, Ramadhan Singano, Saidi Ndemla, Betram Mwombeki, Zahoro Pazi/Sino Augustino na Amri Kiemba.
Azam: Mwadini Ali, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Aggrey Morris, Said Moradi/Steven Mwantika, Kipre Balou, Kipre Tchetche, Aboubakar Salum ‘Sure boy’, John Bocco, Humphrey Mieno/ Khamis Mcha na Joseph Kimwaga.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mabingwa watetezi, Yanga kucheza na Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ambapo wenyeji watakuwa wakipigania ushindi ili kufikisha pointi 22, hivyo kufukuzana kwa karibu na Azam.
Katika mechi ya kesho, Yanga watamkosa nyota wake mahiri, Haruna Niyonzima, aliyekwenda kwao Rwanda tangu juzi kutokana na matatizo ya kifamilia kabla ya kurejea kesho kutwa kuelekea mechi ya Ijumaa dhidi ya maafande wa JKT Ruvu wa mkoani Pwani.
Ligi hiyo itaendelea katika uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kwa wageni katika ligi hiyo, Mbeya City kucheza na Tanzania Prisons katika mechi inayokutanisha timu za mkoa mmoja, hivyo kugubikwa na ushindani wenye sura ya utani wa jadi.
Mbeya City iliyoonesha makali ya aina yake tangu kuanza kwa msimu huu, wanaingia dimbani wakiwa na pointi 20, kusaka ushindi kuendelea kukabana vikali na Azam kwa tofauti ya mabao huku Prisons wakiwa na pointi nane pekee.
Vita nyingine ya ligi hiyo kesho itakuwa Uwanja wa Ali Hassani Mwinyi, mjini Tabora kwa Rhino Rangers kuwaalika JKT Ruvu ya Pwani katika mechi inayotarajiwa kuwa yenye ushindani mkubwa kutokana na mazingira ya timu hizo.

Comments