- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
FURSA NYINGINE YA SCHOLARSHIP YAJA: SHULE ZA SEKONDARI ZATAKIWA KUTUMA MAOMBI SASA KUSHIRIKI MAONYESHO YA SAYANSI YA YST 2018!
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Profesa Simon Msanjila
akikabidhi zawadi kwa Prosper Gasper na Erick Simon kutoka Shule ya Sekondari
St. Jude's jijini Arusha baada ya kuibuka washindi wa jumla wa Mashindano ya
Wanasayansi Chipukizi (YST) yaliyofanyika leo yaliyofanyika katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
SHULE za Sekondari nchini Tanzania zimetakiwa
kuanza kutuma maombi sasa ili kupata fursa ya kushiriki katika Maonyesho ya 8
ya Sayansi kwa wanafunzi yanayoandaliwa na Shirika la Young Scientists Tanzania
(YST) kila mwaka.
Taarifa kutoka YST zimeeleza kwamba, maonyesho
hayo ni kwa wanafunzi wa kuanzia kidato za kwanza hadi cha sita kwa shule zote
za sekondari – za umma na binafsi – zilizoko nchini.
“Mwisho wa kutuma maombi ni Machi 31, 2018 na
maonyesho hayo yatafanyika jijini Dar es Salaam mwezi Agosti,” imesema taarifa
hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kwamba, kutuma mapema
maombi kutasaidia hata zoezi la mchujo ili kuwapata washiriki wenye mawazo
yatakayoleta ushindani pamoja na ubunifu kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia
nchini Tanzania.
Jumla ya mawazo 100 yanatarajiwa kushindanishwa
mwaka huu ambapo washindi katika vitengo mbalimbali watapatiwa zawadi za fedha
pamoja na ufadhili wa masomo ya chuo kikuu.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, wanafunzi Prosper Gasper
na Erick Simon wa shule ya Sekondari ya St. Jude’s kutoka Arusha, ndio walioibuka
mabingwa wa jumla wa sayansi katika Maonyesho
ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania 2017 kutokana na wazo lao la “Kutumia
Simu za Mkononi kama Mfumo wa Kubaini Ajali za Moto” (The Use of Mobile
Network as a Fire Alert System).
Kwa ushindi huo, mbali ya kutunukiwa medali na
tuzo, pia walipata kitita cha Shs. 1,800,000 pamoja na udhamini wa masomo yao
hadi elimu ya juu.
Aidha, walipata nafasi kwa mara ya kwanza ya
kushiriki mashindano ya ubunifu wa sayansi na teknolojia yaliyofanyika jijini
Johannesburg, Afrika Kusini mwezi Oktoba 2017 na mwaka huu 2018 watashiriki
maonyesho ya kimataifa ya sayansi na teknolojia jijini Dublin, Ireland.
Kumekuwepo na ongezeko kubwa la ushiriki wa
shule za sekondari kutoka shule 4 mwaka 2011 hadi 100, hatua ambayo imetokana
na hamasa ya kuendeleza masomo ya sayansi kwa shule mbalimbali za sekondari
nchini.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, uwepo wa maonyesho hayo ya
sayansi kwa wanafunzi usaidia ufaulu wa masomo ya sayansi kwa shule nyingi za
sekondari nchini, mfano mmojawapo ukiwa ni Shule ya Sekondari ya Wasichana
Mtwara.
Katika
matokeo ya kidato cha sita mwaka 2017, kwa mara ya kwanza shule hiyo
ilipata daraja kwa kwanza (Division One) kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi,
jambo ambalo lilikuwa adimu.
Uchunguzi wa MaendeleoVijijini umebaini
kwamba, kwa miaka takriban 10 mchepuo wa masomo ya sayansi, Kemia, Baolojia na
Jiografia (CBG), haujawahi kutoa hata mwanafunzi mmoja aliyepata daraja la
kwanza katika matokeo ya kidato cha sita.
MaendeleoVijijini imegundua kwamba, miaka yote ufaulu mkubwa
wa masomo ya sayansi shuleni hapo umekuwa daraja la pili (division two) ambao
nao haukuwa wa kuridhisha ikilinganishwa na masomo ya sanaa na uchumi, huku
wanaochukua mchepuo wa sayansi ‘wakiongoza’ kwa kupata daraja la nne pamoja na
kupata sufuri.
Kati ya wanafunzi nane waliopata Daraja la
Kwanza mwaka 2017 shuleni hapo, wawili walikuwa wanachukua mchepuo wa sayansi
na kati ya wanafunzi 57 waliopata daraja la pili, 17 wanatoka mchepuo wa
sayansi pia.
Wanafunzi Diana
Sosoka na Nadhra Mresa, ambao walikuwa washindi wa jumla mwaka 2016 katika
maonyesho hayo ya sayansi ya YST nao walionyesha kushangazwa na matokeo hayo.
“Kweli ni maajabu kwa mara ya kwanza kuna
Division One kwenye CBG pale shuleni kwetu, ni mafanikio ambayo yametokana na
hamasa ya kuwepo kwa mashindano haya ya sayansi na sisi tunashukuru kuwa sehemu
ya mafanikio,” anasema Diana.
Diana na Nadhra ambao walipata ushindi kwa
kubuni mashine ya kienyeji ya kutotoresha mayai, pia walipata udhamini wa
masomo ya chuo kikuu kutoka taasisi ya Karimjee
Jivanjee Foundation.
Wote kwa pamoja walikuwa wanachukua mchepuo wa
Kemia, Baolojia na Jiographia (CBG) na kwa bahati nzuri, wote wawili walifaulu.
Imeandaliwa
na www.maendeleovijijini.blogspot.com.
+255 656 331974.
Comments
Post a Comment