- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Bibi wa Kialagwa katika maskani yake huko chini ya Mlima Wasi.
Na Innocent Nganyagwa
NDUGU zangu, nawakaribisheni kwenye safu
yetu ya Asili na Fasili inayotuwezesha kutopea kwenye ujadi wa makabila
yetu mbalimbali hapa nchini.
Basi leo tunawatembelea ndugu zetu Wasi, au
kama wanavyofahamika kwa jina lingine, Waalagwa.
Kwa kupiga hodi kwa ndugu zetu hawa, na tuko
Kondoa huko Dodoma tunapokutana na ndugu zetu hawa wanaozungumza lugha yao ya Chasi.
Utambulisho wa ndugu zetu hawa una utata
kutokana na sababu kadhaa kama nitakavyoeleza.
Kwanza, huwa wanadhaniwa kuwa ni sehemu ya
jamii ya makabila mengine wanayotangamana nayo kwenye eneo moja. Jambo hilo
husababisha kupotoshwa kwa utambulisho wao halisi.
Sababu nyingine ni kutokana na kuhusishwa
na mbari mbili tofauti za Uhamitiki na Ukushi.
Kwa kabila kuhusika na mbari mbili sio
tatizo sana, maana kuna makabila yanatoka moja kwa moja kwenye zile mbari kuu
tano za Afrika.
Lakini pia kuna makabila yanayotokana na
mchanganyiko wa zaidi ya mbari moja, lakini kwa hawa Wasi tutaona kwa kina nini
hasa kinachochanganya utambulisho wao.
Basi ili tuweze kufika huko tuanze kutazama
mambo ya hawa Waalagwa.
Kwanza hawa ndugu zetu ni wachache na ni
moja kati ya makabila madogo hapa nchini, wengi wao bado wanaishi kwenye eneo
lao la nchi ya Ualagwa bila kuhama kutoka eneo hilo.
Majirani zao wa kihistoria walio mkabala
nao ni pamoja na Wamaasai (Wanailotiki), Wasandawe (Wakhoisan), Wairaqw,
Waburunge, Wasi na Wagorowa (Wakushi) na Wambugwe (Wabantu).
Ndugu yangu, kwenye mabano ndizo hizo mbari
kuu tano za Afrika ambazo huwa narudia kuzitaja mara kwa mara, katika kupeana
elimu ya kina kuhusu chanzo cha makabila.
Na tutakapowatembelea Warangi, tutaona
baadhi ya athari za matamshi ya lugha zao kutokana na baadhi ya makabila
majirani zao kugubikwa na lugha yao ya ‘Kilaangi’ (Kirangi).
Halafu lugha hiyo iliporudi tena ndani ya
Kirangi ikawa na zile athari za kimatamshi, mojawapo ya makabila hayo ni
Waburunge na hawa Wasi.
Hilo pia husababisha watu wengi
kutatanishwa na utambulisho wa Waalagwa na kudhania kuwa nao ni sehemu ya jamii
tanzu za Kirangi.
Kadiri tutakavyoendelea kuchambua mambo yao
hawa Waalagwa, tutaona pia sababu nyingine inayosababishwa na mbari yao na
Warangi inavyochangia pia utata huo.
Awali tulipotembelea
kabila la Wairaqw ambao ni Wakushi, tuliona kuwa katika safari yao
iliyowafikisha huko Manyara waliko, walipita mahali tulipo sasa, yaani Kondoa.
Walipoondoka Kondoa walipoishi kwa muda,
Wairaqw waliohamahama ili kukwepa vita waliacha mabaki ya jamii zao kwenye eneo
hilo.
Baadhi ya mabaki hayo yalijumuika na
kuchangia kuwepo kwa makabila ya Waburunge na Wasi, na walipofika karibu na
eneo walilokuwepo walisababisha kuwepo kwa kabila la Wagorowa.
Kwa hiyo, mpaka hapo utaona kuwa kule
kutatanishwa utambulisho wa Wasi kwa kudhani kuwa ni Warangi au Wairaqw,
kunachangiwa pia na hizo mbari mbili za Kikushi na Kihamitiki ambazo makabila
ya Warangi na Wairaqw nayo pia yanatokea humo.
Lakini tukiwaangalia zaidi wao wenyewe, ni
kwamba Wasi wanapatikana katika nchi yao ya Ualagwa yenye vilima vyenye miamba
na mabonde yaliyo katikati ya vilima hivyo.
Vilima hivyo vyenye baadhi ya wanyama pori,
ni chanzo cha nishati kwa matumizi yao ya kila siku kwa kuwapatia kuni.
Nchi ya Ualagwa ina udongo mgumu wenye
asili ya miamba, kutokana na eneo lenyewe lilivyo kijografia.
Katikati ya nchi hiyo ndipo eneo lenye
rutuba zaidi linapopatikana, kutokana na Mto Bubu wenye maji safi kukatiza eneo
hilo.
Maeneo ya mwinuko kwenye vile vilima, kwa
kawaida yana uhaba mkubwa wa maji kutokana na ukame, hali hiyo pia huchangiwa
na uhaba wa mvua.
Kwa kawaida msimu wa mvua za kuaminika
kwenye nchi hiyo ya Ualagwa ni kati ya Desemba na Mei.
Kwa asili, Wasi ni watu kutoka jamii
mchanganyiko za mbari za Kikushi na Kihamitiki.
Kuhusika kwao na mbari hizo mbili ni
kutokana na kuwa na misafara iliyo tofauti na makabila mengi ambayo tutaendelea
kuyachambua kwenye hii safu yetu ya kijadi.
Tofauti hiyo ninayoizungumzia, ni kuwa
mengi ya makabila tutakayoyatembelea tutaona jinsi jamii zao zilivyolowea na
kuweka makazi, baada ya kuzurura hasa kutokea upande wa kaskazini.
Hawakurudi nyuma walikotokea, bali
walitawanyikia maeneo ya pembezoni na kusambaa sehemu mbalimbali baada ya kufika
hapa nchini.
Lakini masalia ya jamii zilizozalisha
kabila la Wasi, yalitoka Iramba-Singida kwenda Mashariki ya Kati miaka mingi
iliyopita.
Kama unaifahamu vyema ramani ilivyo,
utakumbuka kuwa ukipita mashariki ya kati unapoelekea Mashariki ya Mbali lakini
kwa uelekeo wa upande wa Arabuni, huko Saudia, eneo hilo lina kiini cha chanzo
cha mbari ya Kihamitiki. Safari hiyo ya Wasi kurudi kaskazini, ni kinyume na
jamii nyingi zilizokuja huku kutoka kaskazini.
Maana wao walitoka huku kuelekea kaskazini,
lakini walipofika huko hawakuweza kutangamana na wenyeji waliowakuta huko.
Sababu kubwa ni wao kutokuwa na imani kama
za wenyeji waliowakuta, ambao kwa sehemu kubwa walishaukumbatia Uislamu.
Kwa hiyo ndugu zetu Wasi, wakati huo wakiwa
katika zile jamii zao za awali walipofika huko waliendelea kuabudu mizimu ya
mababu zao kwa imani za kijadi zilivyo.
Hilo ndilo lililowafanya wasitangamane na
kuwiana na wale wenyeji wa Mecca, ambako kunafahamika kuwa kiini cha imani ya Uislamu.
Baadaye jamii hizo zikageuza na kuanza kurudi
tena upande huu waliotoka. Katika njia yao wakapitia eneo la Uhabeshi huko
Ethiopia ambako pia Wakushi wanapatikana kwa wingi.
Kukatokea mchanganyiko tena wa mbari, maana
kumbuka kuwa kule walikoenda ni nchi ya Uhamitiki na hapa walipopita ni moja
kati ya nchi za Kikushi.
Ndiyo maana niliwatahadharisha kuwa, kadiri
tutakavyoendelea na mambo ya ndugu zetu hawa tutaona ule utata wa utambulisho
wao kupitia mbari.
Ukiachilia pia kule kubanwa katikati ya
jamii masalia za Warangi (Wahamitiki) na Wairaqw (Wakushi).
Katika kurudi tena hapa nchini, kama
yalivyo makabila mengi yaliyoingia na kuja hadi uwanda wa kutoka kaskazini
magharibi hadi mashariki.
Wakafika Halas’o katikati ya Mlima Hanang’
na Kondoa, wakaishi kwa muda kabla ya kuanza tena safari iliyowafikisha walipo
sasa huko nchi ya Ualagwa-Kondoa.
Eneo hilo walilokaa kwa muda mara kadhaa
hutoa viashirio vya mizimu yao, kwa kusikika sauti za ngoma zao zikipigwa
nyakati za usiku huku watu wakiimba na kucheza bila hao wapigaji na wachezaji
kuonekana. Ni eneo ambalo bado lina nguvu za mizimu yao.
Ndugu yangu, nikufahamishe kuwa hawa
Waalagwa ambao pia huitwa Wasi wana mambo yao yanayotegemea nguvu za kijadi.
Mathalan, walikuwa na kawaida ya kufanya
matambiko ya kuita mvua ukame unapokithiri.
Tambiko la aina hiyo hufanyika chini ya
mti, ambapo majani ya mti husika huchumwa na kusagwa na kupondwa.
Kisha kondoo mweusi huchinjwa na damu yake
hunyunyizwa kwenye yale majani yaliyotapakazwa kuuzunguka ule mti, hivyo damu
ile pia hunyunyizwa kuuzunguka mti huo wa tambiko la kijadi la Kialagwa.
Naam, tumeshapiga hodi kwa ndugu zetu Wasi
(Waalagwa), ambao tutaendelea kuchambua mambo yao kesho.
Makala haya yamehaririwa,
yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Juni 06, 2009.

Comments
Post a Comment